Mama aeleza gazeti la Mwananchi lilivyomrejesha mwanaye shule

Saturday October 12 2019

By Daniel Makaka, Mwananchi [email protected]

Buchosa. Maria Kimbambise, mkazi wa kijiji cha Nyakasungwa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza amelipongeza gazeti la Mwananchi kwa kuandika habari iliyosaidia mwanaye, Kudra Boniphace kuendelea na masomo.

Kudra alikatisha masomo akiwa kidato cha tano baada ya kuolewa na mwalimu wake.

Gazeti la Mwananchi lilifuatilia sakata hilo kuanzia Agosti 20, 2018 na mwanafunzi huyo kukutwa akiishi na mwalimu wake.

Habari hiyo iliwaibua viongozi wa wilaya ya Sengerema waliomsaka mwalimu na mwanafunzi huyo, kumrejesha shuleni ambako anaendelea na masomo katika shule ya Sekondari Nyehunge .

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Oktoba 12, 2019 Maria amesema, “kwa Sasa natamani mwanangu awe mwalimu ili aje kusaidia wadogo zake watano ambao aliachiwa na baba yake baada ya kufariki dunia.”

"Vyombo vya habari ni muhimu  kwa kutatua matatizo ya watu, leo bila Mwananchi mwanangu asingekuwa darasani,” amesema Maria.

Advertisement

Mwanafunzi huyo alihitimu kidato cha nne mwaka 2016  na kuolewa na mwalimu hadi 2019 aliporejeshwa shule.

Mkuu wa shule hiyo, Kafumu Boniphace amesema kwa sasa mwanafunzi huyo amekuwa tishio darasani kwa kufanya vema katika masomo.

“Alifika shule Januari 2019 na mtihani wa muhula wa kwanza alishika nafasi ya 37 kati ya wanafunzi 50 licha ya kuchelewa kuripoti shule,” amesema  Kafumu, akisisitiza kuwa wameweka nguvu kumsaidia ili afaulu mitihani wa mwisho.

Amina Mussa, mkazi wa wilaya hiyo amesema vyombo vya habari vipo mstari wa mbele kutatua matatizo ya wananchi, huku akilipongeza gazeti la Mwananchi.

 

Advertisement