Wabunge Chadema wasimulia walivyopigwa na askari Magereza

Dar es Salaam. Wabunge wawili wa Chadema, Halima Mdee na Ester Bulaya wamesimulia jinsi walivyopigwa na askari Magereza walipokwenda katika Gereza la Segerea kumpokea mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekuwa akitoka jela baada ya kukamilisha taratibu za kulipa faini ya Sh70 milioni.

Wakizungumza jana na Mwananchi katika Hospitali ya Aga Khan walikolazwa, wabunge hao wa Kawe na Bunda wameeleza tangu walipofika katika gereza hilo, walivyoshushwa kwenye magari, kupigwa na kisha kupelekwa Kituo cha Polisi Stakishari walikotoa maelezo na kuachiwa kwa dhamana.

Wakati Mdee akisema amevunjwa mkono wake wa kulia, Bulaya alisema ameelezwa kuwa pingili za mgongo zimetikisika kutokana na kukanyagwa huku Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye pia alikuwa na wabunge hao akieleza hali ilivyokuwa.

Mdee, Bulaya na Jacob pamoja na diwani wa Tabata, Patrick Assenga na Katibu wa Chadema Dar es Salaam Kuu, Henry Kileo ni kati ya watu 27waliokamatwa katika gereza hilo walikoenda kumchukua Mbowe.

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa na mjumbe wa baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Hadija Mwago.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Magereza SSP, Amina Kavirondo alisema, “hakuna mtu aliyepigwa, kilichofanyika walikuwa wakizuiwa kutoingia eneo la Magereza.”

Alisema katika harakati za kudhibiti au kuzuia, anayedhibiti na anayedhibitiwa lolote linaweza kutokea. “Hakuna aliyepigwa, hilo nasisitiza,” aliongeza.

“Magereza ni kama majeshi mengine, nikuulize mwandishi, wanaweza kufanya vile eneo la JWTZ (Jeshi la Wananchi wa Tanzania). Tuliamua kuzuia kwa sababu ndani ya gereza tuna watu zaidi ya 1,000 tunawatunza, tulikuwa tunahakikisha usalama wao,” alisema Kavirondo.

Mapema, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ilala, Zuberi Chembela alisema polisi hawakumpiga mwana Chadema yeyote kwa kuwa hilo si jukumu lao.

“Jukumu la polisi si kupiga watu. Hao wanachama wa Chadema hawajapigwa na polisi labda waseme kuna waliowapiga lakini si polisi,” alisema Chembela.

Mbowe alikuwa kiongozi wa mwisho wa Chadema kutoka jela kati ya viongozi wanane waliohukumiwa kulipa faini ya Sh320 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 ya uchochezi na mkusanyiko usio halali.

Washtakiwa hao walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa faini hiyo hadi fedha hizo zilipochangwa na wananchi.

Baada ya hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Chadema walianza kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi hao.

Walioanza kutoka baada ya Dk Vincent Mashinji wa CCM, ni Mdee, Bulaya na Esther Matiko ambaye ni mbunge wa Tarime Mjini, kisha wakafuata mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika; naibu katibu mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbowe kuhitimisha orodha hiyo.

Alichokisema Mdee

Akionekana kuchoka, Mdee alisema akiwa ndani ya gari nje ya geti la gereza walimfuata askari magereza wengi, “watatu kati yao ninawafahamu na waliniamrisha nishushe kioo.”

“Niliposhusha askari ambao ninawatambua walishika mkono wangu na kuuzungusha. Ni kama walikuwa wanausokota, niliwasikia wakisema ‘ngoja tuuvunje mengine yatafuata baadaye’.” alisema.

Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), alisema askari wa kiume walimshusha kwenye gari na kuanza kumkanyaga, baadaye yeye na wenzake walipelekwa kituo cha polisi Stakishari.

“Licha ya kuvunjwa mkono na nikiwa na maumivu makali nilikaa kituo cha polisi Stakishari hadi saa tatu usiku nilipodhaminiwa,” alisema.

Aliongeza, “wakati tunapokea kipigo askari walikuwa wakisema hawakutaka tutoke walitaka tuendelee kukaa ndani (jela) ili tufanye kazi kama wafungwa wengine.”

Bulaya aeleza alivyopigwa

Huku akieleza jinsi alivyo na maumivu sehemu mbalimbali mwilini, Bulaya alisema baada ya kufika kwenye geti la gereza hilo walikuta askari wakiwa wamejipanga nje ya uzio.

Alisema alijitambulisha kuwa ameleta risiti kutoka Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kumtoa Mbowe lakini waliwazuia.

“Walisema hakuna mtu yoyote kuingia mimi nilimwambia ni mbunge na nilikuwa nimefungwa nimetoka jana (juzi) lakini hawakutaka kunielewa.”

“Ghafla walianza kunipiga na kumfuata Mdee kwenye gari na Jesca (Kishoa) kwa kuwa tulikuwa tunatumia gari moja, wakaanza kutupiga virungu na kutukanyaga kanyaga,” alisema Bulaya.

Aliongeza, “wakati tunachezea kipigo walikuwa wanasema hawakutaka tutoke, walitaka tuendelee kukaa gerezani tufanye kazi, wakawa wanasema eti kwa nini tulichangiwa faini na kutoka.”

Alisema baada ya kupigwa sana alianza kujisikia vibaya na kupelekwa katika zahanati iliyopo karibu na gereza hilo, “baadaye waliomba rufaa kwenda hospitali ya Amana nikiwa chini ya ulinzi hadi nilipodhaminiwa.”

“Hapa (Aga Khan) nimeletwa leo (jana) kutoka Amana lakini hata wakati nikiwa pale nilikuwa chini ya ulinzi na walininyang’anya taarifa ya polisi (PF3).”

Alisema waliopigwa ni wengi wakiwamo viongozi wa Chadema, madiwani na Meya Jacob.

“Cha kushangaza zaidi kama tulipaniwa. Hatukupewa amri ya kutawanyika. Katika hali ya kawaida mtu huwezi kwenda Magereza kufanya fujo. Pamoja na hali yangu kuwa mbaya na kudhaminiwa nikiwa hospitali, nimetakiwa kuripoti tena polisi siku ya Jumatatu,” alisema Bulaya.

Kuhusu vipimo, Bulaya alisema uchunguzi wa awali unaonyesha pingili za mgongo zimetikisika kutokana na kipigo na kukanyagwa.

“Mimi, Mdee na Kishoa tulikuwa tunatumia gari moja baada ya kipigo waliyachukua magari yote na kuyaingiza ndani hadi tulipopata dhamana wakaruhusu yachukuliwe,” alisema.

Kauli ya Jacob

Akisimulia tukio hilo alisema juzi saa 6 mchana alipigiwa simu na wakili Fredrick Kihwelo kuwa amekamilisha taratibu za kimahakama za kumtoa gerezani Mbowe na kuwataka wakutane Gereza la Segerea.

Alisema walikwenda na magari matatu ambapo Mdee na Bulaya walipanda gari moja.

“Tulipofika getini, gari la Mdee na Bulaya lilikuwa limesimama na kulikuwa na mzozo kati ya askari wa getini na kina Bulaya. Sasa walipoanza kugeuza, wale askari wakapiga filimbi wakaja askari zaidi ya 300,” alisema Jacob.

Diwani huyo wa Ubungo alisema, “walipokuja wakafunga njia na walikuwa askari wa kiume, wakawashusha Mdee na Bulaya na kuanza kuwapiga, sasa mimi, Henry (Kileo) na Asenga tukashuka kwenda kuwasaidia.”

“Lakini na sisi tukajumuishwa kuwa tunawazuia wasifanye kazi yao, yaani sisi kuwazuia wasiwapige Mdee na Bulaya ni kuwazuia wasifanye kazi yao. Tulipigwa sana, mwenye kirungu na nini, wanapiga popote. Hata ule mkono wa Mdee kuvunjika siyo kwamba ulipigwa, wale askari walikuwa wanaubembea huku na huko.”

Alisema baadaye waliwekwa kwenye chumba kwa muda wa saa moja hadi walipokuja polisi na kuwapeleka Stakishari na baadaye usiku wakaachiwa kwa dhamana.

Jacob alisema ameumia kidole cha mkono wa kulia na mwilini ana maumivu kutokana na kipigo hicho.

Kauli ya Aga Khan

Akizungumza na Mwananchi jana asubuhi kabla ya Bulaya kuhamishiwa Aga Khan, mkuu wa idara ya masoko na mawasiliano wa hospitali hiyo, Olayce Steven alisema,” waliopo hospitali ni Halima Mdee na Jesca Kishoa. Wapo chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi na hali zao zinaendelea vizuri.”

Imeandikwa na Fortune Francis, Ibrahim Yamola na Bakari Kiango