IMF: Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia sita

Waziri wa Fedha Tanzania, Dk Philip Mpango

Dar es Salaam. Uchumi wa Tanzania unatarajiwa kufikia ukuaji wa asilimia sita mwaka 2020 kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambalo pia limepongeza sera bora za uchumi na fedha.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, amekaririwa mara kadhaa akisema uchumi unakuwa kwa asilimia saba.

Dk Mpango hakupatikana jana kuizungumzia ripoti hiyo mpya, Desemba 31 mwaka jana alisema uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 7 katika mwaka 2018 na kufanya iwe nchi ya kwanza kwa ukuaji wa uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na nchi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki.

“Kasi ya ukuaji wa kazi za kiuchumi inaonekana kuongezeka miezi ya karibuni ikichagizwa na ongezeko la uwekezaji wa Serikali, ukifuatiwa na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi na kukua kwa sekta binafsi,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo inayopatikana kwenye tovuti ya IMF.

Timu ya IMF ikiongozwa na Enrique Gelbard, imemaliza ripoti ya mwaka 2020 kuhusu Tanzania wiki hii, imesema ili kuendeleza hali hiyo, kunatakiwa kuwepo uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza ajira huku pia kukiwa na umuhimu wa kufanyika mabadiliko ya kiuchumi.

Timu hiyo iliyokuwepo Tanzania tangu Februari 20 mwaka huu ilikuwa na majadiliano na mamlaka za Serikali na imeishauri Serikali kuboresha usimamizi katika masuala ya kodi.

Gelbard aliishauri serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

Ripoti hiyo imesisitiza umuhimu wa kufuata kanuni za ukusanyaji wa mapato na udhibiti wake kupitia ukaguzi.

“Hii itahakikisha usahihi na ulipaji kodi kwa wakati na kuimarisha uingizaji wa mapato,” alisema katika ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuna fursa muhimu na ya haraka ya mapato kutokana na ongezeko la walipa kodi pamoja na kuimarishwa utawala katika ukusanyaji wa kodi, ukifuatiwa na itifaki na kanuni zilizoanzishwa.

Ripoti hiyo inapendekeza utekelezaji wa hatua zilizopangwa ili kuondoa malimbikizo ya matumizi, kwa kulipa malipo mbalimbali kwa wakati na kushughulikia mengine yanayoendelea kujilimbikiza.

Pia IMF imependekeza kuendelea kufanyiwa kazi kwa mikakati ya kuboresha biashara na njia za kuingiza mapato, kwa kuhakikisha mikopo ya benki inalipwa kwa wakati na kulinda ukuaji uchumi.

Kuhusu matumizi katika sekta za afya na elimu, ripoti imesema fedha zinapaswa kuongezwa katika miaka ijayo ili kusaidia upatikanaji wa huduma.

Matumizi hayo kwa kujibu wa ripoti hiyo yanapaswa kuandaliwa vema na kupewa kipaumbele ili kupata matokeo bora ya huduma za jamii.

Gelbard alisema Serikali inapaswa kuhakikisha mfumo wa fedha unalindwa na mamlaka zinaandaa mikakati kuhakikisha mikopo isiyolipika inaondolewa na kuzisimamia benki kiutendaji.

Alikuwa akimaanisha kuwa gharama za mikopo zipunguzwe na upatikanaji wa mikopo urahisishwe na masharti ya dhamana yalegezwe. “Ni muhimu kuboresha mifumo ya taarifa za mikopo na kuimarisha mifumo ya kisheria ili kupambana na mikopo isiyolipwa,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inaeleza umuhimu wa kutekeleza mabadiliko ya uboreshaji wa mazingira bora ya biashara na kwa hilo imesisitiza utekelezaji wa sera mpya ya serikali ya kuboresha sekta hiyo kama njia ya mabadiliko.

“Ukuaji wa uchumi unategemeana na kuboreshwa kwa vivutio vya kuwekeza Tanzania. Katika kipindi kijacho, sera madhubuti ni muhimu zikatumika kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi, upatikanaji wa ajira, kukuza uchumi na kukabiliana na majanga,” imesema ripoti hiyo.