Gari jingine litakalozunguka sayari ya Mars lakamilika

Wanasayansi wakiweka sawa gari la Mars 2020 ambalo litaondoka duniani mwezi Julai kuelekea sayari ya Mars likichukua miezi saba kukamilisha safari hiyo. AFP.

Pasadena, Marekani . Gari litakalotumwa katika sayari ya Mars mwakani lililopewa jina la Mars 2020, halitakuwa likifuatilia maisha ya kale pekee, bali litatayarisha njia kwa binadamu wa kwanza kufanya safari katika sayari hiyo nyekundu, wanasayansi wa NASA walisema juzi wakati wakionyesha chombo hicho kwa waandishi wa habari.

Gari hilo (rover) lenye chumba kikubwa, limeundwa katika maabara ya Jet Propulsion mjini Pasadena, karibu na Los Angeles, ambako vifaa vyake vya kuendeshea vilifanyiwa majaribio wiki iliyopita.

Chombo hicho kitakaa Mars kwa mwaka mmoja kwa mujibu wa muda wa sayari hiyo, ambao kwa duniani ni takriban miaka miwili.

“Tunatakiwa kukifanya chombo hiki kiwe katika hali yake halisi na salama hadi kifike Mars,” alisema David Gruel, meneja wa operesheni ya Mars 2020.

Waandishi walilazimika kupitia utaratibu mrefu wa kuua vijidudu kabla ya kuingia kwenye chumba “kwa hiyo tutaleta sampuli duniani kutoka Mars na si nywele kutoka mwilini mwangu au ngozi kutoka kwa mtu mwingine yeyote,” alisema Gruel.

Brashi za kielektroni zilisafisha viatu kabla ya wageni kufikia chumbani na ili kuzuia uchafuzi waandishi walivalishwa makoti maalum yaliyofungwa kwa gundi na hata pia vilinda ndevu.

Gari hilo lililoonyeshwa kwa waandishi wa habari Ijumaa, linatarajiwa kuondoka duniani mwezi Julai 2020 likitokea Cape Canaveral katika jimbo la Florida, na litakuwa gari la tano la Marekani litakapotua katika ardhi ya Mars miezi saba baadaye, yaani Februari mwaka 2021.

“Limeundwa kupeleleza ishara za uwezekano wa kuwepo na maisha (katika sayari ya Mars), kwa hiyo tunapeleka vifaa kadhaa ambavyo vitatusaidia kuelewa jiolojia na kemikali zilizo katika ardhi ya Mars,” naibu kiongozi wa mradi huo, Matt Wallace aliiambia AFP.

Miongoni mwa vifaa vilivyowekwa kwenye gari hilo ni kamera 23, ‘masikio’ mawili ambayo yatawezesha kusikia mvumo wa upepo katika sayari hiyo, na kifaa cha kuchunguza kemikali.

Kwa ukubwa wa gari hilo, lina matairi sita kama lililotangulia lililoitwa Curiosity, ambayo yataliwezesha kupita katika miamba ya mawe bila ya matatizo.

Kasi si kitu cha muhimu katika gari hilo, ambalo litaweza kutembea kwa kasi ya yadi 200 kwa siku, makisio yanayofanana na mwendo wake likiwa duniani.

Mars 2020 lina mikono ya urefu wa futi saba na chombo cha kutoboa (drill) sampuli za miamba katika maeneo ambayo wanasayansi wameona kuwa kuna uwezekano wa binadamu kuishi.

Maisha ya kale

“Tunachotafuta ni maisha ya kale tunazungumza kuhusu miaka bilioni iliyopita katika Mars, wakati sayari hiyo ilipokuwa inafanana na dunia ya sasa,” alisema Wallace.

“Wakati huo, sayari hiyo nyekundu ilikuwa na ardhi ya maji yenye joto, hali nzito ya hewa na nguvu ya sumaku, alieleza.

“Na kwa hiyo ilikuwa na aina ya mazingira inayofaa kwa maisha ya kiumbe kilicho duniani sasa na kilichokuwepo wakati huo,” alisema Wallace.

Mara baada ya kukusanywa, sampuli hizo zitasindikwa kwenye tyubu na gari hilo.

Baadaye tyubu hizo zitahamishiwa kwenye uso wa dunia ambako zitakaa hadi wakati wa mradi mwingine zitakaposafirishwa kuja duniani.

“Tunategemea kwenda kwa kasi. Tunapenda kuona mradi mwingine ukifanyika mwaka 2026, wakati tutakapokwenda Mars na kuchukua sampuli hizo, kuziweka kwenye roketi na kuzipeleka kwenye uzio wa Mars,” alisema Wallace.

Alisema baadaye sampuli hizo zitasafirishwa kuletwa duniani na kwamba zinatarajiwa kufika katika kipindi cha miaka kumi.