OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Makomandoo wa Israel waondoka Entebbe-10

Thursday September 12 2019

 

Kwa ujumla mapambano katika uwanja wa ndege wa Entebbe yaliyoanza saa 5:03 usiku wa Julai 3, 1976 yalimalizika saa 6:30 Jumapili ya Julai 4, 1976—hizo zikiwa ni dakika 87 za mapambano makali kati ya Waisraeli dhidi ya magaidi wakisaidiwa na majeshi ya Uganda.

Kwa muda wote huo wa mapambano hayo Waziri Mkuu wa Israel, Yitzhak Rabin, alikuwa ofisini kwake na mawaziri wengine wakisikiliza kupitia mawasiliano ya redio jinsi mapambano yalivyokuwa yakiendelea Entebbe.

Saa 7:20 usiku wa kuamkia Jumapili ya Julai 4, Waziri wa Uchukuzi wa Israel, Gad Yaakobi, alimpigia simu mwenyekiti wa Kamati ya Familia na Jamaa za Mateka, Profesa Yosef Gross. Katika ukurasa wa 55 wa kitabu chake, Entebbe: The Most Daring Raid of Israel’s Special Forces, mwandishi Simon Dunstan anamnukuu Yaakobi akisema: “(Gross) Hakuamini nilipomwambia kuwa kaka yake na mama mkwe wake walikuwa huru.”

Aliendelea kusimulia, “Hii ilikuwa ni saa chache kabla ya kufanya nami mkutano mwingine Jumapili asubuhi ili kujadili hali iliyokuwa inazidi kuzorota. Alikuwa na hofu kuwa mateka wangeanza kuuawa asubuhi (Julai 4). Dakika kumi baada ya kumwambia kuwa mateka wamekombolewa, alianza kuwapigia simu ndugu na jamaa wa mateka. Tulijua kuwa labda [mateka] wawili waliuawa na wawili au watatu walijeruhiwa, lakini hatukuwa na majina yao. Familia zote zilialikwa kukutana na watu wao (waliokuwa wametekwa) watakapokuwa wanawasili na ndege iliyowabeba. Kuna familia zitafurahia lakini kuna familia angalau mbili zitahuzunika sana baada ya kuona wanaotoka kwenye ndege wakiwa hai si miongoni mwa wanafamilia zao.”

Hopitalini Mulago mjini Kampala ambako Dora Bloch alikuwa amehamishiwa kutokana na hali yake kuwa mbaya, alitembelewa na mwanadiplomasia mwingine wa Uingereza mjini Kampala, Peter Chandley, kuhakikisha kuwa alikuwa salama. Lakini alimkuta amelala.

Wauguzi waliokuwa wakimhudumia walimwambia Balozi Chandley kuwa mgonjwa wao alikuwa anaendelea vizuri na kwamba sasa angeweza kuungana na wenzake baadaye siku hiyo. Hata hivyo, ingawa Balozi Chandley tayari alishajua kilichotokea katika uwanja wa ndege wa Entebbe na kwamba mateka wa Ndege 139 walikuwa wameshaokolewa na wameondolewa Uganda, hakuwaambia wauguzi chochote kuhusu tukio hilo na pia hata wauguzi na madaktari wa hospitali hiyo walionekana kutojua chochote kilichotokea usiku uliopita.

Advertisement

Golda Meir, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Israel kabla ya Yitzhak Rabin na ambaye alikuwa akifuatilia sana habari za utekaji huo, aliamshwa usingizini na mwito wa simu iliyokuwa kando ya kitanda chake.

Kwa mujibu wa kitabu A Political Chronology of the Middle East, Jumatano ya Aprili 10, 1974 ndipo Golda Meir alipojiuzulu uwaziri mkuu wa Israel na ndipo akaja Yitzhak Rabin. Simu hiyo iliita mfululizo kiasi kwamba alilazimika kuamka ili aipokee.

“Bibi Meir,” ilisikika sauti ya Rabin. “Nafikiri ungependa kujua kuwa mateka sasa wako huru na wako njiani kurejea nyumbani … Niwie radhi kwa kukatiza usingizi wako lakini nawiwa kukupasha habari hizi.”

Meir akamjibu, “Unataka nijue? Nakushukuru na hongera sana.” Wakati Golda Meir anapokea simu hiyo ilikuwa ni saa 8:30 usiku.

Wakati wakiondoka Uganda, makomandoo wa Israel waliubeba mwili wa kamanda wa kikosi cha uokozi, Yonathan Netanyahu, na kuupeleka kwenye ndege iliyoondoka na mateka waliookolewa. Wapiganaji wa kikosi chake bado hawakujua kuwa tayari kamanda wao ameshaaga dunia. Waliamini alikuwa amezimia tu.

Kwa upande mwingine, wakati kukiwa na kukurukakara nyingi za uokozi katika uwanja wa Entebbe, hakuna mwokozi hata mmoja aliyejua huzuni kubwa aliyokuwa nayo mtoto wa Dora Bloch aliyeitwa Han Hartuv. Wakati mtoto huyo akiokolewa pamoja na mateka wengine, alikumbuka kuwa mama yake alikuwa amelazwa hospitalini na kwa sababu hiyo huenda hangemwona tena kwa sababu hakuwa na la kufanya kwa wakati huo.

Iliyokuwa ndege ya kwanza kutua mjini Entebbe na kuanza mashambulizi ilikuwa ndiyo ndege ya mwisho kuondoka uwanjani hapo baada ya ndege nyingine zote kuondoka.

Ndege hiyo ilikuwa inarushwa na kiongozi wa marubani wa ndege zote zilizotumika katika operesheni ya Entebbe. Wakati akigeuza ndege yake tayari kwa kupaa angani, ndege za Urusi zilikuwa zikiendelea kulipuka na kuteketea kabisa.

Mkuu wa operesheni ya kuivamia Entebbe, Brigedia Jenerali Dan Shomron, ambaye naye alikuwa wa kwanza kutua Entebbe, pia alikuwa wa mwisho kuondoka baada ya kuwa na uhakika kwamba wote wamekwishaondoka kwenye ardhi ya Uganda. Yeye alikuwa na kile kikosi kilichoharibu mfumo mzima wa radar uwanjani hapo pamoja na kuteketeza ndege za Jeshi la Uganda.

Ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa iliyotekwa na kupeleka mateka mjini Entebbe bado ilikuwa uwanjani hapo. Pamoja na kwamba ndege za Idi Amin ziliteketezwa, ile ya Ufaransa haikuguswa.

Baadaye Shomron alikaririwa akisema “Ikiwa tunaweza kufanya hivyo barani Afrika, tunaweza kuifanya mahali popote.” Alisema uhasama wowote dhidi ya Israel au Myahudi unapaswa kupewa majibu ya mtindo huo. Aliendelea kusisitiza kuwa taifa lolote likionyesha kitendo kama kilichofanywa na Idi Amin litambue kuwa Israel itashambulia.

Idi Amin, ambaye usiku huo alikuwa amerejea kutoka Mauritius na sasa alikuwa amelala mjini Kampala, aliamshwa kitandani saa 8:20 usiku wa kuamkia Jumapili ya Julai 4, 1976. Simu hiyo ilipigwa kutoka Tel Aviv, Israel.

Kwa kuwa simu hiyo ilikuwa kando ya kitanda chake, ilipigwa mfululizo hadi ikamwondoa kabisa usingizini. Wakati simu hiyo ikipigwa, tayari maofisa wa Israel walikuwa wamekaa karibu na redio zao za mawasiliano kusikiliza anachoongea Idi Amin.

Simu hiyo ilipigwa na Baruch Bar-Lev, ambaye alikuwa ni Luteni Kanali mstaafu wa Jeshi la Israel (IDF) na kwa muda fulani alikuwa Uganda na ndiye ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliomsaidia Idi Amin kuiangusha serikali ya Dk Milton Obote Jumatatu ya Januari 25, 1971.

Mwandishi Jef Verschueren katika ukurasa wa 65 na 66 wa kitabu chake, On Speech Act Verbs, aliandika mazungumzo kati ya Idi Amin na Bar-Lev. Kwa mujibu wa kitabu hicho, bila kutambua kuwa mateka wameshakombolewa na idadi kubwa ya ndege zake zimeteketezwa, Idi Amin alipoisikia tu sauti ya Bar-Lev alianza kusema: “Iambie serikali yako ikubaliane na matakwa ya watekaji nyara.”

“I see!” akajibu Bar-Lev kwa utulivu.

“Hili si suala la mazungumzo tena. Ni suala la utekelezaji,” akafoka Idi Amin.

“Kweli? Lakini asante kwa kile ulichofanya,” akasema Bar-Lev.

“Asante! Asante kwa lipi? Akauliza Idi Amin.

Sehemu ya mazungumzo kati Amin na Bar-Lev yalikuwa hivi:

Bar-Lev: Nataka tu nikushukuru kwa ushirikiano uliouoyesha na nataka nikushukuru sana.

Idi Amin: Unaweza kuniambia kuhusu mapendekezo yako?

Bar-Lev: Nimeombwa na rafiki mwenye mawasiliano mazuri na Serikali nikushukuru kwa ushirikiano wako. Sijui amemaanisha nini lakini nadhani unajua.

Idi Amin: Sijui kwa sababu ndiyo kwanza nimerejea kutoka mkutanoni Mauritius.

Bar-Lev: Ahaaa!

Idi Amin: Nimerejea ili kulipatia ufumbuzi tatizo hili kabla ya muda wa mwisho kesho asubuhi.

Bar-Lev: Naelewa vizuri sana bwana mkubwa ... Nakushukuruu kwa ushirikiano. Labda nitakupigia tena simu kesho asubuhi. Ungependa nikupigie tena simu asubuhi kukishapambazuka?

Idi Amin: Ndiyo.

Bar-Lev: Vizuri kabisa. Asante na kwaheri.

Kisha Bar-Lev akaweka mkono wa simu chini. Hata wakati taarifa za redio katika jiji la Paris zikitangaza kuhusu uvamizi wa Entebbe, Idi Amin hakuwa amejua kilichokuwa kimetukia nchini mwake. Mateka walikuwa wameshaondoka na magaidi walikuwa wameshauawa.

Saa chache baadaye, kiasi cha saa 11:00 alfajiri, hali ikabadilika. Sasa Idi Amin akawa ndiye anapiga simu kwenda Israel. Kwa sauti ya mkwaruzo Idi Amin alimuuliza Bar-Lev: “Mmenitenda nini? Kwa nini mmewaua askari wangu? Niliwatunza Waisraeli, niliwatendea vizuri, nikawapa huduma, blanketi, magodoro, nilitarajia kwamba hivi karibuni tutawaachia kwa kubadilishana lakini tazama mmewaua askari wangu.”

Bar-Lev aliripoti baadaye kuwa sauti ya Idi Amin ilikuwa ya taharuki. Hata hivyo Amin hakuwa amejua kwa hakika kilichotokea Entebbe.

Amin: Wamewaua watu wangu.

Bar-Lev: Nani kawaua? Kwani mateka walikuwa na bunduki?

Amin: Si mateka wamewaua. Kuna ndege zimekuja na kuwaua.

Bar-Lev: Ndege? Sijasikia kama kulikuwa na ndege. Umeniamsha usingizini. Niko nyumbani na sijui chochote.

Itaendelea kesho

Advertisement