‘Jitokezeni kwa wingi Oktoba 28 kupiga kura’

Muktasari:

Watanzania wamekumbushwa kuacha uvivu na uzembe wa kutoshiriki upigaji wa kura badala yake wajitokeze kwa wingi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28,2020.

Dodoma. Watanzania wamekumbushwa kuacha uvivu na uzembe wa kutoshiriki upigaji wa kura badala yake wajitokeze kwa wingi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28,2020.

Akihubiri leo Jumapili Oktoba 25, 2020 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa kuu Dodoma, Mchungaji Samwel Mshana amesema kumekuwa na uzembe kwa baadhi ya watu kutoona umuhimu wa kushiriki upigaji kura.

Mchungaji Mshana amesema upigaji wa kura ni haki ya kikatiba kwa kila Mtanzania ambaye amefikisha umri wa miaka 18.

Mchungaji Mshana amesema  kumekuwa na uzembe wa baadhi ya watu kutoona umuhimu wa kupiga kura kuhu wakisubiri kuchaguliwa viongozi na watu wengine.

“Tuache uzembe na kutoenda kupiga kura, kwani ukienda kupiga kura unapungukiwa na nini? Tujitokeze kwa wingi tukachague viongozi kwa maendeleo yetu,” amesema Mchungaji Mshana.

Amesema kila mtu kwa nafasi yake anatakiwa kumuomba Mungu amkumbushe kuwa Oktoba 28,2020 ni siku ya kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais.

Mmoja wa waumini wa kanisa hilo Doreen Julius amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi Watanzania wanatakiwa kijikita zaidi kuliombea Taifa ili uchaguzi umalizike salama.