Kigwangalla asema haogopi kutumbuliwa akijibu hoja matumizi ya Sh2.58 bilioni

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla

Dar es Salaam. Joto la Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania (CAG) limesababisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla kutumia muda wake katika mitandao ya kijamii kutoa ufafanuzi kuhusu hoja za mkaguzi za matumizi ya Sh2.58 bilioni.

Na zaidi ya yote amesema haogopi uteuzi wake kutenguliwa kwa kuwa hana kosa.

Kwa siku tatu mfulululizo, baadhi ya watumiaji mtandao wa Twitter wamekuwa wakitoa maoni yao katika akaunti ya kiongozi huyo kijana, wakimtaka kujibu hoja za mapungufu yaliyoonekana katika ukaguzi au kujiuzulu ili kulinda heshima yake.

Siku tatu zilizopita, ripoti ya ukaguzi wa taarifa za fedha za Serikali kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2019, imeonyesha kuwa matumizi ya Sh2.58 bilioni yalifanywa na wizara hiyo nje ya bajeti na kabla ya kupitishwa na Bunge.

Kwa kawaida hoja hizo hujibiwa na ofisa masuhuli wa wizara ambaye ni katibu mkuu, lakini Dk Kigwangalla amekuwa akiwajibu watu wanaofuata akaunti yake, kueleza kutohusika kwake.

Kitendo kama hicho kilifanywa na mawaziri kadhaa mwaka jana baada ya CAG ripoti yake hadi mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Livingstone Kaboyoka aliposema si sahihi kwa mawaziri kuzungumzia ripoti hizo na kutoa ufafanuzi kuwa kifungu cha 38 (1) na (2) kinaipa kamati hiyo mamlaka ya kuzungumzia ripoti hizo na kutoa utaratibu wa namna ya kuzijadili.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya CAG, Wizara ya Maliasili na Utalii ilitumia fedha hizo kufanikisha kampeni ya Urithi Festival Celebration na chaneli maalum ya kutangaza vivutio vya utalii kinyume na taratibu.

Wengi waliomfuata katika akaunti yake walimtaka awajibike kutokana na dosari hiyo.

“Kuna tuhuma nyingi huwa nazipuuza. Kuna vitu vingi huwa naviacha vipite, lakini si tuhuma ya kuwa nimekula 2.58 bilioni ya umma jamani!” ameandika Kigwangwalla ambaye aliithibitishia Mwananchi kuwa akaunti hiyo ni yake.

“Hii ni nzito na huwezi na wala hupaswi kuiacha ipite. Pamoja na maelezo bado kuna mtu anakung’ang’ania tu. Tena bila ushahidi hata kidogo wa wizi.”

Dk Kigwangalla anasema kifungu cha 11 (5) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma 2008 kinampa mamlaka CAG kuchukua hatua kwa ofisa aliyetumia vibaya fedha za umma, na kwamba hakuchukua hatua kwa sababu hakuna wizi uliofanyika.

Pia, Dk Kigwangalla anasema ripoti za CAG zitajadiliwa Bunge la Februari mwakani baada ya maofisa masuhuli wote wa wizara kuitwa Kamati ya PAC kutoa ufafanuzi. Alisema baada ya hapo wananchi wataelezwa hoja kwa hoja kupitia Bunge na ukweli hubainika.

Pia ameandika: “Ripoti ya CAG ni ya kipindi kinachoishia Juni 30, 2019. Katika kipindi hicho, nilikuwa nimelazwa hospitali na baadaye kupumzika nyumbani kufuatia ajali ya gari nikiwa kazini kuitumikia nchi yangu, na nina hakika Menejimenti ya Wizara iliyokuwepo ilifuata taratibu.” Lakini pia alikuwa na majibu mengine kwa watu wanaofuatilia akaunti hiyo ambao baadhi walimtaka aachie ngazi.

Mmoja wa wafuasi wa akaunti hiyo ni Dk Meni ambaye ameandika: “Hivi aliyeleta mfumo wa kujiwajibisha unadhani alikuwa mjinga? kuwajibika bila kuwajibishwa ni dalili za ukomavu wa kifikra. Sasa nakushangaa Dr unaogopa kuachia ngazi ili ukweli ujulikane? Achia ngazi. “

Lakini Dk Kigwangalla amemwambia: “Nikiachia ngazi wewe utafaidika na nini? Na niachie ngazi kwa sababu gani? Kosa langu ni nini? Labda tuanzie hapo kwanza. Kuachia ngazi si shida sana kwangu, lakini nisaidie hayo majibu hapo kwanza!”

Baada ya Millinga kuhoji kuhusu hofu ya kutumbuliwa kwake, Dk Kigwangalla alijibu si tatizo.

Alisema kwake nafasi ya uwaziri ni fursa ya kuwatumikia wananchi na ndio maana anafanya kazi kwa juhudi.