Hoja mbili zazua mjadala mkali bungeni Dodoma

Wabunge wa Chadema wakitoka ndani ya Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma jana. Kutoka kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Frank Mwakajoka, Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga, Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule na Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa. Picha na Anthony Siame

Dodoma. Masuala mawili kuhusu ukubwa wa majimbo ya uchaguzi na mamlaka ya halmashauri jana yalizua mjadala wakati Bunge likijadili bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) kwa mwaka 2020/2021.

Suala la mgawanyo wa majimbo liliwagawa wabunge wa CCM bungeni baada ya kutofautiana.

Bunge pia liligawanyika kwa itikadi za vyama katika suala la mamlaka za halmashauri, wakati wapinzani walipodai zimepokwa vyanzo vya mapato na serikali kuu.

Mjadala wa mgawanyo wa majimbo uliibuliwa na mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy aliyedai kuna majimbo yamegawanywa kisiasa, akisema yapo yenye kata sita na mengine kati ya 30 hadi 40.

Alisema licha ya tofauti hiyo, Tamisemi imekuwa ikigawa fedha sawasawa bila kujali ukubwa halisi wa jimbo.

“Kuna jimbo lina kata nane, haiwezekani kugawa sawa fedha za kumalizia maboma. Ni lazima tufuate idadi ya kata, hatuwezi kugawa kwa majimbo. Leo wanataka kupewa tena fedha kisiasa. Kule kwangu kata za Kabwe na Korongo ni sawa na majimbo mengine,” alisema.

Keissy alitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuangalia upya mgawanyo wa majimbo.

Naye Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema ni vyema Tamisemi ikaangalia namna wanavyoweza kugawa fedha hizo kulingana na ukubwa wa majimbo.

“Kuna jimbo lina kata 36 unawapa Sh140 milioni, lakini kuna jimbo lina kata 10 linapewa kiasi hicho hicho cha fedha na kila kata kuna maboma ambayo hajamalizika. Haitakuwa sawasawa,” alisema.

Hata hivyo, mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia alitofautiana na wabunge wenzake akitaka kupunguzwa kwa majimbo.

Alitolea mfano wa Halmashauri ya Geita imekuwa inasuasua katika suala la mapato kwa sababu ya kuongezwa maeneo ya utawala bila kufanya tathmini ya kutosha.

“Nilidhani ipo haja ya kupunguza majimbo. Kama tunafanya tathmini ya kutosha na tuna malengo mazuri na Taifa, tuna halmashauri 185 ni vyema kila halmashauri ikawa na mbunge mmoja badala ya halmashauri moja kuwa na wabunge wanne hadi watano, unatengeneza eneo ili fulani awe kiongozi,” alidai Nkamia.

Pia wabunge wa CCM na Chadema jana walivutana kuhusu utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka, wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Tamisemi.

Wabunge waliovutana wakati wakichangia ni Abdalah Chikota (Nanyamba-CCM) na Jaffar Michael wa Chadema.

Chikota alisema kwamba dhana ya ugatuaji ni pana sana na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inaitekeleza kwa dhati.

“Lengo kubwa ni kupeleka huduma karibu na wananchi. Hivi vituo 350 vilivyojengwa kazi yake ni kutoa huduma kwa wananchi,” alisema.

Aliwataka wabunge kutokariri utekelezwaji wa dhana hiyo kuwa ni kwa kutumia sera ya mwaka 1998 na kwamba haiwezi kutekelezwa kwa namna hiyo kwa sasa kwa sababu mambo yamebadilika.

Hata hivyo, Michael alisema anakubaliana na Chikota kuwa dhana ya ugatuaji madaraka ni pana, lakini anachotaka utekelezaji uwe kwa namna ilivyokuwa Serikali ya Awamu ya Tatu (ya Rais Benjamin Mkapa).

Alisema utekelezaji anaozungumza ni halmashauri ziweze kujitegemea kwa vyanzo vyake.

“Kila mtu anapokuja hapa bungeni anaangalia Serikali kuu imejenga zahanati, anaangalia kituo cha afya. Lakini kama ingetekelezwa kwa namna ilivyokuwa inatekelezwa wakati wa awamu ya tatu, ingeipunguzia Serikali mzigo. Utekelezaji huu una faida kubwa sana,” alisema.

Alisema kwa kutekeleza kwa jinsi hiyo kungewezesha halmashauri kuwa na vyanzo vya mapato kwa ajili ya kufanya miradi ya maendeleo katika maeneo yao.