Jinsi mapenzi ya Mugabe na Grace ‘yalivyotikisa’

Robert Mugabe akimbusu mkewe Grace Mugabe kabla ya kuhutubia mkutano. Ilikuwa ni mazoea kwa kion-gozi huyo kumbusu mkewe kabla ya mkutano kuonyesha ishara ya mapenzi. Picha ya Maktaba

Harare. Katika umri wake mkubwa wengi walidhania kwamba aliyekuwa rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe angekuwa akikabiliwa na upungufu wa fahamu, lakini kama mvinyo, alikuwa akionekana kuimarika kila uchao.

Uhusiano wa kimapenzi kati yake na Grace ulianza wakati alipokuwa akifanya kazi kama mpiga chapa katika ikulu ya rais ya Zimbabwe .

Wawili hao walianza kuonana kisiri wakati Mugabe alipokuwa na mkewe wa kwanza Sally ambaye alikuwa akiugua, tofauti ya umri wao ikiwa miaka 40.

‘’Alikuja kwangu na kuanza kuniulizia kuhusu familia yangu’’, alisema Grace katika mahojiano kuhusu walivyojuana na kiongozi huyo miaka ya 80.

‘’Nilimuona kama baba yangu. Sikudhania kwamba atanitazama na kuniambia nampenda huyu msichana, sikutarajia hata kidogo’’, aliongezea Grace alipozungumza na BBC.

Ijapokuwa bado alikuwa na mkewe wa kwanza, Mugabe hakuweza kuzuia mapenzi yake kwa Grace, alisema mrembo huyo akihojiwa na vyombo vya habari nchini Zimbabwe.

‘’Mama yangu alikuwa akilia akisema kwamba angependelea kuwaona watoto wangu kabla ya kufariki dunia,” alinukuliwa Mugabe alipozungumza na chombo cha habari cha Newsdze cha Zimbabwe.

‘’Mke wangu Sally alikuwa mgonjwa na alikuwa kitandani na wakati huo nikakutana na Grace katika ikulu ambapo alikuwa akifanya kazi kama katibu wangu’’, alinukuliwa Mugabe.

‘’Ni kweli tulianza uhusiano huo wakati Sally alipokuwa hai’’, ilinibidi.

‘’Mimi na Grace hatukuchumbiana, nilijulishwa kumuhusu na nikajiambia ni msichana mrembo’’ .

‘’Hivyo, basi alianza kufanya kazi kama katibu na walikuwa wengi katika Ikulu, niliwatazama na hapo mapenzi yakaanza tulipoonana na Grace’’.

Aliongezea, “na baadaye, siku moja nilimwambia, nakupenda na nilimuona ameshikwa na ganzi. Nilimshika mkono wake na kumpiga busu.

‘’Hakukataa na wala kupinga na baadaye nikaiambia nafsi yangu kwamba kwa kuwa amekubali busu langu basi nimemaliza mchezo’’. alinukuliwa na vyombo vya habari vya Zimbabwe akisema.

Mugabe alisema kwamba wawili hao walikuwa wakikutana kisiri katika nyumba ya dada yake Sabina (marehemu) huku wapwa wake wakitumwa nje ili kuficha uhusiano huo.

Mugabe anasema kwamba mkewe wa kwanza Sally aliupatia baraka uhusiano wake na Grace kabla ya kifo chake mwaka 1992.

Hata hivyo, anasema kwamba hakumuoa Grace hadi miaka minne baadaye.

Wapenzi hao wawili walipata watoto watatu: Bona, Robert na Chatunga.

Licha ya wengi kudai kwamba alikuwa akikabiliwa na saratani ya tezi dume, Mugabe aliishi maisha yenye afya .

Grace alinukuliwa akisema kwamba (Mugabe) alikuwa akiamka saa kumi na moja alfajiri ili kufanya mazoezi ya viungo ikiwemo yoga na kwamba mumewe hakunywa pombe ama hata kahawa na mara nyingi alipendelea kula mboga

Kabla ya hotuba zake Mugabe alikuwa akimpiga busu la chini ya kidevu chake mkewe Grace ili kuonyesha upendo wake kwake.

Na kufuatia mapenzi hayo Grace naye hakuachwa nyuma kwani aligonga vichwa vya habari mara kwa mara kwa kumuunga mkono mumewe kwa kila jambo.

Alizua gumzo nchini Zimbabwe wakati mmoja aliposema kwamba mumewe anaweza kupigiwa kura hata akiwa maiti.

Alisema kwamba jina lake litawekwa kwenye karatasi za kupiga kura hata akiaga dunia mbali na kutumia uongozi wa mumewe kuwakabili wapinzani wake mara kwa mara.

Hata hivyo, alizua songombingo wakati wa mwisho wa uongozi wa Robert Mugabe alipomtaka mumewe kumtaja ‘mrithi’ wake ili kupunguza migawanyiko kuhusu mtu atakayemrithi..

‘’Rais hafai kuwa mwoga kumchagua mrithi wake na neno lake litakuwa la mwisho,’’ alisema Grace.

Na wakati alipohisi kwamba mambo yalikuwa yanaenda mrama katika kambi ya kisiasa ya mumewe Grace hakusita kuonya kwamba kulikuwa na uwezekano wa kufanyika kwa mapinduzi nchini humo, huku kukiwa na uvumi kwamba huenda Mugabe akamwachia mkewe uongozi wa taifa hilo.