Majaliwa awapiga ‘stop’ mawaziri kufanya ziara

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu hatua za awali zilizochukuliwa na Serikali kutokana na kuingia kwa ugonjwa wa virusi vya Corona nchini. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka mawaziri wote kusitisha ziara za kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo badala yake waelekeze nguvu kuzuia kuenea kwa virusi vya ugonjwa wa corona nchini.

Majaliwa alitoa maagizo hayo jana jijini Dodoma wakati akizungumza na mawaziri na makatibu wakuu katika kikao kazi chenye lengo la kupanga mikakati ya kukabiliana na corona iliyobainika kuingia nchini Mei 16.

Alisema Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuhakikisha inazuia corona isiweze kusambaa kwa kiasi kikubwa nchini.

“Mawaziri hakikisheni katika kipindi hiki ziara za kwenda kukagua miradi zielekezwe kwa wakurugenzi ikibidi kwa makatibu wakuu, mawaziri mnatakiwa mjikite katika kukinga Taifa na corona,” alisema Majaliwa.

Majaliwa alivishukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona.

Katika kikao hicho, Majaliwa alizitangaza kamati tatu zilizoundwa za kupambana na corona. Kamati hizo ni ya kitaifa ambayo ataiongoza yeye mwenyewe (Majaliwa) na itahusisha baadhi ya mawaziri, makatibu wakuu na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Kamati ya pili ni ya makatibu wakuu kutoka sekta husika na itaongozwa na katibu mkuu kiongozi na kamati ya tatu ni ya kikosi kazi cha Taifa ambacho kitaongozwa na katibu mkuu wa wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto huku wajumbe wake wakiwa ni wataalamu akiwamo katibu mkuu wa wizara ya afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema katika kipindi cha saa 24 jumla ya watu 292,142 duniani walibainika kuwa na virusi vya corona kati yao watu 12,784 walifariki.

Pia, katika Bara la Afrika watu 736 walibainika kuwa na virusi vya corona na kati yake watu 20 walifariki katika kipindi cha saa 24.

Akizungumzia kwa upande wa Tanzania, Waziri Ummy alisema watu 12 walibainika kuwa na virusi vya corona tangu mgonjwa wa kwanza alivyogundulika nchini Machi 16 na kwamba wagonjwa wote hali zao ni nzuri na mmoja amepimwa zaidi ya mara mbili na kubainika kuwa hana virusi vya corona.