Isabel dos Santos, mwanamke tajiri anayeandamwa kwa siasa, ufisadi

Sunday January 19 2020

 

By Reginald Miruko na mashirika

Inategemea unaiangalia habari hii ukitokea upande upi. Ukiwa upande wa serikali ya Angola, Isabel dos Santos utamwona ni mtuhumiwa wa ufisadi anayeogelea katika utajiri aliojikusanyia kutokana na fedha za umma.

Lakini kwa upande mwingine, huyu ni mwanamke mfanyabiashara, mpambanaji mwenye mafanikio anayeandamwa na Serikali kuwa sababu za kisiasa.

Tamko lake la karibuni kuwa anaweza kuwania uraia wa Angola, linamweka katika nafasi nyingine ya kuangaliwa kwa jicho kali zaidi na serikali ya nchi yake, hasa katika kipindi ambacho mali zake na akaunti zinashikiliwa na kwa amri ya mahakama kutokana na tuhuma za ufisadi na utakatishaji fedha.

Isabel mwenye umri wa miaka 46 ni mmojawapo wa wanawake matajiri zaidi duniani, huku jarida la Forbes likikadiria mali yake kuwa yenye thamani ya Dola za Marekani 2.2 bilioni, hatua inayomfanya kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika.

Babake Jose Eduardo Dos Santos wakati huo akiwa Rais wa Angola alimteua Isabel kuongoza kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Angola, Sonangol mwaka 2016.

Mwanamke huyo alifutwa kazi mwaka 2017 na Rais Joao Lourenco, mrithi wa kiti hicho aliyechaguliwa na babake. Rais Eduardo dos Santos aliiongoza Angola kwa miaka 38.

Advertisement

Mwaka huo wa 2017 Isabel alijiongezea utajiri baada ya kuchukua udhibiti wa benki kubwa zaidi nchini Angola, BFA, baada ya kampuni yake kununua hisa zaidi na kudhibiti zaidi ya asilimia 50 ya hisa katika benki hiyo.

Tuhuma na mashtaka

Kutokana na madai kwamba utajiri wake ulitokana mali ya umma, amefunguliwa mashtaka kadhaa huku yeye akiwa nje ya nchi.

Waendesha mashtaka wameomba hati ya mahakama kukamata mali na fedha zake wakiwa katika harakati ya kukomboa Dola 1 bilioni ambazo Isabel na washirika wake wanadaiwa na serikali.

Mahakama moja mjini Luanda mwezi uliopita iliagiza kushikiliwa kwa akaunti yake ya benki na biashara yake katika taifa hilo anazomiliki na mume wake, Sindika Dokolo, ambaye ni raia wa DRC.

Taarifa zaidi zinasema kuwa hisa za wawili katika kampuni kadhaa za Angola, pamoja na kampuni ya simu ya Unitel na ile ya simenti ya Cimangola, pia zimeshikiliwa na mahakama.

Hatua hiyo ni kufuatia misururu ya uchunguzi kuhusu madai ya ufisadi uliofanywa na familia ya dos Santos, ambayo waendesha mashtaka wanasema imeliibia taifa hilo zaidi ya dola bilioni mbili.

Tuhuma zake si tu ndani ya Angola, hata Benki Kuu ya Ureno inaichunguza benki ya Eurobic, ambayo Isabel anamiliki hisa nyingi kwa tuhuma za utakatishaji fedha.

Benki hiyo ililieleza Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) kuwa inatekeleza matakwa ya kisheria ya kuzuia miamala ya fedha isiyo halali, na hivyo iliona uchunguzi huo ni suala la kawaida.

Ilisema uchunguzi huo ulianza Novemba kabla ya Serikali ya Angola kushikilia mali za Isabel mwezi Desemba.

Maisha hatarini

Katika mahojiano na vyombo vya habari, Isabel ameripotiwa akisema maisha yake yapo hatarini iwapo atarudi nchini Angola katika hali ilivyo.

‘’Haya ni madai ya uongo na huu ni mpango wa kisiasa wa serikali iliyopo,” anasema.

Nduguye wa kambo Jose Filomeno Dos santos pia anakabiliwa na kesi nchini Angola kutokana na mashtaka ya ufisadi.

Upande wa mashtaka unadai kwamba yeye na wenzake walisaidia kupeleka nje ya nchi $500m wakati alipokuwa mkuu wa hazina ya Angola.

Adai tuhuma za kisiasa

Isabel anamshutumu mara kwa mara Rais Lourenco ambaye alimrithi babake miaka miwili iliopita, kwamba licha ya kutoka katika chama kimoja cha MPLA ameonekana akiilenga familia ya Dos Santos katika anachoita mikakati ya kupambana na ufisadi.

“Mimi ni mfanyabiashara. Watu wengi wananipenda na kunielewa ninachofanya na kuamini ninachofanya,” alisema akisifu biashara zake na kukana madai kwamba utajiri wake ulitokana na mali ya babake.

Isabel, sawa na wengi wa wanafamilia ya dos Santos, aliondoka Angola akidai anakabiliwa na vitisho vya kuuawa baada ya baba yake kuondoka madarakani.

‘’Haya ni madai ya uongo na huu ni mpango wa kisiasa wa serikali iliyopo,” anasema.

Mwaka 2016 aliteuliwa kuwa mkuu wa kampuni ya matuta ya taifa Sonangol lakini alitolewa kwenye wadhifa huo mwaka uliofuata wa 2017, katika hatua ya kwanza iliyofanywa na Rais Lourenco ya kuwaondoa jamaa za dos Santos kutoka kwenye nyadhifa mbalimbali.

‘’Iwapo kutakuwa na mgombea tofauti kabla ya uchaguzi mkuu wa 2021 ambaye ataungwa mkono na rais wa zamani Jose dos Santos ama washirika wanaohusishwa naye, hiyo itatoa changamoto kuu kwa Lourenco kwa kuwa rekodi yake ni mbaya sana,” aliongezea, akitaja ukosefu wa ajira, uchumi uliozorota na msururu wa migomo.”.

Kuhusu madai ya ufisadi yanayomlenga Isabel, mchambuzi wa siasa za Angola, Daria Jonker anasema, ‘’ukweli ni kwamba kuna ushahidi mwingi dhidi yake. Ni mtu muhimu katika familia ya Dos Santos na tisho kubwa kwa Lourenco.”

‘’Lourenco anatuma ujumbe kwamba kuna kiongozi mpya akiwa na sheria mpya’’, anasema Jonker akinukuliwa na BBC.

Hata hivyo Isabel anasema anatumika kama ‘kafara’ na Rais Lourenco na anaishutumu idara ya mahakama ya Angola, akimlaumu mwanasheria mkuu kwa kudanganya na kukataa mawakili wake kuona ushahidi uliopo.

‘’Najuta kwamba Angola imetumia njia hii. Nadhani sote tutapoteza mengi, kiongozi mzuri ni kiongozi mzuri,” alisema akitaka kufanyika kwa mazungumzo ili kupata suluhu ya kisiasa kuhusu hali inayomkabili.

Kuwania urais

Katika taarifa ambazo huenda zilisubiriwa na wengi na zinaweza kuwasumbua wengi pia, Isabel wiki hii amesema anafikiri kuwania urais mwaka 2022.

‘’Kuongoza ni kuhudumu, hivyo basi nitafanya ninachoweza maishani mwangu,’’ alisema.

Isabel aliieleza televisheni ya Ureno kwamba kuna uwezekano atawania urais 2022, lakini alipohojiwa awali na BBC alipinga mara nne kuhusu uwezekano huo.

Tangazo hilo liliadhinisha mabadiliko kwa mwanamke huyo ambaye amekuwa akijitaja kama mfanyabiashara asiye na hamu ya kufanya siasa.

Advertisement