Ikulu: EU yakubali kuruhusu mabilioni iliyoyazuia

Rais John  Magufuli akiagana na Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) hapa nchini Balozi
Manfredo Fanti baada ya kukutana jana Ikulu jijini Dar es salaam. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya (EU) umekubali kuruhusu kutoa Sh132 bilioni kwa ajili ya kuchangia bajeti ya maendeleo ulizokuwa umezizuia.

Uamuzi huo ulitangazwa jana baada ya Rais John Magufuli kufanya mazungumzo na balozi wa EU nchini, Manfred Fanti Ikuku jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inasema mazungumzo ya wawili hao yalikuwa na manufaa makubwa na yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na umoja huo.

Msigwa alisema katika siku za karibuni wamekamilisha mazungumzo yaliyoruhusu kuendelea kwa mpango wa EU kuchangia bajeti ya maendeleo ya Tanzania na sasa wanaandaa mpango mwingine wa miaka saba utakaoanza mwaka huu.

Taarifa hiyo inamnukuu balozi Fanti akisema kwa jinsi anavyoyaona maendeleo ya Tanzania, ana matumaini makubwa EU itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na nchi hii ili kufanya vizuri zaidi.

Rais Magufuli alimshukuru balozi huyo kwa juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na EU katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Mwezi Desemba 2018, EU Ilisimamisha kutoa msaada wa Euro 80 milioni (Sh 203 bilioni) baada ya kutokea mgogoro wa kidiplomasia.

Ingawa taarifa hiyo haikueleza kwa kina kwa sababu za mabilioni hayo kuzuiwa, mwaka jana kuliibuka mvutano wa chini kwa chini kati ya umoja huo na Serikali hadi kusababisha aliyekuwa balozi wa EU nchini, Roeland van de Geer kuamriwa kuondoka nchini.

Geer aliondoka Novemba 3 mwaka jana kwenda Ubelgiji kwa kile kilichoelezwa ni kwenda kufanya mashauriano na mabosi wake, hali iliyoilazimisha EU kumteua Fanti kuja kurithi nafasi ya Geer.

Hali hiyo ilifuatiwa baadhi ya nchi kupunguza misaada kwa Tanzania, na Denmark ilikata msaada wa dola 9.8 milioni (Sh 24 bilioni) na hivi karibuni Sweden imetangaza kukata robo ya misaada.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na katibu mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), Dk Stergomena Tax na balozi wa China nchini, Wang Ke

Dk Tax alikwenda kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala ya jumuiya hiyo kama uendelezaji wa viwanda na kanda huru ya biashara na wamekubaliana kuendelea kuhamasisha nchi wanachama kuendeleza viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

Alisema baadhi ya maeneo yaliyopo katika mkakati wa kukuza uchumi wa Sadc ni kuendeleza miundombinu, hasa ya usafiri na nishati ambayo bado ni changamoto kwa nchi za Sadc.

Pia aliipongeza Tanzania kwa hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa, kama za ujenzi wa barabara, reli na kuongeza uzalishaji wa umeme.

Katika mazungumzo yake na balozi huyo, Magufuli alimkabidhi barua aliyomwandikia rais wa China, Xi Jinping akimpa pole kwa janga la homa ya virusi vya corona lililolikumba jiji la Wuhan na kusababisha vifo vya takriban watu 500 hadi jana.

Pamoja na kukabidhi barua hiyo, Rais Magufuli alisema Tanzania imeguswa na mlipuko wa virusi hivyo vipya aina ya corona na ipo tayari kutoa ushirikiano wowote ambao serikali ya China itahitaji katika jitihada za kukabiliana na homa hiyo.

“China ni ndugu zetu, na marafiki zetu,” alisema Magufuli.

“Tunatoa pole kwa Rais Xi Jinping na Wachina wote waliopatwa na madhara ya homa hii, daima Tanzania tupo pamoja na China na katika hili tupo pamoja pia,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, balozi Wang Ke alimshukuru Rais Magufuli kwa kuguswa na janga hilo na kuungana na China katika kipindi hiki kigumu.