KESI YA KINA KITILYA: Serikali ilivyoweka msingi wa kesi katika kikao cha kwanza kuelekea cha pili

Kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili mkurugenzi wa kampuni ya ushauri wa uwekezaji, huduma za uwezeshaji na upatikanaji wa fedha, Enterprise Growth Market Advisors Limited (Egma), Harry Kitilya na wenzake, leo inaingia katika kikao cha pili cha usikilizwaji wa ushahidi upande wa mashtaka.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 04 ya mwaka 2019, inasikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama ‘Mahakama ya Ufisadi’ mbele ya Jaji Immaculata Banzi.

Imepangwa kuendelea kusikilizwa katika kikao cha pili kwa siku 19 mfululizo kuanzia leo mpaka Oktoba 4, 2019.

Wakati kiko cha pili kinaanza, tunakuletea muhtasari wa kile Serikali ilichokifanya katika kikao cha kwanza, ambacho ndicho kilijenga msingi wa kikao hiki cha pili, ili kupata picha halisi ya mendeleo ya usikilizwaji wa kesi hii.

Washtakiwa na mashtaka yanayowakabili

Mbali na Kitilya ambaye aliwahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), washtakiwa wengine ni Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Shose ambaye ni mshindi mashindano ya Urembo (Miss Tanzania) mwaka 1996 na Solomoni, walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbick, Shose akiwa mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa na uwekezaji, na Sioi akiwa mwanasheria wa benki hiyo.

Shallanda na Misana walikuwa watumishi wa Wizara ya Fedha, Shallanda akiwa kamishna wa sera wizarani hapo na Misana kamishna msaidizi wa kitengo cha madeni.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwamo ya kuisababishia Serikali hasara ya Dola 6 milioni, kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingereza.

Serikali ilivyojenga msingi wa kesi

Katika kikao cha kwanza cha usikilizwaji wa kesi hiyo kilichoanza Julai 8 hadi 19, mwaka huu, jumla ya mashahidi saba wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao kati ya mashahidi 54 wanaotarajiwa, na wakiwa wameshawasilisha vielelezo kadhaa kati ya 218 vinavyotarajiwa kuwasilishwa.

Kati ya mashahidi hao saba waliopanda kizimbani kutoa ushahidi, mashahidi sita wameshakamilisha ushahidi wao huku shahidi wa saba akiwa ametoa nusu tu ya ushahidi wake, na anatarajiwa kuukamilisha katika kikao kinachoanza leo.

Hata hivyo, katika muda huo wa siku 10 za kikao hicho cha kwanza, Serikali kupitia kwa mashahidi wote hao na vielelezo walivyoviwasilisha, haijaweza kuonyesha ni namna gani washtakiwa hao walitenda makosa wanayoshtakiwa nayo.

Badala yake, upande wa mashtaka ulitumia kikao hicho cha kwanza kuweka msingi tu wa kesi yake utakaoiwezesha kuithibitishia mahakama mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Hata hivyo, katika kujenga msingi huo wa kesi kwa kiasi kikubwa imewagusa washtakiwa wawili (Shallanda na Misana), huku Shose

akitajwa mara moja tu na shahidi kwa madai ya kuhusika kuwasilisha wizarani hapo moja ya barua za mapendekezo ya kuiwezesha Serikali kupata mkopo.

Kwa upande wao Kitilya na Sioi hadi kikao hicho cha kwanza kinamalizika, hawakuguswa kwa namna yoyote ile japo kwa kutajwa katika ushahidi.

Chanzo cha kesi

Chanzo cha kesi hiyo ni mkopo ambao Benki ya Standard ya Uingereza (Standard Bank PLC, London) kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic Tanzania (Stanbic Tanzania Ltd) ziliiwezesha Serikali kupata Dola 600 milioni badala ya Dola 550 zilizotajwa awali, kwa ada ya uwezeshaji asilimia 2.4.

Serikali inadai kuwa washtakiwa hao walishirikiana na kupanga uhalifu kwa kughushi barua ya Standard Bank na Stanbic, kuonyesha kwamba zilikuwa zimefanya marekebisho katika vigezo na masharti hususan ada ya uwezeshaji wa mkopo, na nyaraka nyingine mbalimbali.

Inadai kuwa marekebisho hayo ya kughushi yalilenga kuonyesha kuwa benki hizo zimeongeza ada ya uwezeshaji upatikanaji mkopo kutoka asilimia 1.4 ya mkopo ya awali hadi asimilia 2.4 ya mkopo halisi.

Kwa mujibu wa mashtaka na maelezo ya kesi ya upande wa mashtaka, kutokana na ongezeko hilo la kughushi la asilimia moja ya uwezeshaji wa mkopo, washtakiwa hao walijipatia Dola 6 milioni.

Kiasi hicho cha fedha ni asilimia moja inayodaiwa kughushiwa katika mkopo uliopatikana wa Dola 600 milioni, hivyo kuisababishia Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha, ambazo pia wanadaiwa kuzitakatisha.

Hivyo upande wa mashtaka katika kujenga msingi wa kesi yake ambao utaiwezesha kuthibitisha mashtaka hayo, ulianza kuwaita mashahidi kuelezea uwepo wa mchakato na mkopo huo, utaratibu wa mikopo kama hiyo, hatua zinazopitiwa na wahusika na namna wanavyofanya kazi.

Pia, imewasilisha vielelezo ambavyo vinajenga msingi wa kesi, ambavyo ni nyaraka zinazoonyesha kuwepo kwa mchakato na hatimaye mkopo huo.

Mashahidi

Mashahidi hao ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha wa wakati huo, Mustafa Mkulo, aliyefungua pazia la ushahidi, yaani shahidi wa kwanza (first prosecution witness –PW1) na PW2, Mgonya Benedict, ambaye ni kaimu kamishna wa sera wa wizara hiyo.

Hawa walielezea kwa kirefu sababu za Serikali kuhitaji mikopo ya aina hiyo, ambayo waliita ni ya masharti nafuu ni kufidia upungufu katika bajeti ya Serikali baada ya kupitishwa, ili kutekeleza miradi mbalimbali.

Pia, walieleza utaratibu kuwa baada ya bajeti kupitishwa na kuona upungufu Serikali huziomba taasisi mbalimbali za kifedha kuwasilisha mapendekezo ya kuiwezesha kupata mkopo kwa kiasi ambacho inahitaji au taasisi hizo zenyewe kuwasilisha mapendekezo hayo baada ya bajeti kupitishwa.

Walieleza kuwa mapendekezo hayo ambayo huwasilishwa kwa katibu mkuu au kwa waziri moja kwa moja, huonyesha taarifa mbalimbali, kama vile kiasi cha mkopo ambacho zinaweza kuiwezesha Serikali kuupata, riba, ada ya uwezeshaji na muda wa kujipanga kabla ya kuanza kurejesha mkopo.

Baada ya kupokea barua hizo, katibu mkuu au waziri huelekeza zipelekwe idara ya sera, kwa kamishna wa sera, ambaye ndiye ana jukumu la kutafuta vyanzo vya fedha ili kujazia upungufu katika bajeti ya Serikali, ikiwamo mikopo na mikopo ya masharti nafuu.

Hivyo sekretarieti ya idara ya sera hufanya uchambuzi wa awali wa mapendekezo ya mikopo kutoka taasisi za fedha kabla ya kuyapeleka katika hatua zinazofuata hususan katika vyombo vingine vinavyohusika na ushauri hadi kwa waziri ambaye hufanyia kazi ushauri na mapendekezo hayo.

Vyombo hivyo vya ushauri wa masuala ya mikopo ni kamati ya wataalamu ya usimamizi wa madeni (TDMC) na kamati ya taifa ya usimamizi wa madeni (NDMC).

TDMC hutoa ushauri wa kitaalamu kwa NDMC na NDMC humshauri waziri wa fedha kuhusu masuala yote yanayohusu Serikali kukopa ndani na nje.

Hivyo mashahidi hao walieleza kuwa mapendekezo ya mikopo yanapowasilishwa baada ya kufanyiwa uchambuzi wa awali na idara ya sera, hupelekwa na kufanyiwa uchambuzi na TDMC ambayo baadaye huwasilisha uchambuzi na mapendekezo au ushauri kwa NDMC, nayo huwasilisha mapendekezo yake kwa waziri.

Mashahidi hao walidai wote walieleza kuwa TDMC ambayo inaundwa na wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali za kifedha na kisheria kutoka bara na Zanzibar, mwenyekiti wake ni kamishna wa sera na katibu wake ni kamishna msaidizi wa madeni.

Walibanisha kuwa kamishna wa sera wakati huo alikuwa mshtakiwa wa nne, Shallanda; na kamishna msaidizi wa madeni alikuwa mshtakiwa wa tano, Misana.

Pia, walibainisha kuwa NDMC ambayo pia huundwa na wakuu wa taasisi na idara mbalimbali za Serikali Bara na Zanzibar zikiwamo za kifedha ambayo mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, na katibu wake ni kamishna wa sera.

Mkulo alieleza kwenye ushahidi wake kuwa wakati akiwa Waziri wa Fedha, katika mwaka wa fedha 2011/2012 kulikuwa na upungufu wa Dola za Marekani kama 800 milioni na katika bajeti, hivyo Serikali ikaanza mchakato wa kutafuta mkopo kufidia upungufu huo.

Alieleza kuwa katika mchakato huo taasisi mbalimbali za kifedha zikiwamo benki za Stanbic Tanzania na Standard ya Uingereza zikishirikiana, ambazo ziliwasilisha pendekezo kwake la kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekani 550 na maelezo yote muhimu kuhusu mkopo huo.

Alidai kuwa benki hizo zingeweza kuiwezesha Serikali kupata mkopo huo kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 1.4 ya mkopo huo na kwa riba ya asilimia 6.5 na muda wa kuanza kulipa ulikuwa miaka saba.

Alieleza kuwa baada ya kuisoma aliandika maelekezo juu ya barua hiyo akimwelekeza katibu wake aipeleke kwa kamishna wa sera kwa ajili ya uchambuzi na kisha iwasilishwe kwa TDMC kuendelea na hatua nyingine zinazofuata.

Hata hivyo, alidai kuwa baadaye aliamua mchakato huo usitishwe hadi mwaka uliofuata baada ya kushauriwa na wataalamu kuwa wakati huo mwaka ulikuwa unaelekea kuisha.

Alidai hata hivyo, Mei 2012 aliondoka katika wizara hiyo na kwamba hadi anaondoka mchakato huo ulikuwa bado haujakamilika, lakini mwaka 2016 aliitwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhojiwa kuhusiana na mchakato wa mkopo huo.

Mkulo alidai kuwa huko ndiko alipofahamu kuwa baadaye mkopo huo ulitolewa tena Dola 600 milioni badala ya 550 milioni na kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4 badala ya asilimia 1.4 ya awali, kiwango ambacho alidai kilikuwa kikubwa.

Vielelezo na jinsi kina Kitilya walivyopinga

Baada ya mashahidi hao kutoa maelezo hayo ya msingi katika kesi hiyo, hatua iliyofuata ni upande wa mashtaka kuanza kuwasilisha mahakamani vielelezo mbalimbali ili viwe sehemu ya ushahidi wake ili kuunga mkono ushahidi wa maneno ya awali uliotolewa na mashahidi hao wa awali.

Vielelezo hivyo ni nyaraka mbalimbali zinazohusiana kwa kiasi kikubwa na suala la msingi yaani mkopo na vichache vinavyohusu taarifa za baadhi ya washtakiwa hususan waliokuwa watumishi wa wizara, ili kuthibitisha kuwa kweli walikuwa watumishi wa umma na kwa nyadhifa zilizotajwa.

Vielelezo hivyo viliwasilishwa na mashahidi sita kati ya saba waliotoa ushahidi wao, baada ya upande wa mashtaka (mawakili wa Serikali) wanaoendesha kesi hiyo, kupangua na kuvuka vikwazo vyote vya mapingamizi kutoka kwa mawakili wa washtakiwa.

Ushahidi wa vielelezo katika kesi yoyote huwa ni wa muhimu kwa upande wowote na hasa nyaraka, iwe ni upande wa mashtaka (kesi za jinai) au madai (kesi za madai).

Vielelezo hivi hurahisisha jukumu la kuthibitisha mashtaka au madai dhidi ya washtakiwa, wadaiwa na kwa upande wa utetezi (yaani washtakiwa au wadaiwa) huwarasishia utetezi wao kwa kuvunja nguvu ushahidi wa upande wa mashtaka au madai.

Kutokana na umuhimu wa vielelezo hivyo, nyaraka ambazo ndizo zinazothibitisha kuwepo kwa suala linalobishaniwa na ambalo ndilo chanzo cha kesi, kutokuwepo kwake mahakamani kungeifanya hata kesi hiyo upande wa mashtaka kutokuwa na nguvu sana, hivyo kuwapa washtakiwa urahisi wa kujitetea.

Hivyo mawakili wa washtakiwa katika kesi hii hawakuwa tayari kuona vielelezo hivyo vinaingia mahakamani kirahisirahisi tu ili viweze kutumika kama sehemu ya ushahidi dhidi ya wateja wao.

Badala yake walifanya kila juhudi kupinga vielelezo hivyo vya upande wa mashtaka kwa kutumia hoja mbalimbali za kisheria ili visipokelewe mahakamani na kuwa sehemu ya ushahidi wake.

Hoja zao za mapingamizi zilijikita ama kwa uhalali wa nyaraka hizo au kwa mashahidi walioomba kuziwasilisha, wakidai kuwa hawakuwa na mamlaka ya kuziwasilisha mahakamani au vyote.

Mapingamizi hayo yaliibua mvutano mkali wa kisheria dhidi ya mawakili hao wa utetezi na waendesha mashtaka (mawakili wa Serikali), ambao nao walikuwa wakizipinga vikali hoja hizo za mapingamizi, wakiomba mahakama izitupilie mbali na ivipokee vielelezo hivyo, wakidai kuwa hazikuwa na mashiko kisheria.

Katika kujibu hoja hizo mawakili hao wa Serikali walikuwa wakitumia sheria na vifungu vilevile vilivyokuwa vinatumiwa na mawakili wa utetezi au na vingine vya kisheria pamoja na uamuzi wa kesi mbalimbali, zilizokwishakuamriwa hasa na Mahakama ya Rufani kuhusiana na hoja husika.

Kutokana na mapingamizi hayo na hoja nzito zilizokuwa zikitolewa na mawakili wa pande zote, Jaji Banzi alikuwa akilazimika kusitisha kuendelea na usikilizaji.

Badala yake Jaji Banzi alikuwa akiahirisha usikilizwaji kwa ajili ya kwenda kupitia au kufanya rejea katika vifungu na kesi mbalimbali. Pia kufanya utafiti zaidi katika tafsiri ya vifungu hivyo na kesi rejea zilizokuwa zikitumiwa, hata kwa kutafuta za kwake nyingine zaidi, kabla ya kutoa uamuzi.

Hata hivyo, juhudi zote za mawakili wa utetezi kupinga vielelezo hivyo visipokelewe mahakamani, ziligonga ukuta baada ya mahakama kutupilia mbali hoja zao za mapingamizi.

Badala yake mahakama ilivipokea vielelezo vyote baada ya kukubaliana na hoja za upande wa mashtaka za majibu ya mapingamizi hayo.

Vielelezo vya ushahidi vilivyopokewa

Vielelezo hivyo vilivyokwishawasilishwa mahakamani ni barua ya kwanza ya mapendekezo ya mkopo ya Stanbic Tanzania kwa kushirikiana na Standard ya Uingereza, iliyowasilishwa mahakamani na Mkulo, na ambayo iliwasilishwa kwake na benki hizo.

Barua hiyo ya Februari 21, 2011 inapendekeza mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 1.4 ya mkopo halisi.

Pia, zimewasilishwa barua za uteuzi wa Shallanda na Misana zinazothibitisha utumishi wao katika Wizara ya Fedha. Barua hizo ziliwasilishwa mahakamani na shahidi wa tatu, Grace Sheshui, ambaye ni kaimu mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu, Wizara ya Fedha na Mipango.

Barua ya kwanza inaonyesha uteuzi wa Shallanda kuwa kamishna wa sera, iliyoandikwa na kusainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ramadhani Khijja, Oktoba 15, 2010, uteuzi ulioanza tangu Oktoba Mosi, 2010.

Barua nyingine ya uteuzi wa Misana kuwa kamishna msaidizi kitengo cha madeni iliyoandikwa na kusainiwa na aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Servacius Likwelile, Juni 19, 2013, uteuzi ulioanza Agosti Mosi, 2013.

Hivi ndivyo vielelezo pekee ambavyo vilipokewa mahakamani bila ya kupingwa hata na washtakiwa wenyewe.

Mbali na hivyo kielelezo kingine ni muhtasari wa kikao cha kamati ya wataalamu ya usimamizi wa madeni (TDMC), kikao cha 61 cha Septemba 18, 2012 cha uchambuzi wa mapendekezo ya mkopo ya Stanbic na Standard. Katika kikao hicho Shallanda ndiye aliyekuwa mwenyekiti na Misana akiwa katibu.

Kielelezo kingine ni kitabu kilichokuwa kinatumika kuweka kumbukumbu ya barua zilizokuwa zinapokewa katika idara ya sera, mwaka 2012, kinachoonyesha kupokewa kwa barua nyingine ya mapendekezo ya mkopo kwa Serikali kutoka benki za Stanbic na Standard, Juni 26, 2012.

Kiliwasilishwa mahakamani na shahidi wa nne wa upande wa mashtaka, Amisa Nyambi, msaidizi wa mtendaji mkuu idara ya sera Wizara ya Fedha na Mipango.

Wakati huo alikuwa mwandishi mwendeshaji ofisi ya idara ya sera, majukumu yake yakiwa ni kupokea na kuweka kumbukumbu za barua zilizokuwa zikiingia ofisini hapo.

Alidai kuwa majukumu yake yalikuwa kupokea barua mbalimbali zilizokuwa zinaingia ofisini hapo, na kwamba Juni 26, 2012 alipokea barua ya mapendekezo ya uwezeshaji wa mkopo kwa Serikali, ikitoka Benki ya Standard.

Barua nyingine ya mapendekezo ya mkopo kwa Serikali kutoka kwa benki za Stanbic na Standard, ya Agosti 2, 2012 iliwasilishwa ofisi ya kamishna wa sera, Agosti 6, 2012,

Iliwasilishwa na shahidi wa sita, Neema Chelelo, ambaye wakati huo alikuwa mwandishi mwendeshaji kitengo cha madeni.

Alidai, yeye ndiye aliyeipokea barua hiyo akaipeleka kwa mkuu wake wa kazi, Misana (mshtakiwa wa tano) na kwamba baada ya hapo hakuiona tena barua hiyo ikitoka.

Nyaraka nyingine muhimu

Nyaraka hizo ni zile zinazohusu mchakato wa mkopo wa Dola 600 milioni uliotolewa na Benki ya Standard ya Uingereza kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic Tanzania, mwaka 2013, ambazo ndizo kiini cha kesi hiyo.

Miongoni mwake ni muhtasari wa kikao cha NDMC, makubaliano ya benki ya Standard na Stanbic katika kuiwezesha Serikali kupata mkopo huo, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na maelekezo ya aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Dk. William Mgimwa.

Nyaraka hizo ziliwasilishwa mahakamani hapo na shahidi wa saba, Deodata Makani, ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto.

Shahidi huyo ambaye hakuwemo katika orodha ya awali ya mashahidi 54 waliotajwa na upande wa mashtaka aliongezwa katika kesi hiyo baada ya kuanza kusikilizwa baada kugundua kwamba ni muhimu kwani ndiye anayeweza kuziwasilisha mahakamani nyaraka hizo kwa kuwa ndiye aliyeshughulikia.

Mwaka 2011 haadi 2016 alikuwa akifanya kazi Wizara ya Fedha na Uchumi, akiwa na wadhifa huo alionao sasa huko alikohamishiwa na pamoja na mambo mengine majukumu yake yalikuwa ni kutunza nyaraka zote za wizara.

Hadi kikao cha kwanza cha usikilizwaji wa kesi hiyo kinaisha shahidi huyo alikuwa hajamaliza ushahidi wake.

Hivyo Mahakama wakati ikipokea nyaraka hizo iliamuru shahidi huyo afike mahakamani kuendelea na ushahidi wakati kesi hiyo itakapoendelea tena katika kikoa kingine ambacho kinaanza leo.

Katika hatua hiyo mahakama iliamuru aje kuelezea kilichomo ndani ya nyaraka hizo na kuhojiwa maswali na mawakili wa utetezi.