Kisa Simba, Kaze abadili gia Yanga

Muktasari:

Kocha Kaze aliyesainishwa mkataba wa miaka miwili katikati ya wiki hii kuchukua nafasi ya Zlatko Krmpotic aliyetimuliwa mapema mwezi huu, licha ya kuiongoza timu hiyo kucheza mechi nane, zikiwamo tano za Ligi Kuu Bara na tatu za kirafiki, tayari ameanza mambo ndani ya timu hiyo.

MASHABIKI wanasubiri kwa hamu kuinoa Yanga mpya chini ya Kocha Mkuu mpya, Cedric Kaze, lakini unaambiwa kocha huyo kutoka Burundi baada ya kuchungulia ratiba ya timu yake na kubaini ana mechi nne tu kabla ya kuvaana na watani zao, Simba na fasta akafanya jambo moja fasta.

Kocha Kaze aliyesainishwa mkataba wa miaka miwili katikati ya wiki hii kuchukua nafasi ya Zlatko Krmpotic aliyetimuliwa mapema mwezi huu, licha ya kuiongoza timu hiyo kucheza mechi nane, zikiwamo tano za Ligi Kuu Bara na tatu za kirafiki, tayari ameanza mambo ndani ya timu hiyo.

Inaelezwa kutokana na kubaini ugumu wa ratiba kwa timu yake, ameamua kuzuia wachezaji wake kutoka kambini na badala yake akataka kujichimbia hapo mpaka baada ya mechi hiyo ya watani itakayopigwa Novemba 7 baada ya kuahirishwa kutoka jana Oktoba 18.

Habari kutoka ndani ya Yanga na kuthibitishwa na Ofisa Habari wao, Hassan Bumbuli ni kwamba Kocha Kaze amekataa wachezaji kupiga mazoezi nje ya kambi yao iliyopo Kigamboni, pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.

Inaelezwa Kaze aliwaomba viongozi wa Yanga wasivunje kambi ambayo awali ilikuwa wachezaji wakipiga mazoezi nje ya kambi hiyo, akilenga kuwapiga vijana wake kwa mechi yao ya Alhamisi dhidi ya Polisi Tanzania, lakini pia kwa mechi nyingine ikiwamo ya Simba.

Yanga iliingia kambini tangu Oktoba 12 huku ikiwa haina mchezo wowote ule wa Ligi Kuu, lengo kubwa lilikuwa kocha Kaze akija awakute wachezaji wakiwa katika hali nzuri.

Mwanaspoti lilipenyezewa na mmoja wa watu wa ndani Yanga kwamba kocha huyo aliwaambia mabosi wa Yanga baada ya mchezo wa Alhamisi kikosi chake kisitoke kambini bali kiendelee kuwekeza nguvu zake katika mechi zao zijazo zikiwamo mitatu ya ugenini dhidi ya KMC, Biashara United na Gwambina.

“Mwalimu aliwaomba viongozi baada ya mchezo wa Alhamis timu isitoke kambini kwani kuna mechi mfululizo, uongozi ulikubaliana nae kwahiyo kila kitu kipo safi kwa upande wake,” chanzo hicho kilisema, huku Meneja wa timu, Hafidh Saleh alipoulizwa juu ya jambo hilo alisema yeye hana kauli yoyote bali wanaotakiwa kufanya hivyo ni viongozi wa juu.

“Mimi ndugu yangu naambiwa tu leo kaeni kambini na kesho tokeni kambini, wanaotakiwa kuzungumzia hayo ni viongozi wa juu au wasiliana na Bumbuli ambaye anapewa mambo yote.”

Bumbuli alipotafutwa alikiri ni kweli timu haitovunja kambi baada ya mchezo wao na Polisi Tanzania kwani wana mechi mfululizo.

“Baada ya mechi na Polisi Tanzania sisi kesho yake (Oktoba 23) tutasafiri kwenda Mwanza kucheza mechi na KMC na baada ya hapo tukirudi tutakuwa na maandalizi ya mechi dhidi ya Simba, hivyo hapo kambi haitovunjwa.”

Kaze mwenye umri wa miaka 40 ameanza kazi ya kuwanoa vijana wake kwenye mazoezi, huku morali ya wachezaji ikielezwa ipo juu, kutokana na mbinu ambazo Mrundi huyo amekuwa akiwalisha akishirikiana na wasaidizi wake.