Magufuli: CCM tusijisahau, vyama vilivyoongoza kwa mazoea vilipoteza imani ya wananchi

Thursday December 12 2019

 

By Peter Saramba, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Tanzania ni kati ya nchi chache barani Afrika ambazo Serikali zake imeundwa na  vyama vya ukombozi  na vilivyopigania uhuru.

Nchini Tanzania, wanachama wa chama tawala (CCM) mara kadhaa wamenukuliwa wakisema chama hicho tawala kitaendelea kushika hatamu ya uongozi zaidi ya miaka 100 ijayo kwa kuwa ni chama cha ukombozi, kimepigania uhuru wa nchi.

Lakini leo Alhamisi Desemba 12, 2019 Rais  wa Tanzania, John Magufuli amewaonya viongozi na wanachama wa CCM kuwa chama hicho  kinaweza kupoteza uongozi wa Dola ikiwa kitajisahau na kuongoza kwa mazoea bila kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi.

Mwenyekiti huyo wa CCM ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa majadiliano wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) jijini Mwanza.

 Magufuli amesema kujisahau na kuongoza kwa mazoea ni miongoni mwa sababu zilizoviangusha vyama kadhaa viliyopigania ukombozi na Uhuru katika mataifa kadhaa barani Afrika.

“CCM kushika hatamu ya uongozi kwa miaka 58 ni suala la kujipongeza kwa sababu ni nadra katika nchi nyingi za Afrika. Naamini kila mjumbe aliyepo hapa angependa CCM kuendelea kushika hatamu ya uongozi. Hilo litawezekana endapo tutaendelea kukidhi mahitaji na matarajio ya Watanzania,” amesema Magufuli.

Advertisement

Amewataka viongozi na wana CCM kujenga utamaduni na kujitathmini kama chama kinakidhi mahitaji na matarajio ya wananchi, kujisahihisha na kubadilika.

“Tuepuke uongozi wa mazoea,  na kusema kweli vyama vingi vilivyojisahau na kuongoza Serikali kwa mazoea vilifikia hatua ya kupoteza imani ya wananchi na uhalali wa kisiasa. Ndicho kilichotokea kwa vyama vingi vilivyopigania Uhuru barani Afrika. Ndugu zangu (CCM) tusifikie huko,” amesema Rais Magufuli.

Amewataka wajumbe wa NEC kutumia mkutano wao kutathmini utendaji wa CCM na Serikali kwa kuangalia Taifa lilipotoka, lilipo na mwelekeo wa chama hicho miaka 10 ijayo.

 “Tujadiliane kwa kuangalia mwelekeo wa  masuala mapana ya sera ya CCM kwa miaka 10 ijayo,  kuanzia mwaka 2020 hadi 2030 pamoja na mipango mahususi itakayotekelezwa kupitia ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025,” amesema  Magufuli.

 

Advertisement