IGP Sirro: Polisi ukijihusisha na siasa tutakushangaa

Muktasari:

Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Tanzania (IGP), Simon Sirro amesema kulingana na amri za jeshi hilo, askari atakayejihusisha na siasa lazima wenzake watamshangaa

Dar es Salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Tanzania (IGP), Simon Sirro amesema kulingana na amri za jeshi hilo, askari atakayejihusisha na siasa lazima wenzake watamshangaa.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Septemba 24, 2019 katika ufunguzi wa kikao cha siku tatu  cha maofisa waandamizi wa polisi kinachofanyika jijini Dar es Salaam ambako ameeleza masuala mbalimbali yanayolikabili jeshi hilo, likiwemo la kujihusisha na siasa.

“Changamoto nyingine ni baadhi yetu kujihusisha na siasa, katiba iko wazi na police general order (kanuni za polisi)  iko very clear (wazi kabisa) wala sio sifa, sisi Polisi wenzako tunakushangaa hata umma utakushangaa.”

“Watu wanataka kusikia unasema nini, wewe sio mwanasiasa unajiaibisha mwenyewe, tujikite kwenye majukumu yetu hayo unayofanya umeyatoa wapi,” amehoji Sirro.

Ameongeza, “Halafu unafanya hivyo kwa sababu uko kwenye nafasi hiyo tukikutoa hapo utaweza kufanyia nyumbani kwako? Si Pahala pa kufurahisha watu, wengine wanafanya vitu  kutafuta umaarufu wa kisiasa tu, unamfurahisha nani?”