Juhudi za wanasayansi kusaka dawa, chanjo ya covid 19

Wakati maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 yakiendelea kuongezeka duniani, wanasayansi wanaendelea kukuna vichwa kusaka chanjo na dawa ya ugonjwa huo.

Mpaka jana jumla ya watu 876,348 waliripotiwa kupata maambukizi ya virusi hivyo, huku watu 43,521 wakifariki dunia.

Chanjo ni njia pekee ya kuwalinda watu dhidi ya maambukizi, lakini kwa waliopata maambukizi wanahitaji tiba.

Sasa watu waliopata ugonjwa huo hupatiwa tiba kulingana na dalili walizonazo. Mfano kama mgonjwa ana dalili na homa, hupatiwa dawa za kutibu dalili hiyo.

Hata hivyo, Marekani juzi iliruhusu dawa ya chloroquine kutumika kama sehemu ya tiba ya covid 19 ikieleza hatua hiyo imefikiwa baada ya utafiti kuonyesha kuwa zina uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

Pamoja na hayo, Mamlaka ya chakula na dawa ya Marekani (FDA) imeonya kuwa matumizi ya kupindukia ya dawa hizo yanaweza kusababisha madhara. Pia watalaamu wa afya hawajaruhusu vidonge hivyo kutumika kutibu covid 19.

Kampuni ya dawa ya mjini Tubongem iitwayo Curevac ya Ujerumani hivi karibuni ilitoa matumaini kuwa chanjo ya virusi vya corona inaweza kupatikana baadaye mwaka huu ikiwa kila mpango utakwenda kama ulivyopangwa.

Mjumbe wa bodi ya kampuni hiyo, mkemia Friedrich von Bohlen alinukuliwa na mtandao wa DW akisema mbali na kampuni hiyo kuweka nguvu kutafuta chanjo, pia inafanya utafiti wa tiba dhidi ya ugonjwa huo.

Katikati ya mwezi uliopita, Marekani ilianza kufanya jaribio la chanjo ya kinga dhidi ya virusi hivyo na watu wanne walijitokeza kudungwa sindano ya virusi hivyo katika kituo cha utafiti Kaiser Permanente mjini Seattle, Washington, Marekani.

Wataalamu walisema chanjo hiyo haiwezi kusababisha Covid 19, lakini ina jeni ya virusi vinavyoweza kusababisha ugonjwa huo.

Nako China, mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa bioteknoojia, Zhang Xinmin alisema utafiti uliofanywa juu ya dawa iliyotengenezwa Japan kwa ajili ya kutibu mafua, umeonyesha dawa hiyo inaweza kuharakisha mgonjwa wa Covid 19 kupata nafuu.

Dawa hiyo inayoitwa Faviprapir, pia hujulikana kama Avigan au Favilavir ilitumika kwa kundi fulani la wagonjwa.

Kituo hicho kilieleza muda wa kupata nafuu ulipungua kutoka siku 11 hadi siku 4 kwa wagonjwa waliotumia tiba ya dawa hiyo, huku asilimia 91 ya wagonjwa walionyesha kuboreka katika afya ya mapafu.

Inaendelea uk 22

Inatoka uk 21

Katika hilo, Shirika la afya duniani (WHO) lilisema ugunduzi huo ni kitu muhimu katika kufikia tiba ya ugonjwa wa Covid 19.

Hata hivyo, lilisema inaweza kuchukua miezi 18 kabla ya chanjo dhidi ya virusi vya corona kutolewa kwa umma.

Kwanini muda mrefu? WHO imesema kuna mambo kadhaa yanatakiwa kuzingatiwa kabla ya majaribio ambayo wanasayansi wanatakiwa kutambua na kufanyia utafiti.

Mkurugenzi wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus alipongeza watafiti wote duniani ambao wamekuwa pamoja, ili kutathimini majaribio ya tiba.

“Majaribio madogomadogo ya njia mbalimbali yanaweza yasitupe ushahidi wa kutosha, tunahitaji tiba yoyote ambayo itatusaidia kuokoa maisha,” alisema.

Alisema shirika hilo na washirika wake wanaandaa utafiti katika nchi nyingi, ili kukusanya takwimu zinazohitajika kuonyesha matibabu yapi yanafaya kazi zaidi.

Mkurugenzi huyo alisema nchi kadhaa zimethibitisha kushiriki utafiti huo wa ‘mshikamano wa majaribio’ zikiwemo Argentina, Bahrain, Canada, Ufaransa, Iran, Norway, Afrika Kusini, Hispania, Uswisi na Thailand na anaamini nchi nyingine nyingi zitajiunga.

Ili kuanzisha utafiti huo, jopo la wataalamu wa shirika hilo lilichagua tiba nne ambazo wanazithamini zinaweza kukabiliana na virusi vya corona. Tiba hizo zina dawa mchanganyiko ambazo zimetumika kutibu Ebola, malaria na zile za kufubaza virusi vya Ukimwi.

Wataalamu hao walisema tiba hizo zitatumika bila mpangilio, madaktari watachunguza jinsi wagonjwa wanavyoendelea, ikiwemo siku watakazoondoka hospitalini au iwapo atashindwa kupona.

Tiba ya kwanza ni dawa ya Remdesivir ambayo licha ya kutengenezwa kutibu Ebola, inaonekana kuwa na uwezo dhidi ya virusi vya corona.

Stephen Morse, mkurugenzi wa mpango wa magonjwa ya kuambukiza katika Chuo Kikuu cha Columbia (EE) alilimbia BBC kuwa “kati ya dawa zilizojumuishwa katika mradi wa Solidarity, remdesivir inaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na virusi vya corona katika vipimo vya maabara.”

Dawa nyingine ni chloroquine/hydroxychloroquine ambazo kwa miaka mingi zilitumika kutibu malaria kabla ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo havijatengeneza usugu dhidi ya dawa hiyo.

Tiba nyingine ni dawa ya Ritonavir na lopinavir ambazo zimetumika kwa matibabu ya kufubaza virusi vya Ukimwi, ingawa inaelezwa kuwa mchanganyiko huo haujaonyesha matokeo mazuri dhidi ya kupambana na virusi vya corona.

Tiba ya mwisho inayofanyiwa utafiti ni mchanganyiko wa ritonavir na lopinavir pamoja na interferon-beta, molekyuli ambayo husaidia kudhibiti uchochezi na imeonekana kuwa bora kwa wanyama walioambukizwa ugonjwa wa Mers.

Pamoja na hatua hizo, kwa mujibu wa WHO, wanasayansi kutoka maeneo mbalimbali duniani wanafanya kazi ya kutengeneza chanjo takribani 20 za virusi hivyo.

Dk George Rutherford, Profesa wa takwimu za kibaiolojia katika Chuo Kikuu cha Carlifonia, Marekani alinukuliwa na BBC akisema utafiti kama huo unaweza kusajili wagonjwa kwa haraka.

“Mfano nikifanyia majaribio haya katika maabara yangu, ningekuwa na wagonjwa wawili au watatu kwa siku, lakini kutokana na ushirikiano wa vituo kadhaa unaweza kuwa na wagonjwa 100 kwa siku,” alisema.

Profesa Rutherford alisema iwapo hakuna matatizo ya kimpango, utafiti kama huo unaweza kutoa matokeo katika kipindi cha mwezi mmoja.

Wakati wanasayansi wakiendelea na harakati za kusaka chanjo na dawa, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani alisema haki ya kutafiti kinga ya virusi hiyo haiuzwi baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutaka nchi hiyo inunue haki peke kwa dawa inayoweza kuwa kinga iliyotengenezwa na kampuni ya Ujerumani.

“Watafiti wa Ujerumani wanachukua nafasi kubwa katika utengenezaji wa dawa na kinga na hatuwezi kuruhusu wengine kuomba haki peke za matokeo yake,” Heiko Maas aliiambia Funke.

Awali gazeti la Die Welt liliripoti awali kuwa Trump aliahidi dau la “mabilioni ya dola” ili Marekani ipatiwe haki hizo za kutafiti kinga na kampuni ya CureVac inayojihusisha na teknolojia ya virusi.