Makaburi ajali ya Mv Bukoba hatarini kuharibiwa

Mwanza. Makaburi ya waliofariki dunia katika ajali ya Mv Bukoba yaliyoko Igoma jijini Mwanza yako hatarini kufukuliwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha baada ya uzio uliojengwa kuyazunguka kuangushwa na maji.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi juzi katika eneo hilo lenye makaburi zaidi ya 400 umegundua kuwa baadhi ya makaburi tayari yameanza kudidimia kutokana na wingi wa maji ya mvua yanayoingia eneo hilo.

Ajali ya Mv Bukoba ilitokea Mei 21, 1996 na kusababisha vifo zaidi ya watu 1,000 ambao baadhi yao walizikwa kwenye makaburi ya pamoja eneo la Igoma Barabara Kuu ya Mwanza – Musoma, nje kidogo ya jiji la Mwanza.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa majirani wanaoishi eneo hilo, Deus Ndaki aliiomba Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la Mwanza kujenga upya uzio ulioanguka kulinda hadhi ya Watanzania waliopumzishwa kwenye makaburi hayo.

“Hii ni sehemu ya kumbukumbu muhimu kitaifa. Ni lazima patunzwe kwa heshima ya waliolala hapo,” alisema Ndaki.

Mkazi mwingine, Emmanauel Machumu alisema ni jambo la aibu ukuta wa makaburi hayo kuanguka na kuachwa muda mrefu bila kurekebishwa upya.

“Kwenye hili, viongozi wa Serikali Jiji na Mkoa wa Mwanza hawana utetezi kwa sababu wanapita hapa kila siku na kuona hali halisi ilivyo kwenye makaburi haya,” alisema Machumu akiwatupia lawama viongozi kwa kuyatelekeza makaburi hayo.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomonio Kibamba alisema ofisi yake tayari imemwagiza mhandisi wa jiji kufanya tathmini kujua gharama za kujenga upya ukuta huo.

“Tunayathamini na kuyaheshimu makaburi ya waliofariki dunia katika ajali ya Mv Bukoba kwa sababu ni eneo la kumbukumbu la kitaifa. Tutajenga upya ukuta uliodondoka na tayari tathmini inafanyika,” alisema Kibamba.