Ifahamu shule iliyoingia 10 bora mara nne katika miaka mitano matokeo darasa la saba

Muktasari:

  • Baada ya Baraza la Mitihani nchini Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019, Mwananchi limebaini Shule ya Msingi Rocken Hill imeingia kwenye orodha ya shule 10 bora kitaifa mara nne katika kipindi cha miaka mitano.

Dar es Salaam. Baada ya Baraza la Mitihani nchini Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019, Mwananchi limebaini Shule ya Msingi Rocken Hill imeingia kwenye orodha ya shule 10 bora kitaifa mara nne katika kipindi cha miaka mitano.

Shule hiyo iliyopo mkoani Shinyanga imeingia kwenye orodha hiyo mwaka 2015, 2016, 2018 na 2019 ikifuatiwa na shule nyingine kutoka kanda ya ziwa ambazo zimeingia kwenye orodha hiyo mara tatu katika kipindi cha miaka mitano.

Shule zinazoifuatia Rocken Hill ni shule ya Twibhoki (Mara) ambayo iliingia mwaka 2015, 2018 na 2019; Mugini ya Mwanza (mwaka 2015, 2016 na 2019) na Kwema Modern ya Shinyanga (mwaka 2016, 2018 na 2019).

Shule hiyo ambayo mwaka huu imeshika nafasi ya 10 imejiwekea rekodi ya kuwa kwenye orodha ya 10 bora kitaifa huku baadhi ya shule nyingine zikiingia na kutoweka kabisa katika orodha hiyo.

Katika matokeo ya mwaka huu, shule 10 zilizoongoza kitaifa ni Graiyaki (Mara), Twibhoki (Mara), Kemebos (Kagera), Little Treasures (Shinyanga), Musabe (Mwanza), Tulele (Mwanza), Kwema Morden (Shinyanga), Peaceland (Mwanza), Mugini (Mwanza) na Rocken Hill (Shinyanga).

Mwaka 2018  zilizoongoza zilikuwa ni Raskazone (Tanga), Nyamuge (Mwanza), Twibhoki (Mara), Kwema Modern na Rocken Hill (Shinyanga), St Anne Marie (Dar es Salaam), Jkibira (Kagera), St Akleus Kiwanuka (Kagera), St Severine (Kagera), Rweikiza (Kagera).

Kumi bora ya mwaka 2017 zilikuwa ni St. Peters (Kagera), St Severine (Kagera), Alliance (Mwanza), Sir. John (Tanga), Palikas (Shinyanga), Mwanga (Kagera), Hazina (Dar es salaam), St. Anne Marie (Dar es salaam), Rweikiza (Kagera) na Martin Luther (Dodoma).

Mwaka 2016, shule zilizoingia 10 bora ni Kwema Modern (Shinyanga), Rocken Hill (Shinyanga), Mugini (Mwanza), Fountain of Joy (Dar), Atlas (Dar) na Gift Skillfull (Dar), Mudio Islamic (Kilimanjaro), St. Achileus (Kagera) na Carmel (Morogoro).

Mwaka 2015 ulikuwa na shule kama vile Waja Springs (Geita), Enyamai, Twibhoki (Mara), Mugini, Rocken Hill, Karume (Kagera), Alliance (Mwanza), Little Flower (Mara), Palikas (Shinyanga) na St Caroli (Mwanza).