Kauli za Mbatia kuhusu wapinzani zaibua mjadala

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia akisisitiza jambo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na waandishi waandamizi wa gazeti la Mwananchi, alipotembelea chumba cha habari cha magazeti ya Mwananchi Communications Limited, Tabata, jijini Dar es Salaam, Jumatatu ya wiki hii. Picha na Salim Shao

Dar es Salaam. Wasomi na wachambuzi wa siasa nchini wamesema kauli zinazotolewa na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia siku chache baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam zinatia shaka, zinaweza kuwagawa wapinzani.

Wameeleza hayo baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu kauli za Mbatia tangu wawili hao wakutane Machi 3, na alichokisema jana katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Mbeya kuwa hajatumwa na Rais Magufuli kuiangusha Chadema katika majimbo ya Rungwe, Busokelo na Kyela katika uchaguzi ujao.

“Nimekuja Mbeya katika ziara ya kukiimarisha chama cha NCCR. Si kwamba nimetumwa na Rais Magufuli kuja kuiua Chadema,” Mbatia aliwaambia waandishi wa habari.

“Hiyo ni hofu yao, majungu na ufike wakati kujenga hoja za fikra.”

Lakini utetezi wake haujawazuia wachambuzi kukosoa kauli anazotoa, wakisema zinatia shaka na kwamba anaongeza mtaji kwa CCM na kuwavuruga wafuasi wa upinzani, huku baadhi wakiamini ni njia sahihi ya NCCR kujijengea mtaji baada ya kutonufaika na Ukawa mwaka 2015.

Wamesema mazungumzo yake na Rais yatapimwa kwa vitendo au kauli atakazoendelea kutoa kuelekea uchaguzi ujao.

Mbatia, Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad wameshaenda Ikulu mara mbili kila mmoja, huku mshauri huyo wa ACT Wazalendo akisema mwaliko wake wa safari hii ulitokana na barua tatu alizoomba kukutana na Rais.

Siku moja kabla ya kuanza ziara, Mbatia na Rais Magufuli walifanya mazungumzo ya faragha.

Baadaye mchana, Mbatia alikutana na waandishi wa habari na kumpokea katibu mwenezi wa zamani wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Edward Simbeye na kisha kutangaza kuanza ziara ya kukiimarisha chama hicho.

“Nakumbuka diwani wetu wa Tarime, Chacha Wangwe alijiunga na Chadema na akawa mwenyekiti wa mkoa, hatukulalamika. Ni utaratibu tuliojiwekea, vyama vyote kwa ujumla navishauri tuzungumzie utaifa wetu, tushindane kwa hoja,” alisema Mbatia Machi 3.

Kwa mara nyingine, jana katika hotuba yake, Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), alisema vyama vya siasa vinajidanganya kuwa ni bora kuliko vyama vingine, akisema hakuna chama wala serikali yenye nchi.

“Kila chama kina haki ya kushika dola na kuongoza wananchi na ndio maana Hayati Baba wa Taifa aliingiza mfumo wa vyama vingi ili kushindana kwa hoja na si matusi, kejeli na propaganda zisizo na maslahi mapana kwa Watanzania,” alisema Mbatia.

Wakizungumza na gazeti hili kwa wakati tofauti, Dk Richard Mbunda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alitafsiri kauli hizo katika mitazamo miwili, akiamini huenda ikawa ni sehemu ya matokeo ya kikao chake na Rais Magufuli.

“Kwanza ijulikane Mbatia ni mwanasiasa na alienda Ikulu kwa malengo maalumu ambayo hayakuwekwa wazi, kwa hiyo matokeo ya mambo waliyozungumza labda tutaiona kidogokidogo kwa matendo, matamshi na katika mahusiano yake kwa CCM na upinzani,” alisema Dk Mbunda.

“Sehemu ya pili katika mtazamo wangu, namuona Mbatia kama mwanasiasa anayepiga hesabu za kuongeza ushawishi kabla ya majadiliano ya muungano wa vyama kisheria. Kwa hiyo anaweza kuwa anajiandaa kuomba share (mgao) unaoridhisha katika majimbo, isiwe kama 2015.”

Katika makubaliano ya mwaka 2015 ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Chadema ilipata nafasi nyingi zaidi za ubunge na udiwani Tanzania Bara, huku CUF ikipata nafasi nyingi visiwani.

Makubaliano hayo yalizingatia kukubalika kwa chama au mgombea katika eneo ndiko kungemuwezesha apitishwe na vyama vyote vinne.

Dk Mbunda alisema changamoto aliyonayo Mbatia ni kuhakikisha anapata mtaji wa kutosha ili kuwa na mgawo mkubwa endapo kutakuwa na makubaliano hayo ya kisheria ya muungano wa vyama.

Msomi mwingine, Profesa Mohamed Bakari alisema kauli za Mbatia zinaonyesha wazi hamasa ya Ukawa kwa sasa haipo.

“Ukawa unaweza kuwapo lakini kwa kauli anazotoa kwa sasa zinanaashiria ya kuwepo Ukawa hamasa imepungua sana,” alisema.

“Lakini pia hatuwezi kujua mazungumzo yao ya siri Ikulu yalikuwaje. Lakini kwa kauli za Mbatia zinaweza kujenga hisia kwa umma kwamba kuna ahadi fulani fulani ameahidiwa.”

Profesa Bakari alisema huenda Mbatia anadhani muungano huo wa Ukawa haukuwa na msaada 2015. Alisema katika uchaguzi huo, kuna vyama vilivyonufaika zaidi na vingine kutonufaika.

Hata hivyo, Profesa Bakari alishauri vyama vya upinzani kuwa hakuna vijenge mitaji ya vyama kushinda kuliko kusambaratika, akisema nafasi ni ndogo kwa NCCR Mageuzi kusimamisha wagombea na kushinda bila kushirikiana.

Lakini katibu mkuu wa Chadema, John Manyika hakutaka hata kujadili kauli hizo alipoulizwa na Mwananchi jana. “Kujadili hoja za Mbatia ni kuhamisha mjadala wa madai ya msingi kwa Serikali kama hoja ya tume huru ya uchaguzi,” alisema Mnyika.

Naye mkurugenzi wa Itikadi na uenezi wa Chadema, John Mrema alimshauri Mbatia kufanya siasa za kujijenga badala ya kutafuta huruma kwa wananchi.

Mbatia

“Mimi ni mwenyekiti wa Jukwaa huru la maridhiano kwa vyama vyote vya siasa nchini tuliomba kuonana na Rais naye alitukubalia sasa baada ya kutoka Ikulu nilianza ziara yangu mkoa wa Mbeya na nilipata baraka kwani vikao nilivyofanya katika majimbo hayo ni vya ndani na wala sio kampeni “ alisema.

Aliongeza kuwa, “Kila chama kina mlengo wake na Uhuru wa kuongea na Rais kwani ndio serikali iliyoshika dola ukifika wakati wa kushindana kwa hoja kila mmoja ataeleza sera zake za chama na kuziuza ka wapigakura na atakayekubalika atashika nchi ila nashangazwa kuna baadhi ya wabunge wanasema kwenye maeneo yao kuwa hilo ni jimbo langu na viongozi serikalini wanasema serikali yangu kimsingi hakuna mtu mwenye serikali wala mbunge mwenye jimbo sera za vyama ndio zitawaingiza wagombea kwenye majimbo na serikali ni,” alisema.

Alisema kuwa anashangazwa na vyama vya siasa vinajifanya vyenyewe ni bora kuliko vingine mpaka kudiliki kusahau wosia wa hayati baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuweka misingi ya vyama vingi na sasa unafika wakati mtu anataka serikali iongozwe na Chama kimoja hilo halikubaliki na badala yake turejee kwenye misingi yake ya kujenga umoja,undugu na ufike wakati kuwepo kwa midahalo ya vyama vyote kueleza Sera zao na wananchi wakasikiliza na kupina pumba na Michele.

“Hii nchi kila Chama kinapaswa kupatiwa semina za namna ya kuandaa Sera kwani tunaona wa nakwenda nje ya Sera zao kwa kushindwa kutekeleza kauli zao ambao waliwahaidi wananchi wakati wa kampeni sasa umefika wakati wa kupokezana vijiti na kuiondoa Ccm madarakani kwani wananchi wamechoka kulalamika” alisema.

Alisema mwaka 1995 NCCR Mageuzi kilikuwa Chama kikuu cha Mageuzi pekee basi ikaletwa migogoro,ubinafsi, chuki, majungu jambo lililopelekea NCCR kuwa na mwakilishi mmoja tu bungeni mwaka 2000 na sasa tumegundua wapi tulikosea tumerejea tena na kuanza maandalizi ya kuangalia wanachama watakaofaa kuwasimamisha katika uchaguzi Mkuu October 25 mwaka huu na hawatafanya makosa lengo kuwaletea maendeleo wanambeya.

“ Nasema kwa dhati ya moyo wangu tuliwakosea watanzania sasa katika makosa Yale tunaomba watusamehe sasa hayatajirudia tena na tutahakikisha majimbo yote matatu la Kyela,Rungwe, Busokelo yanarejeshwa mikononi wa Chama ili kujenga utu,umoja,mshikamano na kulisogeza taifa mbele na kukuza uchumi katika sekta ya kilimo ,miundombinu ya barabara ,Afya,elimu”alisema.