Lissu alia rafu, NEC wamjibu

Muktasari:

Malalamiko hayo ya Lissu yamekuja wakati tayari Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe wakitoa madai ya kuongezwa kwa wapiga kura na vituo hewa vya kupigia kura.

Lindi/Dar. Mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu amelia hujuma akidai wamebaini upungufu kwenye daftari la wapigakura kwa kuwa lina wapigakura hewa, wasio na sifa sambamba na vituo hewa.

Malalamiko hayo ya Lissu yamekuja wakati tayari Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe wakitoa madai ya kuongezwa kwa wapiga kura na vituo hewa vya kupigia kura.

Hata hivyo,Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Mahera amekanusha madai hayo akisema kumezuka kikundi cha viongozi wa siasa wa ngazi za juu, waliojipanga kuharibu taswira ya uchaguzi, ikiwa pamoja na kutoa taarifa na vielelezo vya uongo na uzushi kwa lengo la kuzua taharuki kwa wadau wa uchaguzi na wananchi.

Lakini akizungumza na vyombo vya habari jana mkoani Lindi, Lissu aliendelea kusisitiza kuwapo kwa hujuma ikiwa pamoja na wapiga kura hewa.

“Tumebaini kuna mamilioni ya wapigakura hewa, wapigakura wasio na sifa pamoja na vituo hewa. Wameacha kushindana na sisi kwenye majukwaa, sasa wanataka kuvuruga uchaguzi,” alidai Lissu.

Mgombea huyo alidai wana taarifa juu ya mpango wa kubadilisha matokeo kwa kutangaza watu ambao hawajashinda, kutangaza matokeo kwa nguvu na kutumia mabavu kutangaza ambao hawajashinda uchaguzi.

Lissu ametoa madau hayo ikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Watanzani kwenda kushirik haki yao ya kikatiba ya kupiga kura katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 28.

Majibu ya NEC

Hata hivyo, katika taarifa ya NEC iliyotolewa kwa vyombo vya habari Oktoba 23, Mkurugenzi wa uchaguzi Dk Mahera alisema wamebaini kuwepo wa kundi akidai wamenasa mazungumzo yake ya kukubaliana kufanya propaganda.

“Mojawapo ya mipango ya kuzusha ni wimbi linaloendelea la kudai uwepo wa vituo hewa,” alisema Dk Mahera huku akitoa mfano wa jimbo la Misungwi mkoani Mwanza. “Kama walivyojipanga hali ya kudai vituo hewa inaendelea kujitokeza maeneo mbalimbali,” aliongeza kusema.

Lissu azungumzia mikutano kutofanyika

Siku moja baada ya wananchi kupigwa mabomu ya machozi katika mikutano yake, Lissu amesema kitendo hicho ni njama za kuvuruga mikutano yake ya kampeni ili asishinde uchaguzi mkuu wa Jumatano ijayo.

Alisema jana alipata taarifa kwamba wananchi walipigwa mabomu katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji, hivyo, mikutano iliyopangwa kufanyika katika maeneo hayo ikavurugika.

“Tulianza safari tukapigiwa simu tukajulishwa kwamba polisi na wanajeshi wamepiga watu mabomu Mkuranga, Kibiti na Rufiji na kuwatawanya na kuwanyang’anya vifaa vyao,” alisema Lissu.

Mgombea huyo alisema walikwenda Somanga kufanya mkutano wa kampeni, baada ya muda mfupi akatokea mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ofisa mtendaji wa kata, akawaamuru polisi kupiga mabomu na kuwatawanya wananchi.

Baada ya mkutano huo kuvurugwa, Lissu alisema walikwenda Kilwa Kivinje ambako hawakutua kabisa kutokana na polisi kupiga mabomu wakiwatawanya wananchi waliokuwa wakimsubiri kwenye mkutano huo.

“Vitendo ambavyo tumeanza kuviona vya matumizi ya vyombo vya dola na taasisi za Serikali vinalenga kuhakikisha kwamba kampeni zetu hazifanyiki,” alisema Lissu.

Mgombea huyo alibainisha kwamba yeye ndiye mgombea pekee ambaye amefanya mikutano mingi ya kampeni na tafiti za ndani ya chama chake zinaonyesha kwamba atapata ushindi wa kati ya asilimia 65 hadi 75.

Alipongeza Jeshi la Polisi

Mgombea huyo alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri inayofanya katika kuimarisha usalama kwenye mikutano yake huku akibainisha kwamba jeshi hilo katika mkoa wa Kagera lilifanya vizuri zaidi wakati mkoa wa Dodoma ukifanya vibaya.