Hasara, faida kwa wanaokiri makosa uhujumu uchumi

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya washtakiwa wa kesi za uhujumu uchumi wakitekeleza sheria ya makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) na kukwepa kifungo, wanasheria nchini wameeleza hasara na faida zinazotokana na uamuzi huo.

Miongoni mwa hasara waliyoitaja ni mshtakiwa kutokuwa na uwezo wa kukata rufaa na kubaki na dosari na kushindwa kuwania uongozi baadaye.

Plea bargaining ni utaratibu wa majadiliano baina ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na washtakiwa wa makosa mbalimbali ya jinai na uhujumu uchumi.

Majadiliano hayo yanalenga kuwezesha washtakiwa kukiri makosa wanayoshtakiwa nayo, waweze kupunguziwa adhabu au kupunguziwa mashtaka au kusamehewa kabisa.

Hadi Oktoba Mosi mwaka huu, DPP Biswalo Mganga alisema watuhumiwa 467 wa kesi za uhujumu uchumi waliandika barua za kuomba kukiri makosa na kurudisha fedha ambazo kwa jumla zimefikia Sh107.84 bilioni.

Wanasheria mbalimbali nchini wameelezea faida na hasara za utaratibu huo.

Wakili Benedict Ishabakaki wa kampuni ya Victory Attorneys and Consultants amesema moja ya madhara kwa mshtakiwa kufanya majadiliano hayo ya kukiri makosa yake ni kwamba huondoa nafasi ya kukata rufaa kwa mshtakiwa.

“Katika sheria hii kuna hofu kubwa watu kuingizwa katika mfumo huu kwa kufanya makubaliano ya kukiri hata kama hawajafanya makosa na hivyo kuingizwa katika rekodi ya jinai kwa wasio na hatia,” alisema.

“Kwa mtu ambaye amekaa gerezani kwa muda mrefu, ataenda kufanya makubaliano na mwendesha mashtaka hata kama hajafanya kosa ili tu atoke awe huru,” anasema Ishabakaki.

John Seka, wakili wa kujitegemea aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alisema miongoni mwa haki atakazokosa mtu anayekiri kosa la uhujumu uchumi ni pamoja na kubakia na dosari ya mtu aliyeshtakiwa ambayo inaweza kumfanya akose haki mbalimbali ikiwamo ya kugombea uongozi.

Alisema anaweza kukosa haki nyingine zinazokuwa zimeweka masharti ya kumkataa mtu aliyewahi kuwa na rekodi ya kukutwa na hatia, “ziko document nyingi tu, lakini pia huenda mali zake zikataifishwa kwa hiyo inategemea na makubaliano kati yake na DPP wakati wa majadiliano.”

Wakili mwingine wa kujitegemea, Daimu Halfani alisema mtu anayekiri kosa la utakatishaji fedha ndiyo hatari zaidi kwani anaweza kukosa haki nyingi zaidi ndani ya nchi na kimataifa ikiwamo kukosa haki ya kufanya biashara au kuwekeza.

“Inategemea na anayoingia lakini atasumbuliwa sana, hata akaunti zake zinaweza kushikiliwa na nchi aliyokuwa anafanya biashara au amewekeza. Pia atakosa haki ya kugombea nafasi za uongozi kwenye fursa za kimataifa.”

“Lakini ifahamike kwamba mazingira ya kosa la uhujumu uchumi ndiyo yanayotoa mwelekeo wa kukosa haki gani katika jamii kwa sababu makosa ya uhujumu ni mengi sana lakini yaliyo na viashiria vya uvunjifu wa maadili vitaathiri mtu kugombea uongozi.” alisema wakili Halfani.

Faida kukiri makosa

Kuhusu faida za sheria hiyo, Ishabakaki alisema ni kupunguza muda wa mahakama kusikiliza kesi, gharama zinazotumika katika uendeshaji wa kesi na suala zima la upelelezi.

Alisema kuwepo kwa sheria hiyo kunasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani, “mfano mshtakiwa anapokiri mashtaka yake anakuwa amesaidia upande wa mashtaka kutoleta mashahidi mahakamani, unakuta mashahidi wengine wanatoka nje ya mkoa hivyo wanatakiwa kulipwa fedha na Serikali kwa ajili ya kuja kutoa ushahidi.”