Kinana, Membe, Makamba wawekwa kiporo

Dar es Salaam. Shauku ya wananchi kutaka kujua hatima ya makada waandamizi wa CCM, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Bernard Membe imezidi kusogezwa mbele baada ya suala hilo kuwekwa kiporo.

Kamati Kuu ya CCM iliyokutana jana imeamua sasa suala hilo lishughulikiwe katika siku saba zijazo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema kikao cha Kamati Kuu kilichokaa chini ya Rais John Magufuli kimetoa smuda huo kwa kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama hawa watatu na kuiwasilisha katika vikao husika.

Wanasiasa hao walihojiwa kwa nyakati tofauti Dodoma na Dar es Salaam kutokana na kutuhumiwa kwa makosa ya kimaadili baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika Desemba 13 mwaka jana jijini Mwanza kuazimia waitwe na kuhojiwa.

Kinana na Makamba ni makatibu wakuu wa zamani wa chama hicho waliohojiwa Jumatatu iliyopita katika ofisi ndogo ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam na kamati ya maadili chini ya Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula wakati Membe, waziri wa zamani wa Mambo ya Nje alihojiwa wiki iliyopita.

Vigogo hao wamehojiwa baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mtu anayejiita mwanaharakati, ambaye alikuwa akitoa tuhuma dhidi yao.

Sauti hizo zilianza kusambaa mitandaoni baada ya Kinana na Makamba kuandika waraka Julai 14 mwaka jana kwenda kwa Katibu wa Baraza la Wazee la CCM, Pius Msekwa wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu huyo ambaye walisema amekuwa akiwadhalilisha na kuwa huenda alikuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Kabla ya kuhojiwa, Makamba na Kinana walizua mjadala kutotokea mbele ya kamati ya nidhamu jijini Dodoma lakini juzi wakaitikia wito katika mazingira ambayo pia yalizua maswali.

Katika picha za video zilizotolewa zikiwaonyesha kwa namna walivyofika kwenye ofisi ya CCM Lumumba, Kinana aliingia kwenye ofisi hizo wakati Makamba alionekana tu akiwa ndani ya gari akizungumza na Dk Bashiru, tofauti na kilichotokea kwa Membe alipohojiwa Dodoma.

Vigogo hao waliokitumikia chama hicho kwa nyakati tofauti, wanakabiliwa na adhabu mbili kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la mwaka 2017, ikiwa watapatikana na hatia.

Katika kanuni hizo kifungu cha 5(2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama au katika uongozi.

Hata hivyo, kipengele cha kuwavua uongozi hakiwagusi kwani kwa viongozi hao hawa wadhifa wowote kwa sasa. Makamba alikuwa katibu mkuu kuanzia mwaka 2007 hadi 2011 na Kinana alishika wadhifa huo kuanzia mwaka 2012 hadi 2018 alipomwachia Dk Bashiru.

Bila shaka CCM itakuwa na wakati mgumu kuamua adhabu hizo hasa ile ya kuwatimua katika chama hasa wakati huu amnapo chama kinaelekea katika uchaguzi mkuu na pia kutokana na vigogo hao kila mmoja kuwa na nguvu ya kisiasa.

Kinana ndiye aliendesha kampeni ya kuirejesha CCM kwenye mstari wakati wa uongozi wake wake baada ya kuzunguka nchi nzima kusikiliza na kutatua kero za wananchi na wanachama, akiwa mkali kwa watendaji wa Serikali waliokuwa wazembe wakiwamo mawaziri aliowaita mizigo na baadaye akaongoza kampeni ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uliomwingiza madarakani Rais John Magufuli.

Membe, mwanadiplomasia mbobezi alikuwa mmoja wa wanachama 38 wa CCM waliojitokeza kuwania urais ndani ya chama hicho mwaka 2015, ambapo Rais Magufuli ndio alipitishwa.

Makamba aliyetumika katika mikutano kadhaa ya kampeni mwaka 2015, ujuzi na ubobezi wake kwenye siasa unaweza kuwafanya pia CCM kuangalia jinsi ya kumaliza suala hilo kwa njia nyingine, hasa ikizingatiwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi na CCM haingetaka kuingia kwenye uchaguzi ikiwa na mgogoro.

Wakati suala la Kinana, Makamba na Membe limefikishwa hatua hiyo, makada wenzao ambao sauti zao zilisikika katika mkanda huo ni Nape Nnauye, mbunge wa Mtama, William Ngeleja (Sengerema) na January Makamba (Bumbuli) ambao kwa nyakati tofauti walimuomba radhi Rais John Magufuli na akawasamehe.

Hii si mara ya kwanza ya Membe kufika mbele ya kamati hiyo. Mara ya kwanza ilikuwa Februari 10 mwaka 2014 akiwa na wenzake William Ngeleja (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini) na Januari Makamba (akiwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).

Wengine walioitwa ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye waliowahi kuwa mawaziri wakuu na Steven Wasira, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wakikabiliwa na tuhuma ya kufanya kampeni kabla ya wakati na baada ya kuhojiwa wakawekwa kitanzini kwa miezi 12 na kuwa chini ya uangalizi.

Katika kipindi hicho, hawakuruhusiwa kujihusisha na uvunjifu wa amani wala kugombea nafasi yoyote ile na ikiwa ikatokea hivyo tena kwa vigogo hao kipindi hiki, inaweza kuwa pigo kwa Membe kama atakuwa na nia ya kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.

Maandalizi ya Ilani 2020/2030

Katika mkutano huo na waandishi, Polepole alisema pamoja na mambo mengine kikao cha Kamati Kuu kilipokea taarifa za maandalizi ya mwelekeo wa sera za CCM kwa mwaka 2020 – 2030 na Ilani ya CCM ya 2020-2025 katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

“Kamati kuu imepokea taarifa ya maendeleo ya uandishi wa waraka huu muhimu wa kisera na kujiridhisha na kazi nzuri ambayo imekwisha kufanyika mpaka ngazi ya rasimu.”

“Kamati kuu pia imepitia zoezi la uandishi wa Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na kuagiza maoni ya wadau mbalimbali kujumuishwa na kuzingatia ratiba ya kukamilisha uandishi wake ili vikao vya chama vifanye uamuzi na kupitisha,” alisema Polepole.

Pia, alisema kamati kuu ilipokea maombi ya kujiunga na uanachama wa CCM kutoka kwa waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye Jumatatu iliyopita alitangaza kurejea katika chama hicho baada ya kukihama Agosti 22 mwaka 2015 na kujiunga na Chadema.

CCM yawapokea madiwani

Katika mkutano huo na waandishi, ulihudhuriwa pia na Dk Bashiru ambaye baada ya Polepole kumaliza kuzungumza aliwapokea madiwani watano wa ACT- Wazalendo kutoka Kigoma Ujiji katika jimbo linaloongozwa na Zitto Kabwe.

Madiwani hao na kata zao katika mabano ni; Khamis Rashid Khamis (Gungu), Ismail Hussein (Kagera), Hamduni Nassor (Kasingirima), Mussa Ngogolwa (Kipampa) na Fuad Nassor (Kasimbu).

Madiwani hao wamesema wameamua kuchukua uamuzi huo ili kuunga mkono juhudi za utendaji kazi unaofanywa na Rais Magufuli.

Kufuatia uamuzi huo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma, ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema, “sisi msimamo wetu, watu wanapotoka ACT-Wazalendo kwenda vyama vingine tunawatakia kila la kheri kwani inakuwa ni uamuzi binafsi.”

Ado alisema, “kuna jitihada za muda mrefu za kuwashawishi madiwani wa Kigoma Ujiji kujiunga na CCM na kinachotokea sasa ni matunda ya ushawishi mkubwa ikihusisha ahadi mbalimbali na madiwani hawa kushindwa kuhimili vishawishi hivyo.”

Hata hivyo, Ado alisema, “bado tunaongoza Halmashauri na tutaendelea kuiongoza tukiwa na meya na naibu meya kutoka ACT-Wazalendo na bado hatutayumba kwenye uchaguzi mkuu, kwani madiwani hao hawatoi taswira ya wananchi wa Kigoma ambao bado wanatuamini.”