Latra yataka wenye mabasi kuomba leseni kuokoa adha ya usafiri Dar

Waendesha Bodaboda wakisubiri abiria katika Kituo cha Stesheni jijini Dar es Salaam jana. Huduma ya usafiri wa bodaboda kuchukua abiria katikati ya jiji imerudi tena kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makondo kuruhusu waingie katika kipi hiki ambacho daladala zinapakia abilia kwa kukalisha kwenye viti tu kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, hivyo kusababisha abiria wengi kupata shida ya kupata usafiri kwa wakati. Picha na Salim Shao

Dar es Salaam. Mamlala ya Usafiri wa Ardhini (Latra) imewaalika watu binafsi au taasisi zenye mabasi ambayo hayajapangiwa njia, kuomba leseni za muda mfupi ili kutoa huduma za usafiri maeneo ya mijini.

mwaliko huo umetolewa juzi, siku ambayo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliagiza Latra kukaa na Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam(Latra) ili kubadilisha njia za mabasi zitakazorahisisha hali ya usafiri jijini humo.

Hatua hiyo ya Makonda ilikuja baada ya Machi 31, daladala za mkoa wake kujikuta katika wakati mgumu katika kutekeleza agizo la kuchukua abiria kulingana na idadi ya viti.

Lengo la utaratibu huo maarufu kama level seat, ulioagizwa na Latra ni kuwaepusha na abiria na maambuziki ya virusi ya corona.

Hata hivyo, utaratibu huo bado unasababisha baadhi ya abiria kukosa usafiri kwa wakati na baadhi yao kulazimisha kuchuchumaa au kuketi chini kuwakwepa askari wanaokagua.

Mbali na agizo hilo la Latra Makonda aliondoa zuio la bodaboda na bajaji kuingia katikakati jiji la Dar es Salaam ili kupunguza kero ya usafiri uliotokana na ‘level seat’.

Latra ilitoa mwaliko huo katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kuthibitishwa na mkurugenzi wake wa usafiri na udhibiti wa barabara, Johansen Kahatano.

Taarifa hiyo, Latra iliwaomba wadau wa usafiri wa umma “kufika katika ofisi ya Latra iliyopo karibu wakiwa na kadi ya gari.”

“Vigezo na masharti ya usafiri wa abiria mijini vinazingatiwa,” iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Bodaboda kicheko, kilio

Katika hatua nyingine, madereva wa wa pikipiki maarufu kama bodaboda wameupokea kwa mikono miwili uamuzi wa kuruhusiwa kuingia katika jiji lakini wakisema bado wanakabiliana na changamoto ya kukamatwa na mamlaka husika.

Walisema hivi sasa baadhi ya abiria wamekuwa wagumu kuvaa kofia ngumu ‘helmet’ kutokana na corona, jambo linalowapa wakati mgumu na kujikuta wakikamatwa.

‘Tunamshukuru sana Makonda kwa uamuzi huu, lakini sasa tangu kuingia kwa corona abiria wamekuwa wagumu kuvaa helmet. Huku nje ya mji ni rahisi na ni nadra kukamatwa, sasa huku mjini abiria asipovaa kofia chombo kinakamatwa.

“Ukianza tu kumpa abiria kofia ni ugomvi, anakujibu sasa hivi kuna magonjwa mengi na hii corona hapana. Kwa vile tuna shida tunaamua kuwabeba ingawa siyo salama,” alisema Samir Ameir

‘Msamaha’ kodi ya nyumba

Miongoni mwa mambo aliyoeleza Makonda ni kuwataka wenye nyumba kuwapunguzia kodi wapangaji katika kipindi hiki, jambo ambali baadhi ya watu wamesema ni jema, lakini mchakato wake ni mgumu usiposimamiwa.

Katika ziara yake juzi, Makonda akiwa Makumbusho aliwaomba wamiliki wa majengo, nyumba na vibanda vya biashara kuwapunguzia kodi ya asilimia 50 wapangaji wao kwa kuwa hali ya kiuchumi si nzuri kutokana uwepo wa ugonjwa wa corona.

Katika maelezo yake, alisema baadhi ya biashara haziendi vizuri, kuna watu wamepanga nyumba, ofisi na ‘apartments’ na kwamba amejaribu kuongea na baadhi ya wamiliki wamekubali.

Baadhi ya wakazi ambao ni wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali ikiwamo ushushaji wa mizigo walimpongeza Makonda.

Hamis Hassan alimwomba Makonda kuwaagiza wenyeviti wa mitaa na wajumbe kukaa na wenye nyumba kujadili mchakato huo ili ufanikiwe.

“Huku chini ndiko kwenye matatizo, Makonda ana nia nzuri ya kuwasaidia wananchi, lakini hawa watu sio wote watakubali. Lakini viongozi wetu hawa wakiwaelimisha watakubali tu.

Uhamasishaji sokoni

Wakati huohuo, kumekuwa na uhamasishaji wa wafanyabiashara katika masoko dhidi ya ugonjwa huo.

Mwamtum Mgonja, mdau maendeleo wilayani Ubungo, alifika katika soko la ndizi Mabibo kwa ajili ya kuwahamasisha wafanyabiashara namna ya kujikinga na dhidi ya corona.

“Ni lazima tujikinge huu ugonjwa unaua, tuache uzembe ndugu zangu. Nitajitahidi kuwaletea vifaa mbalimbali vya kujikinga dhidi ya corona,” alisema.

Katibu wa soko hilo, Khalid Hassan aliungana na Mwamtumu akiwataka wafanyabiasha ra wenzake kuchukua tahadhari huku akimshukuru mdau huyo kwa ahadi za vifaa pamoja na ndoo za kunawia mikono.

Katika vivuko wa Kigamboni, meneja wa vivuko hivyo, Samwel Chibwana alisema “tumeweka vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali, tumepulizia dawa kwenye eneo la kusubiria abiria. Pia tumeweka maji katika matenki ili abiria wanawe kabla ya kuingia ndani.”