Jinsi vyama vikubwa vya siasa Afrika vilivyoanguka

Tahadhari iliyotolewa na Rais John Magufuli kwa chama tawala (CCM) kuwa kiache kuongoza kwa mazoea kwani kinaweza kuanguka, ni muhimu kwa chama hicho.

Rais Magufuli alitoa tahadhari hiyo wiki iliyopita wakati wa akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM jijini Mwanza na kusema CCM inaweza kupoteza dola iwapo viongozi wake watajisahau.

Pamoja na changamoto mbalimbali, kubwa na ya muda mrefu ni ya wananchi kulalamikia hali ngumu ya maisha, hivyo ni jukumu la chama kilicho madarakani kuifanyika kazi vinginevyo itaweza kuwa ‘kaa la moto’ kwao katika chaguzi zijazo.

CCM, chama ambacho kimetokana na muungano wa mwaka 1977 wa vyama vya ukombozi vya Tanu kilichofanikisha kupatikana uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na ASP kilichoongoza mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kinatakiwa kuifanyia kazi tahadhari iliyotolewa na Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho kwa kufanyia kazi changamoto mbalimbali za wananchi.

Mara kadhaa katika mikutano ya hadhara, Rais Magufuli ameonekana kuwa mstari wa mbele kutatua kero mbalimbali zinazowasilishwa kwake na wananchi kwa njia ya mabango yenye ujumbe.

Hata hivyo kama kuna kipindi ambacho tishio la CCM kung’olewa madarakani kupitia sanduku la kura lilikuwa kubwa basi kipindi hicho bila shaka ni wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Ni wakati ambao mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru akiwa katika kampeni za uchaguzi mkuu alionya kuwa CCM imeishiwa pumzi ya kuongoza nchi kutokana na kudorora kwa uchumi.

“Nusu karne ya CCM ni muda mrefu kuongoza nchi, hii ni sawa na kupanda mlima unafika mahala pumzi zinakuishia, huwezi kuendelea mbele, CCM imeishiwa pumzi,” alisema Kingunge.

Wakati Rais Magufuli akitoa tahadhari hiyo, vyama kadhaa barani Afrika vilivyotawala kwa muda mrefu vimeondolewa madarakani kwa njia ya sanduku la kura ama kwa nguvu za wananchi.

Sudan

Chama cha National Congress (NCP) kilichoongoza Sudan tangu mwaka 1989 kiliondolewa madarakani mapema mwaka huu, baada ya wimbi kubwa la maandamano.

Baada ya kuondolewa, viongozi wapya wa Sudan walikivunja na kukifuta chama hicho katika madaftari ya vyama vya siasa vilivyosajiliwa Sudan ingawa chama hicho cha Rais aliyeng’olewa madarakani, Omar al-Bashir kililaani uamuzi wa viongozi wapya

wa Sudan kukipiga marufuku na chama hicho na kusema hawatishiki na amri yoyote au sheria kwa kuwa wanatambua wao wana nguvu na fikra zao zitadumu.

Al Bashir alichukua mamlaka mwaka 1989 kwa mapinduzi na kuliongoza taifa hilo kwa takriban miongo mitatu, hadi alipoondolewa kwa vuguvugu la maandamano ya upinzani Aprili mwaka huu.

Sudan kwa sasa inaongozwa na utawala unaojumuisha jeshi na baraza la kiraia pamoja na baraza la mawaziri la raia linaloongozwa na waziri mkuu, Abdallah Hamdok.

Juzi, Mahakama Sudan ilimkuta Al-Bashir (75) na hatia ya makosa ya utakatishaji fedha na rushwa na kumhukumu kifungo cha miaka miwili katika kizuizi chenye ulinzi mdogo. Al-Bashir alikuwa kizuizini tangu Aprili mwaka huu.

Hukumu hiyo ni ya kwanza katika msururu wa kesi zinazomkabili Al-Bashir, ambaye pia anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuhusiana na mashitaka ya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki yaliyotokana na mgogoro wa Darfur katika miaka ya 2000.

Algeria

Aliyekuwa Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika mapema mwaka huu alilazimishwa kustaafu baada ya kudumu madarakani kwa miaka 20. Baada ya kustaafu, Bunge la Algeria lilimteua Spika wa Bunge Kuu, Abdelkader Bensalah kuwa kaimu rais wakati wa kipindi cha mpito.

Bouteflika alijiuzulu baada ya maandamano ya wiki kadhaa nchini mwake. Pia alikuwa amefuta mpango wake wa kugombea muhula mwingine kutokana na kukuwa kwa upinzani.

Jeshi la Algeria ambalo lina nguvu, lilimtaka atangaze kuwa hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya uongozi. Bouteflika alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi tangu mwaka 2013, mara chache alikuwa akionekana hadharani. Chama tawala Algeria FLN kiliunga mkono kuondolewa madarakani kwa Rais Bouteflika.

Ghana

Mwaka 2016, mgombea Nana Akufo-Addo wa chama cha New Patriotic (NPP) alishinda uchaguzi nchini Ghana kwa asilimia 53.8.

Rais aliyekuwa madarakani, John Mahama wa chama cha New Democratic Congress (NDC)alikubali kushindwa katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Congo

Felix Tshisekedi, alishinda uchaguzi wa urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Tshisekedi alimshinda mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu na yule aliyekuwa akiungwa mkono na Serikali, Emmanuel Shadary.

Tshisekedi, alimsifu rais aliyeondoka Joseph Kabila aliyeongoza kwa miaka 18. Tshisekedi amekuwa mgombea wa kwanza wa upinzani kushinda uchaguzi wa urais tangu DRC ilipojipatia uhuru kutoka Ubelgiji mwaka 1960.

Malawi

Chama cha Malawi Congress (MCP) kilikuwa chama pekee kilichotawala Malawi chini ya Rais Hastings Kamuzu Banda. Kilikaa madarakani kwa miaka 30 kabla ya kutolewa kwa shinikizo la uchumi duni na rushwa.

Mwaka 1993 Serikali ya Banda ililazimshwa kukubali kura za wananchi walioamua kumaliza mfumo wa chama kimoja na kuanzisha ule wa vyama vingi.

Uchaguzi wa mwaka 1994 ulimaliza utawala wa MCP ukamfanya Bakili Muluzi wa United Democtaric Front (UDF) kuwa ndiye rais ambaye aliongoza hadi 2004.

Vyama vingine vya ukombozi vilivyoanguka ni Kanu cha Kenya, UNIP cha Zambia chini ya Rais Kenneth Kaunda na mwaka 1971 Milton Obote wa UPC aliyekuwa Rais wa Uganda alipinduliwa na Idi Amin na kukimbilia uhamishoni nchini Tanzania, na baadae alirudi madarakani mwaka 1980 - kabla ya kuondolewa tena miaka sita baadae na rais wa sasa Yoweri Museveni.

Kauli za wanasiasa

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema anawahakikishia CCM kuwa hawana uwezo na hoja za kupambana na nguvu ya upinzani ukiwa pamoja.

Alisema kwa hali ilivyo sasa hatamani mikutano ya hadhara, bali anatamani siasa za namba na kueleza kuwa wakati wa harakati wa kutafuta uhuru wa nchi viongozi waliopo hawakufanya mikutano ya hadhara.

“Mikutano ya hadhara ilipigwa marufuku na wakoloni. Sheria ya uchochezi tunayoiishi leo ni ya kikoloni, iliyopiga marufuku harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu, leo watawala wanazitumia sheria hizo hizo kupinga sisi kutafuta uhuru wa kweli na maendeleo ya kweli,” anasema na kuongeza:

“Mbinu zile zile za mababu zetu za mguu kwa mguu, nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda tunakwenda kuziimarisha,” alisema Mbowe wiki iliyopita katika mkutano wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha).

Alisema kuna mbinu 1,001 za kufanya siasa, hivyo wanafanya operesheni nchi nzima na kufika katika kanda zote 10 za chama hicho, mikoa yote 32, majimbo 264, kata 3,948, vijiji 12,260 na kuandikisha wanachama kwa mamilioni.

Katibu wa itikadi, mawasiliano na uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu anasema ana imani kulingana na nafasi ya Rais, anafahamu mambo mbalimbali ndani ya nchi, hivyo anatambua kuwa bado CCM haijajipanga vizuri kwa ajili ya kupata ushindi katika chaguzi.

Katibu mkuu wa CUF, Khalifa Khalifa anatoa wito kwa Rais Magufuli kutoishia kutoa tahadhari kwa CCM pekee, bali atumie nafasi yake kutoa maelekezo kwa mamlaka nyingine.

“Rais kwa mamlaka aliyonayo anatakiwa aende mbali zaidi kwa kuhakikisha anakuza na kulinda demokrasia nchini,” anasema.