HOJA ZA KARUGENDO: Lowassa ni kigeugeu, mnafiki au mzalendo?

Thursday February 20 2020

 

Kuhama vyama vya siasa na hasa kuhama upinzani kwenda CCM, kumezua maswali mengi na hasa inapotokea wale waliokihama chama cha CCM wakati wa uchaguzi Mkuu na sasa wamerudi nyumbani kwao, watu wanakuwa na maswali mengi. Je, ni vigeugeu wa siasa, wanafiki au ndiyo wazalendo wa Taifa letu?

Bahati mbaya mtu mwenyewe ninayeandika makala hii sina chama. Leo ninaweza kuwa CCM, nikishawishiwa na sera zao na utendaji kazi wao. Lakini kesho naweza kuwa Upinzani, nikishawishiwa na sera zao na utendaji kazi wao. Vyama vyote ni vya Watanzania, hivyo sote tuna haki kujiunga na chama chochote na wakati wowote.

Kati ya watu waliohama CCM na kuingia upinzani wakati wa uchaguzi mkuu na kurejea CCM baada ya uchaguzi ni pamoja na Edward Lowassa! Nimjadili huyu kwanza na baadaye nitamgeukia Frederick Sumaye. Wote hawa ninawafahamu vizuri.

Lowassa ni rafiki yangu na ndugu yangu wa karibu na tunasali. Ninampenda na hakuna wa kunitenganisha naye. Ni mtu mwema anayependa watu. Ana marafiki wengi na wa miaka mingi. Ni mtu wa msaada, ukimwendea na shida lazima atakusaidia. Kwenye nafasi zote za uongozi alizopitia alihakikisha anawasaidia rafiki zake na watoto wao wote walipata kazi.

Ni mcha Mungu anapenda kusali na analipenda Kanisa lake na viongozi wake. Yuko mstari wa mbele kusaidia madhehebu mengine hata na misikiti. Akiingia kanisani lazima atoe sadaka kubwa. Viongozi wengi wa dini wanampenda kwa moyo wake huo wa kupenda kusaidia.

Wanaosema anapenda madaraka wanamsingizia, bali anapenda kuwatumikia na kuzungukwa na watu na kusikilizwa. Ana tabia kama ya machifu wa zamani.

Advertisement

Tena badala ya kusema anapenda ana uchu wa madaraka, ni bora waseme huyu ni chifu. Alikuwa hivyo maisha yake yote, waliosoma naye wanamkumbuka kwa tabia hiyo ya kutaka aonekane ndiye kiongozi wao au anayewaunganisha.

Kwa tabia hiyo, alijenga mtandao mkubwa ndani ya Sipendi kuingia kwa undani juu ya mtandao, lakini sote tunafahamu mtandao huu ulikuwa na faida chanya na hasi. Na kwa wastani, hasi ni kubwa kuliko chanya.

kwa sababu ulijenga makundi ndani ya CCM.

Mtu anayejenga makundi kwenye jamii hawezi kuwa kiongozi bora zaidi ya kuwa mfalme. Sote tunakumbuka wafalme walikuwa watawala, hawakuwa viongozi. Dunia ya leo inatafuta viongozi si watawala.

Nikisema huyu asingeweza kuwa Rais mzuri au kama angekuwa rais kupitia upinzani, angerudi CCM kama alivyofanya si kwamba ninamchukia hapana.

Ninasema hivyo kwa sababu ninamfahamu. Ninajua kwamba “tabia ya uchifu” isingemruhusu awe Rais mzuri. Urais si nafasi ya kuwapenda rafiki na ndugu na haitoshi kuwa mtu mwema mwenye upendo na mcha Mungu. Kuna karama nyingi zinahitajika. Karama ambazo si kila mtu anazo. Ni bahati mbaya hapa nchini kila mtu anafikiri anaweza kuwa Rais. Kila mtu anafikiri anaweza kuwa kiongozi, si kweli, uongozi ni karama si watu wote wanayo.

Ndugu zangu wanaohama vyama si vigeugeu, wanafiki au wazalendo zaidi, bali hawajajitambua, bado hawafahamu karama zao.

Nia ya kuhama vyama ni kutafuta uongozi lakini kumbe wao wanatafuta utawala. Wanaweza kubahatisha kuupata uongozi lakini kwa vile akilini mwao kuna utawala, hawawezi kwenda mbali. Na pale wanaposhindwa kupata wanachokitaka wanatimka na wataendelea kutimka. Mtu asiyejitambua ataendelea kutimuka maisha yake yote.

Advertisement