Kama unasumbuliwa na matatizo haya, kula boga

Je unafahamu kama boga lina protini ambayo husaidia kupambana na magonjwa yatokanayo na fangasi?

Elizabeth Lyimo ni mtaalamu wa Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe(TFNC), anasema protini ya pr-2 iliyopo katika maboga hutibu michubuko inayotokana na mkojo au nepi, huku ikizuia aina 10 za fangasi ikiwamo candida albicans ambayo ni fangasi hatari.

Fangasi hao pia ni maarufu kwa kusababisha matatizo kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari na husababisha pia, kupata fangasi midomoni, katika ngozi, chini ya kucha na kwenye mfumo mzima wa mwili.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la kilimo na kemia la vyakula, umeonyeshwa kuwa protini inayotokana na boga iitwayo Pr-2, hupambana na ugonjwa unaosababisha fangasi sehemu za siri kwa mwanamke.

“Vile vile maboga yana kiwango kikubwa cha potasiamu na alikalini ambayo utendaji na asili yake nzuri ni vitamin B na C, hivyo ulaji wa boga lililopikwa kila siku husaidia kuzuia saratani na husaidia kuleta nafuu kwa watu wanaoumwa kichwa,”anasema.

Lyimo anasema juisi ya boga lililochemshwa ni zuri kwa watoto wenye umri wa miezi sita na kuendelea.

“Katika mlo wa mtoto jaribu kumsagia kiasi kidogo cha boga lililochemshwa vizuri, angalau mara moja kwa siku,” anasema Lyimo. Mbali na maboga, pia mbegu zake zimesheheni protini na madini mbalimbali kama chuma, kopa, maginizia na manganizi. Pia, anazitaja faida za ulaji wa maboga na mbegu zake katika mwili wa binadamu kuwa maboga hupunguza mafuta kwenye mishipa ya damu.

Pia, ulaji wa mara kwa mara wa mbegu hizo huzuia ugonjwa wa kiharusi, mshtuko wa moyo na kusaidia ufanisi wa utumbo mkubwa kufanya kazi vizuri.

Anasema maboga huzuia saratani kutokana na mafuta yaliyopo, huimarisha kinga za mwili na ukuaji wa seli.

Pia, kwa wale wanaokosa usingizi hawana budi kutumia mbegu za maboga pale wanapotaka kulala. Kwa muda mrefu, maboga yamekuwa yakitumika katika tiba za kiasili kutibu kisukari, shinikizo la damu.