Majaliwa apiga marufuku uagizaji sukari Zanzibar

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Juma Hassan Reli kuzuia utoaji wa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje hadi sukari inayozalishwa na kiwanda cha sukari cha Zanzibar kilichopo Mahonda iishe.

Amesema haiwezekani kiwanda hicho kinachozalisha tani 6,000 za sukari kwa mwaka kikakosa wateja wakati mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000 kwa mwaka.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana alipotembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar kilichopo katika eneo la Mahonda wilaya ya Kaskazini ‘A’ mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema ni vizuri wizara ikahahakikisha sukari inayozalishwa na kiwanda hicho inapewa kipaumbele cha kwanza kwa kununuliwa kwa sababu wana uhakika na ubora wake kwa kuwa wameshuhudia uzalishaji wake kuanzia hatua ya awali miwa ikiwa shambani.

Awali, mkurugenzi mkaazi wa kiwanda hicho, Rahim Bhaloo alisema kiwanda chao kinazalisha tani 6,000 kwa mwaka huku kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani zaidi ya 20,000 kwa mwaka ila tatizo ni ukosefu wa soko pamoja na ardhi ya kutosha kulima miwa.

Aliomba Serikali kuzuia utoaji wa vibali vya uagizaji wa sukari kutoka nje hususani kipindi cha uzalishaji ili waweze kuuza sukari yao na itakapoisha ndio vibali hivyo vianze kutolewa.