Mangula: Tunzeni siri za vikao

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula akizungumza katika kongamano la Jumuiya ya Wazazi la chama hicho lililofanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Kati ya mambo ambayo Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula alisisitiza wakati wa Kongamano la Jumuiya ya Wazazi ya CCM ni kwa viongozi kutunza siri za vikao.

Alionya kutokuwepo usiri kwenye kipindi cha kujadili majina ya wagombea kunaweza kuleta mgongano.

Jumuiya ya Wazazi iliandaa kongamano maalum kwa ajili ya kupongeza utendaji kazi wa Rais John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, mjini Dodoma, wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Dk Edmund Mndolwa anasema kongamano hilo lilifikisha idadi ya 200 yaliyofanyika ndani ya jumuiya hiyo kwa lengo la kuendelea kuimarisha CCM.

Kongamano hilo liliandaliwa katika kipindi ambacho taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani 2020.

Taifa litakuwa na uchaguzi mkuu mwakani kwa ajili ya kuchagua Rais, wabunge na madiwani.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mangula alisema “naombeni kutunza siri za vikao hasa tunapojadili majina ya watu, mtaleta mgongano.”

“Kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu kuficha siri za kinachojadiliwa kwa faragha ni muhimu ingawa kunahitajika kifua maana inawezekana ukasema utajitahidi kutunza siri lakini ukajikuta unatoa bila kujua, tunzeni siri,” anasisitiza Mangula na kuongeza;

“Mnaweza kutoka kwenye kikao mkaingia kwenye gari na kuanza kujadili halafu dereva anasikia siri za vikao muhimu sana, mnatakiwa kuwa na vifua hasa tunapojadili majina ya watu ili msilete mgongano,” anaonya Mangula.

Mangula pia ameonya watu walioanza kujipitisha pitisha kupiga kampeni kwa ajili ya kujipanga na uchaguzi mkuu mwakani.

Anatishia kuwafungulia mafaili watakaokiuka kanuni na katiba ya chama hicho kwa kuanza kampeni kabla ya wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mangula anasema muda wa kuanza kampeni bado haujafika hivyo wabunge na madiwani walio madarakani wakiwakilisha chama hicho wanapaswa kuachwa wamalize muda wao wa miaka mitano.

“Tukigundua tu tunafungua faili na siku moja mtaitwa, muda wa kampeni bado hata mchezo wa ngumi una sheria zake mnangoja refa aseme, refa wa CCM bado hajapiga filimbi kuanza mchezo kiherehere cha nini?” anahoji Mangula.

Anasema viongozi wa chama hicho hawapaswi kuwa mashabiki wa watu wanaotaka kuwania ubunge au udiwani mwakani.

Wakati wa kongamano hilo, Katibu wa Wazazi mkoa wa Njombe, Hussein Mwaikambo alionya pia wajumbe kutunza siri za vikao na kuacha kujipitisha mapema kabla ya muda wa kampeni haujafika akifafanua ni mambo ambayo hukipasua chama.

“Tunaunga mkono maagizo ya Mangula kwamba, tusubiri muda ufike. Viongozi tusiwabebe wagombea,” anaoanya Mwaikambo.

Mwaikambo anasema kwa sababu chama hicho kinaongozwa na kanuni basi kamati ya maadili iwawajibishe wanaokiuka kanuni hizo.

“Chama chetu hakijiendeshi hivi hivi, kina vikao vya maadili kwa hiyo kama watu hawatasikia kwenye hili wachukuliwe hatua tu ili twende sawa,” anasema Mwaikambo.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Wazazi kutoka Tanga, Daudi Nchia anasema suala la kuanza kujipitisha kabla ya chaguzi huwa linasababisha migongano japo chama kinahitaji kupata mtu sahihi mapema.

Kwa upande wake, Katibu wa Wazazi kutoka Kondoa, Bahati Mwaipungu anasema wataendelea kusimamia katiba ya chama hicho kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi za chama kulingana na maadili.

“Mangula ameongea sahihi kabisa tunahitaji vifua na hatutakiwi kubeba watu na kuingia nao kwenye vikao kwa sababu tukifanya hivyo hatutaweza kutenda haki,” anasema.

Uchaguzi wa 2020 iwe ajenda

Mangula anasema kinachotakiwa sasa ndani ya chama hicho ni kufanya uchaguzi mkuu kuwa ajenda ya kudumu kwenye kila kikao.

Anasema mwisho wa uchaguzi wa serikali za mitaa ndio mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi ujao.

Jumuiya ya Wazazi imefikisha idadi makongamano yaliyoandaliwa na jumuiya hiyo yakianzia ngazi ya kata kwa lengo la kupongeza utekelezaji wa ilani ya CCM unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano.

“Tumeona kazi mbalimbali zikifanywa na serikali yetu kupitia sekta mbalimbali nasi tumeona ni vizuri tukapongeza juhudi hizi,” anasema Dk Mndolwa.

Ushindi wa Serikali za mitaa

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba, Mangula anasema ushindi wa CCM ulitokana na maandalizi mazuri waliyokuwa wameyafanya tangu awali.

Anasema rekodi ya chama hicho imekuwa nzuri tangu mwaka 1994 wakati uchaguzi wa serikali za mitaa ulipoanza kufanyika kwa mfumo wa vyama vingi.

“Muwashangae wanaoshangaa ushindi wa kishindo wa CCM, upande wa wenzetu walifanya makosa ya kisheria na ndio maana wakashindwa,” anasema Mangula.

Anavituhumu vyama vya upinzani kwa kukosa demokrasia ndani ya vyama vyao kwa sababu hawakua na mchakato wa kupata majina ya wagombea wa uchaguzi huo.

Ombi la wazazi kuhusu viti maalum

Kati ya maombi ya Jumuiya ya Wazazi kwa CCM ilikuwa ni kupata madiwani na wabunge wa viti maalum kwa idadi sawa na jumuiya nyingine ndani ya chama hicho.

Desemba 12, 2017, Rais John Magufuli alipokea ombi la jumuiya hiyo la kutaka idadi ya wabunge na madiwani wa viti maalum iwe inatolewa sawa na jumuiya nyingine za Umoja wa Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT).

Wakati idadi ya wabunge wa viti maalum wanaotokana na jumuiya hiyo ikiwa ni wawili pekee ambao ni Zainab Mwamwindi na Nagma Murtaz hakuna madiwani wanaotokana na wazazi.

Dk Mndolwa alitumia kongamano hilo kukumbushia ombi lao.

Anasema jumuiya zote zina nafasi sawa ndani ya CCM na wanataka wabunge wao wachaguliwe na baraza lao la wazazi na sio mabaraza ya jumuiya nyingine.

“Sisi ndio tunajua wawakilishi wetu wanaotufaa kama tunachaguliwa na jumuiya nyingine inakuwa sio sawa,” anasema Dk Mndolwa.

Anasema kama ilivyo kwa jumuiya nyingine wanatamani kuona wabunge wanaotokana na wazazi wanapitishwa kwenye michakato ya awali na mwisho, wamalizie kwenye baraza la wazazi na sio vinginevyo.

“Katika maandiko ya kitabu cha Habakuki 1, mstari wa saba mpaka wa 14, inaonyesha namna Mungu alivyomsikia Nabii Habakuki, nasi tunaomba Rais Magufuli asikie maombi yetu, tunaomba mfahamu kuna watu wasioipenda jumuiya hii,” alisema Dk Mndolwa alieleza wakati wa kongamano hilo.

Mndolwa alitumia nafasi hiyo kumuomba Mangula kumfikishia Rais Magufuli ombi lao la kutaka jumuiya yao kuongezewa nafasi za viti maalum.

Mangula ambaye anaahidi kufikisha ombi hilo kwa mwenyekiti wa chama hicho kama lilivyotolewa na wazazi.