Kikwete afichua siri ujenzi sekondari za kata

Dodoma. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amefichua kuwa uthubutu na maono ya mbali ndio siri ya ujenzi wa shule za sekondari za kata nchini enzi ya uongozi wake.

Aliyasema hayo juzi usiku katika hafla ya chakula cha hisani kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa kitega uchumi cha Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika.

Kikwete, ambaye alikuwa Rais kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, aliusifu uongozi wa kanisa hilo kwa kuwa na uamuzi wa kuthubutu kujenga kitega uchumi hicho kama serikali yake ya awamu ya nne ilivyothubutu kujenga shule za kata.

Alisema sababu ya kuamua kujenga shule hizo za sekondari kila kata ilitokana na idadi ndogo ya wanafunzi waliokuwa wakipata nafasi za kujiunga na sekondari baada ya kufaulu elimu ya msingi.

Kikwete alisema wakati wa uongozi wake, ni asilimia sita tu ya wanafunzi waliofaulu darasa la saba ndiyo waliokuwa wakipata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari.

Alisema wengi waliishia njiani kutokana na idadi ndogo ya shule za sekondari zilizokuwapo.

Hata hivyo, Kikwete alisema walipoamua kujenga sekondari hizo za kata, waliamua kuhamasisha wananchi nao wasaidie kujenga shule moja ya sekondari kila kata.

“Mwitikio ulikuwa wa ajabu sana waliposhirikishwa wananchi, sisi tulisema mkijenga tutatoa bati, lakini halmashauri nyingine zikawa dhaifu, wananchi wakaamua kujenga na kumaliza kabisa,” alisema Rais huyo mstaafu.

Alisema kuna wakati alikwenda kuzindua shule ya kata wilayani Rombo, Kilimanjaro, wananchi walimwambia wameitikia wito wa kujenga shule hizo kutokana na idadi kubwa ya watoto kukosa shule licha ya kufaulu.

“Hivyo wakaniambia kwa kipindi kile hawakutaka msaada wowote wa ujenzi bali tuwapelekee walimu kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao maana shule wameshajenga,” alisema Kikwete.

Alisema hali hiyo pia alikutana nayo wilayani Lushoto mkoani Tanga ambapo wananchi walijenga shule za sekondari saba katika kata moja kwa nguvu yao.

Kikwete alisema baadhi ya shule za kata zilianza na walimu wawili tu.

“Wakati huo, Margaret Sitta alikuwa waziri wa Elimu, siku moja akanifuata akasema baba nimepata tatizo, kwa kasi hii ya wananchi `we can’t cope’(hatutaweza kwenda na kasi), hatuna walimu. Kwa hiyo waambie waache kujenga shule, wapunguze hiyo kasi. Nikamwambia nimekusikia na nimekuelewa,” alisimulia Kikwete.

Hata hivyo, alisema alimjibu kuwa iwapo watawazuia wananchi kujenga shule hizo kwa wakati huo kwa dhana kuwa wasubiri hadi Serikali itakapokuwa tayari basi wataipunguza hamasa yao.

“Hili litatushinda, nikasema lazima tufanye kwa sababu wakati ule vijana waliokuwa wakifanya mtihani (wa kuhitimu shule ya msingi) waliokuwa wanaingia sekondari ilikuwa ni asilimia sita tu. Sasa nikaona haiwezekani tuwe na nchi ya watu waliomaliza elimu ya msingi tu.

“Sio kwamba elimu ile ilikuwa haina thamani, lakini inamwezesha mwanadamu kutawala mazingira yake na akatoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo yake mwenyewe, jamii na taifa lake, kwa hiyo ilikuwa muhimu kwa watoto kupata elimu ya sekondari, sisi changamoto yetu ibaki namna ya kupata walimu,” anasema alimwambia Sitta.

Kikwete alisema kipindi kile, vyuo vyote vilikuwa vinazalisha wastani wa walimu wenye shahada na diploma 500 kwa mwaka, lakini wakati huo walikuwa wamejenga shule za sekondari zaidi ya 3,000.

Kikwete alisema ili kutatua tatizo la upungufu wa walimu, alikutana na vyuo mbalimbali kikiwemo St John na kuwaomba waanzishe vitivo vya ualimu na kuahidi kuwa Serikali itawaajiri wahitimu wao.

Alisema hatua hiyo ilipunguza pengo la upungufu wa walimu na kwamba, wakati huo walikuwa wakiajiri hadi walimu 18,000.

Kikwete alisema mpango huo ulizaa matunda, hivi sasa walimu wa sayansi ya jamii wamekuwa wengi na wengine wanafundisha shule za msingi.

Alishauri walimu wanaomaliza vyuo vikuu hivi sasa, washuke ngazi na kufundisha shule za msingi na awali kama inavyofanyika katika mataifa yaliyoendelea ili kuboresha elimu ya Tanzania.

Alitoa simulizi ya namna walivyozungumza na Rais wa Marekani, George W. Bush alipokuja nchini mwaka 2008, alimuomba aisaidie Tanzania kupata walimu wa sayansi, lakini akamjibu hata Marekani hawakuwa na walimu wa somo hilo wa kutosha.

Alisema ombi lake jingine kwa Rais Bush lilikuwa ni kuchapishiwa vitabu vya sayansi kwa shule za sekondari, jambo ambalo alikubali na hivyo wakaondoa upungufu wa vitabu hivyo.

Hivyo, Rais huyo mstaafu alisema kutokana na uthubutu wa kufanya mambo mbalimbali, anakumbuka wakati wa kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika wakati wa utawala wake, alitumia kauli mbiu ya `Tumethubutu tumeweza na tunasonga mbele.’

Alitolea mfano kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipokea nchi kutoka kwa wakoloni kukiwa na barabara tatu tu za lami za kwenda mikoani na wahandisi wawili.

Kikwete alisema kutokana na uthubutu sasa hivi Tanzania ina wahandisi zaidi ya 18,000.

Akimkaribisha Kikwete, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dickson Chilongani alisema jengo hilo lenye ghorofa mbili litakuwa na maeneo ya kibiashara na ukumbi utakaochukua takribani watu 400.

Alisema jengo hilo litagharimu Sh5.82 bilioni na kiasi kilichokuwa kikitafutwa ni Sh3.69 bilioni.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na waziri mkuu wa zamani John Malecela na mkewe Anne Kilango na Sh296.27 milioni zilipatikana.