KKKT watoa salamu za Pasaka wakitaka uchaguzi huru na haki

Moshi/Mwanza. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeisihi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kwa uaminifu, uhuru na haki.

Kanisa hilo limesema haki na kweli ikitamalaki katika taasisi au taifa lolote, umoja, mshikamano na amani ya kweli hujengwa na kwamba palipo na mambo hayo matatu maendeleo ya watu huwa ni dhahiri.

Ushauri huo umetolewa na mkuu wa KKKT, Askofu Fredrick Shoo katika salamu zake za Pasaka kwa waumini wao ambazo zimesambazwa katika sharika zote nchini.

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 2020 na tayari NEC imeanza mchakato wa uchaguzi kwa kuboresha daftari la kupigia kura na tayari Rais John Magufuli ameahidi uchaguzi huru na wa haki.

Rais alitoa ahadi hiyo alipokutana na mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa kuuaga mwaka uliopita.

Katika salamu hizo za Pasaka, mkuu huyo wa KKKT ametoa wito kwa raia wote kujiandikisha na kushiriki kupiga kura na kutaka kazi hiyo itendeke katika mazingira ya upendo, ukweli, uhuru na haki.

“Watakaogombea nafasi za uongozi au uwakilishi wafanye hivyo bila kuchukiana, uadui, kugombana na kutendeana hila,” alisema Askofu Shoo, ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini.

“Ninaisihi sana Tume ya Taifa ya Uchaguzi isimame katika zamu yake kwa uaminifu wote. Tukumbuke kuwa haki na kweli ndio matunda yaupasao upatanisho tulioupata kwa njia ya Yesu Kristo.

“Sote tunaitwa kutenda haki na kusimama katika kweli, pasipo haya, amani haipo. Haki na kweli ikitamalaki katika taasisi au taifa lolote, basi umoja, mshikamano na amani ya kweli hujengwa. Kama Kristo alivyosukumwa na upendo akaja kutupatanisha na Mungu, kupitia kifo chake pale msalabani, basi na sisi Wakristo na taifa zima tutafute kupatanishwa kati yetu.”

Alisema kabila, cheo, rangi, jinsi wala itikadi visitufanye kugawanyika wala kutengana na kudhalilishana.

“Upendo, upatanisho, haki, amani na kweli uwe wimbo wetu kama taifa,” alisema.

“Kanisa kama taifa la Mungu tunapaswa kuwa mfano na kielelezo katika haya yote, ndipo tunaweza kuwa sauti ya kinabii na ya utetezi kwa wale wanaoonewa na kuteswa.”

Pia Askofu Shoo alizungumzia ugonjwa wa virusi vya corona ambao umeshaua zaidi ya watu 91,000 kote duniani, kwa mujibu wa worldometer.com.

“Wakristo wanaadhimisha Sikukuu ya Pasaka wakati dunia nzima imejaa hofu na mahangaiko kutokana na janga la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona,” amesema.

“Hakika janga hili limeitikisa dunia. Sote tumeguswa na tutaguswa na janga hili kwa namna moja ama nyingine. Tunatakiwa kuendelea kuchukua kila tahadhari na kufuata maelekezo ya wataamu wa afya.”

Alisema Mungu anao ujumbe kwa Wakristo kujinyenyekeza na kumrudia Mungu kwa toba, akisema kujinyenyekeza si udhaifu bali kinyume chake ni kiburi, majivuno na matumizi mabaya ya madaraka.

Maskofu Munga, Bagonza

Salamu za Pasaka pia zilitolewa na maaskofu wengine wawili wa KKKT, Dk Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe na Dk Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambao wamesihi Watanzania kutumia maadhimisho hayo kama alama ya tendo la kuponya maisha ya kila mtu na jirani yake.

“Tunaitwa kuvumilia mateso tunapokuwa katika kutetea haki kwa sababu Bwana yu upande wetu. Hakumwacha mwana wake, hawezi kutuacha sisi,” amesema.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Peter Saramba na Burhani Yakub.