Katibu Mkuu atakiwa kutoa ‘mapepo’ Mambo ya Ndani

Rais John Magufuli akimuapisha Brigedia Jenerali, Suleiman Mzee kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam jana. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemtaka katibu mkuu mpya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Chritopher Kadio kwenda kutoa alichokiita kuwa ni ‘mapepo; katika wizara hiyo.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana Ikulu, Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.

Pia, Rais Magufuli alieleza sababu za kumteua Brigedia Jenerali wa JWTZ kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza na kueleza mkakati wa kuiboresha Wizara ya Mambo ya Ndani aliyodai ‘ina mapepo’ yanayopaswa kuondolewa.

Jana si mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuizungumzia hivyo wizara hiyo aliyoifanyia mabadiliko kwa kumtoa Kangi Lugola na kumteua George Simbachawene na kuridhia aliyekuwa Katibu Mkuu Meja Jenerali, Jacob Kingu kujiuzulu.

Januari 23, Rais Magufuli alichukua uamuzi huo akidai viongozi hao na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengeye walihusika na mkataba tata wa Sh 1 trilioni wa ununuaji vifaa vya zimamoto ukiihusisha kampuni ya Romania.

Baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Magufuli alitumia dakika 26 kuwaelezea aliowaapisha.

Alisema Kadio alikuwa katibu tawala Mwanza na alifanya kazi nzuri ikiwamo kutumia fedha zilizobaki za rambirambi baada ya kuzama Kivuko cha MV Nyerere katika Ziwa Victoria Septemba mwaka jana na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 100.

Rais Magufuli alisema Kadio na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella walijenga hospitali kubwa nzuri ya wilaya, “na alikuwa anajenga kituo cha kupokea abiria Mwanza kwa kutumia ‘force account.”

“Tukafikiri tumpeleke Mambo ya Ndani ambayo ina mapepo akayaombee. Wakashirikiane na Simbachawene. Tumempeleka pale kwa sababu lazima tumpeleke mtu ambaye yuko ‘committed,” alisema.

Kuhusu Dk Hassan Abbas ambaye alikuwa mkurugenzi Idara ya Habari- Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye jana aliapishwa kuwa katibu mkuu Wizara ya Habari, alisema, “amefanya kazi nzuri, hakuchoka, aliisemea vizuri Serikali. Ningependa aendelee tu kuwa msemaji wa Serikali lakini mahali mtu anapotakiwa kupandishwa usimnyime. Ataendelea kuwa msemaji wa Serikali mpaka tutakapopata mwingine na atakuwa anasema sasa akiwa mkubwa zaidi,” alisema.

Rais pia alisema amemteua Brigedia Jenerali Suleiman Mzee kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza akichukua nafasi ya Phaustine Kasike aliyeteuliwa kuwa balozi.

Pia, Rais Magufuli alimwapisha Naibu Kamishna Magereza, John Masunga kuwa Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji. Masunga amechukua nafasi ya Andengenye ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Viongozi wengine walioapishwa ni Profesa Riziki Shemdoe kuwa Katibu Mkuu Viwanda na Biashara, Zena Ahmed Said (Katibu Mkuu Nishati). Leonard Masanja (naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati) ambaye kabla ya kuteuliwa alikuwa kamishna wa umeme na nishati mbadala.

Wengine walioapishwa ni makatibu tawala (RAS) wapya wa mikoa mitatu ambao ni Judica Omari (Tanga), Stephen Mashauri (Ruvuma) na Emmanuel Turuba (Mwanza).

Pia, Rais Magufuli alimwapisha Nathaniel Nhonge kuwa Kamishna wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi; Wilbert Chumakuwa kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama, Kelvin Mhina kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na Shamira Sarwat anayekuwa Msajili wa Mahakama Kuu.

Wengine walioapishwa ni Jaji Gerald Ndika, Wakili Julius Kalolo Bundala na Wakili Genoveva Kato wanaokuwa makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Mzee aliingia ukumbini akiwa amevalia sare na vyeo vya Brigedia Jenerali vya JWTZ sawa na Masunga aliyevaa sare za Magereza na vyeo vyake vya Naibu Kamishna kisha baadaye wakaenda kubadilisha mavazi. Mzee akavaa ya Magereza na Hasunga akavaa ya Zimamoto kisha Rais Magufuli akawavalisha vyeo vyao vipya.

“Mzee ni miongoni mwa ma-Brigedia Jenerali wanaochapa kazi sana, yeye alikuwa mkuu wa kamandi ya Pangawe, aliikuta iko chini, akaisimamia vizuri, akajenga nyumba, akanunua magari kwa kutumia ‘force account,’ hakaagi ofisini.”

“Sasa nilipokuwa napata matatizo Magereza namna ya kumtafuta hapatikani mwingine nikichunguliA hivi inashindikana, nikasema lakini wote si wanafundishwa kozi moja, mguu pande, mguu sawa, kulia geuka mwili legeza nikaona nimpeleke huyu,” alisema.

Rais Magufuli alisema, “niliona nikiteua wa chini wale wa juu watamdharau na wa juu zaidi anafanya kazi vizuri lakini amebakisha miezi minne kustaafu, anayefuatia naye anafanya kazi nzuri ila kwa nafasi ya kamishna jenerali hatatusaidia sana lakini ni mama mhandisi mzuri sana, nazungumza ukweli.”

“Nikaona ngoja nimpelekee huyu brigedia kwa sababu haiwezekani nyumba zikitaka kujengwa unapeleka watu wa JKT wakati wana wafungwa wanakula tu mle ndani. Hicho kilikuwa kinaniumiza kweli,” alisema.

Akimzungumzia bosi mpya wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Rais Magufuli alisema, “Hasunga yeye alikuwa Magereza, alikuwa nafikiri namba tatu au nne, ukimteua palepale Magereza halafu kuna watatu au wanne wamemtangulia, nilijua atapata shida kama aliyeondoka kwa sababu walimwachia tu.”

“Anazunguka kule, anaeleza saa ingine anafanya kikao hadi saa saba wengine wamelala, hakupata ushirikiano mzuri na yeye hakutaka kutumia intelijensia vizuri kujua je anasafiri na watu au anasafiri peke yake, katika kufanya mabadiliko nikaona nimpeleke Zimamoto, ni matumaini yangu yale aliyoyafanya aliyekuwako huko hatafanya huko, kafanya kazi,” alisema.

Viongozi wengine walioapishwa ni Profesa Riziki Shemdoe kuwa Katibu Mkuu Viwanda na Biashara, Zena Ahmed Said (Katibu Mkuu Nishati). Leonard Masanja (naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati) ambaye kabla ya kuteuliwa alikuwa kamishna wa umeme na nishati mbadala.

Walichokisema walioapishwa

Baada ya kuapishwa, Dk Abbas alisema anakwenda kufanya mageuzi katika sekta zilizo katika wizara hiyo kwa sababu anaifahamu vizuri.

Dk Abbas alisema anakwenda kuendeleza jitihada alipoishia mtangulizi wake na kwamba katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu akiwa Msemaji wa Serikali, alipitia vipindi vigumu kama vile majanga yaliyotokea likiwano lile la kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.

“Nimekuwa kwenye wizara hii, nazifahamu vizuri sekta zote za habari, michezo na sanaa. Baada ya siku mbili nitatoa vipaumbele vyangu lakini ninakwenda kufanya mageuzi makubwa kama nilivyofanya nilipokuwa Msemaji wa Serikali,” alisema Dk Abbas.

Naye Zena alisema anafahamu kwamba kipaumbele kikubwa cha Serikali kwa sasa ni kuhakikisha umeme wa uhakika na bei nafuu unapatikana hapa nchini, hivyo, atakwenda kushirikiana na watendaji wengine wizarani kuhakikisha azma hiyo inafanikiwa.

“Kwa sasa tumeamua kujenga viwanda na viwanda vinahitaji umeme wa uhakika, ni wajibu wangu kusimamia utekelezaji wa suala hilo. Nitashirikiana na wenzangu wizarani ili kupata umeme wa uhakika,” alisema.

Naye Kamishna Jenerali Masunga alisema amejipanga kwenda kukabiliana na changamoto ya vitendea kazi katika jeshi hilo na kwamba kazi hiyo itakuwa rahisi kwake kwa sababu Serikali inafahamu changamoto hiyo.