Kabudi aihakikishia dunia uchaguzi huru na wa haki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amerudia ahadi ya Rais John Magufuli alipoiambia jumuiya ya kimataifa kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa wazi, huru na wa haki.

Alikuwa akirudia ahadi ambayo Rais Magufuli aliitoa kwa mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukaribisha mwaka mpya.

Ahadi kama hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene aliyekutana na mabalozi na kuwahakikisha uchaguzi huru na haki.

Jana, Profesa Kabudi alirudia ahadi hiyo wakati akihutubia kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linaloendelea jijini Geneva, Uswisi likiwakutanisha wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa sita tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa na uchaguzi huo utakuwa wa uwazi, huru na wa haki,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema hatua zote ambazo zimechukuliwa na Bunge kwa kufanya mabadiliko katika Sheria za Vyama vya Siasa, Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na ile ya Vyombo vya Habari zina lengo la kuimarisha uwajibikaji na uwazi pamoja na kuhakiskisha misingi na tunu za Taifa zinaheshimiwa na kuendelezwa.

Alisema Tanzania itawaalika waangalizi wa uchaguzi watakaotaka kushuhudia namna Watanzania wanavyotekeleza moja ya haki zao za msingi katika suala la kidemokrasia kwa kuchagua viongozi wao.

Wakati Profesa Kabudi akisema hayo, kilio kikubwa cha vyama vya siasa ni kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, vikisema kuwa mfumo wa sasa unawapa mamlaka wakurugenzi kusimamia uchaguzi wakati ni wateule wa Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala.

Waziri Kabudi pia alisema Tanzania inaheshimu na itaendelea kuheshimu haki zote za binadamu zikiwemo za kisiasa na kwamba sheria zilizotungwa na Bunge zina lengo jema la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa Taifa lenye amani, umoja na utulivu.

Alisema madai dhidi ya Tanzania kuwa inakiuka haki za binadamu ni propaganda zinatokana na hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, dawa za kulevya, uzembe katika ofisi za umma pamoja na hatua zinazochukuliwa kulinda rasilimali za Taifa.

Kuhusu sheria mpya za Huduma za Vyombo vya Habari na Haki ya Kupata Taarifa, Profesa Kabudi alisema zimetungwa kuimarisha, kulinda na kuweka mazingira bora kwa waandishi wa habari.

Katika tukio jingine, Profesa Kabudi alifanya mazungumzo na katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia Scotland kuhusu masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na mradi ambao Jumuiya ya Madola imeifanya Tanzania.

Mradi huo umelenga kuangalia takwimu mbalimbali zinazohusu biashara kwa kuangalia nchi ambazo Tanzania inaagiza ama kuuza bidhaa zake kwa wingi katika nchi za Jumuiya ya Madola. Mradi ambao umeelezwa kuwa na manufaa kwa Tanzania ana kwa sasa nchi za India na Afrika Kusini ndiyo kinara.

Kwa upande wake, Scotland alisema kwamba Tanzania ni mdau muhimu katika jumuiya hiyo na kwamba alifurahi kumkabidhi Profesa Kabudi nakala ya utafiti huo kwa niaba ya Serikali, jambo litakaloifanya Tanzania kuendelea kuangalia maeneo ya kujiimarisha katika ufanyaji wa biashara na nchi za Jumuiya ya Madola.

Mbali na masuala hayo, wawili hao walizungumzia masuala mengine ikiwa ni pamoja na namna jumuiya hiyo na Tanzania zitakavyofanya kuongeza usawa wa jinsia, masuala ya haki za binadamu pamoja na uimarishaji wa mahakama.