Maalim Seif amvaa Membe

Muktasari:

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Maalim Seif ambaye anagombea urais Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho wameshatangaza msimamo wa kumuunga mkono Lissu.

Dar es Salaam. Wakati Uongozi wa ACT Wazalendo, ukisema uamuzi wa Bernard Membe kuendelea na kampeni za urais wakati chama hicho kinamuunga mkono Tundu Lissu unawachanganya wananchi, wachambuzi wameeleza kummtilia shaka mwanadiplomasia huyo wengine wakisema ni haki yake.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi Dar es Salaam, Membe aliyesitisha kampeni zake kwa mwezi mmoja na nusu tangu alipozizindua Septemba 2 mkoani Lindi, alisema bado ni mgombea halali wa chama hicho na atapiga kampeni kwa wiki moja iliyobaki.

Lakini jana Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad alisema “chama chetu katika mkutano mkuu tuliamua kuwa tunataka mabadiliko kama hatutashirikiana hatutaweza kuiondoa CCM,” alisema Maalim Seif.

Alisema na msimamo huo walimwambia Membe ambaye juzi katika mkutano wake na wanahabari alieleza kutokuwa na imani kama wapinzani wanaweza kushirikiana na kuing’oa CCM, bali mpasuko ndani ya chama tawala ndio unaweza kuwapa wapinzani ushindi.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Maalim Seif ambaye anagombea urais Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho wameshatangaza msimamo wa kumuunga mkono Lissu.

Hatua ya Membe kuibuka katika kipindi cha lala salama kimeelezwa na Profesa wa sayansi ya siasa wa chuo kikuu cha Ruaha (Ruco), Gaudence Mpangala kuwa ni cha hatari kwa kambi nzima ya upinzani.

“Kitendo cha Membe kujitokeza kipindi hiki kinaleta utata, kinaweza kuwachanganya wapiga kura na kitaathiri mafanikio ya wapinzani kwa ujumla,” alisema.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu uamuzi wa juzi wa Membe kujitangaza kwamba bado ni mgombea wa chama hicho, Maalim Seif alisema suala la kumuunga mkono Lissu lilijadiliwa kwenye vikao na Membe alikuwepo.

“Alipokuja Membe tulimwambia kabisa uamuzi ya mkutano mkuu ni kwamba tushirikiane na vyama vingine akakubali. Sasa leo anasema anaendelea na kampeni, mmeona akifanya kampeni?” alihoji Maalim Seif.

Akieleza sababu ya kumuunga mkono Lissu, Maalim Seif alisema ni baada ya kuona mgombea wao hafanyi kampeni.

“Tulikaa wiki moja na nusu tukaona kampeni zikisuasua, tukaitana kamati ya uongozi na Membe alikuwepo. Tukasema mgombea wetu haonekani, yaani hata mzee wa ubwabwa anaonekana,” alisema.

Aliendelea kusema katika kikao hicho Membe alitoa muda maalumu akisema ikishindikana waunge mkono mgombea mwingine.

“Sasa amesema ataanza kampeni, haya tuone kampeni zake. Nia yake ni kuwachanganya Watanzania.

“Mgombea anayeelekea kushinda ni Lissu, na jana nilikuwa naye Moshi kwenye mkutano mkubwa,” alisisitiza Maalim Seif.

Aliendelea kusema kuwa kauli zilizotolewa na Kiongozi wa chama Zitto Kabwe na yeye, siyo kauli zao binafsi, bali za chama.

Akizungumzia suala hilo mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza alisema kitendo cha Membe kupotea katika kampeni kinadhihirisha jinsia alivyo mchanga katika siasa za upinzani.

“Kwenye siasa za upinzani, Membe bado ni mchanga, anajua zile siasa za kuandaliwa za chama tawala, amejikuta hana uzoefu wa kupambana upinzani.

“Unaweza kusema CCM inamtumia, lakini ukweli ni kwamba hawawezi kumtumia kwa sababu hana masilahi kwao,” alisema Kaiza.