Maswali magumu Makonda kuzuiwa kwenda Marekani

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Hatua ya Marekani kumpiga marufuku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuingia nchini humo imeibua maswali magumu, huku baadhi ya wachambuzi wakieleza kuwa inalenga kutoa tahadhari kwa Serikali kuelekea uchaguzi mkuu.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani juzi imesema sababu za kumzuia ni pamoja na kuhusika kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, kukandamiza upinzani.

Makonda pia amehusishwa na ukandamizaji wa wapinzani, kuminya uhuru wa kujieleza na kukusanyika na kulenga baadhi ya makundi katika jamii.

Mwandishi wetu aliyemfuata Makonda wakati akitoka katika maonyesho ya wiki ya sheria Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, hakuweza kupata maoni yake kuhusu zuio hilo.

Mwandishi huyo wa Mwananchi alimuuliza Makonda kuhusu uamuzi huo wa Marekani, lakini kabla ya kumaliza kumuuliza, Makonda aliondoka eneo hilo akiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha.

Taarifa ya wizara hiyo ilieleza kuwa uamuzi huo umetokana na jinsi Marekani inavyofuatilia uvunjwaji wa haki za binadamu nchini Tanzania pamoja na kuonyesha kuunga mkono uwajibikaji.

“Idara hii inamtangaza hadharani Paul Makonda chini ya kifungu cha 7031 (c) cha FY2020 cha Sheria ya Idara, Uendeshaji wa Mambo ya Nje na Programu Zinazohusiana kutokana na kuhusika kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,” inasema taarifa hiyo ikitoa mifano ya ukiukwaji huo.

Taarifa hiyo inasema inao ushahidi kuwa Makonda alihusika katika vitendo hivyo akiwa mkuu wa mkoa.

“Kwa nafasi hiyo, pia anahusishwa na ukandamizaji wa siasa za upinzani, ukandamizaji wa haki za kujieleza na kukusanyika na kulenga makundi ya wachache,” inasema taarifa hiyo.

“Kifungu cha 7031 (c) kinasema iwapo Waziri wa Mambo ya Nje atapata habari za uhakika kuwa viongozi wa mataifa ya nje wamehusika katika rushwa kubwa au ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, watu hao na wa karibu katika familia zao hawana sifa za kuingia Marekani.”

Imesema zuio hilo pia linamuhusu mkewe Mary Felix Masenge.

Mbali na barua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo aliandika katika akaunti yake ya Twitter kuhusu marufuku hiyo.

“Leo tumemtangaza Makonda kuwa hana sifa ya kuingia Marekani kutokana na kuhusishwa kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu. Tuna wasiwasi mkubwa na kuporomoka kwa heshima ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania,” ameeleza Pompeo katika ujumbe wake.

Zuio hilo liliibua mjadala tangu juzi usiku na watu waliofuatwa na Mwananchi jana walikuwa na maoni tofauti, baadhi wakijiuliza kuhusu hatima yake.

Wako wanaohoji kama ataendelea na wadhifa huo katika kipindi ambacho Serikali inataka kuonyesha taswira nzuri kwa jumuiya ya kimataifa.

Pamoja na kwamba zuio hilo linamuhusu Makonda, nafasi yake kama mkuu wa mkoa ni ya ya juu kisiasa, ikiwa sawa na ya waziri na hivyo marufuku hiyo inaweza kuwa changamoto kubwa kwa Serikali.

Na pengine ndio maana mwenyekiti wa kwanza wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba aliona zuio hilo ni kama tahadhari kwa Watanzania.

“Marekani hawataishia kwa kiongozi huyo peke yake,” alisema.

“Katika hili Serikali ingeweza kukaa pamoja na kushauriana namna ya kulimaliza, lakini haikufanya hivyo na badala yake vikwazo vinaendelea kuwekwa.”

Maswali mengine ni kama zuio hilo ni sahihi kwa kuwa limewekwa kwa msimamo na mtazamo wa taifa jingine na taarifa ambazo wengi hawana au hawazielewi.

Moja ya tafsiri za ukiukwaji wa haki za binadamu iliyo katika taarifa hiyo ni kuwanyima watu haki ya kuishi, uhuru na usalama wa watu, jambo ambalo halijaeleweka lilitendekaje.

Maswali mengine ni kwa vipi hatua hiyo itaathiri taifa wakati imeelekezwa kwa watu wawili.

Wakati Zimbabwe inalalamika kuwa vikwazo ilivyowekewa na Uingereza pamoja na marufuku ya watu na taasisi 141 waliozuiwa kuingia Marekani na nchi washirika, ndio sababu ya matatizo ya kiuchumi, taifa hilo tajiri duniani linahusisha kuporomoka huko na uendeshaji mbaya wa kiuchumi.

Katika taarifa yake, Marekani haikutaja vitendo ambavyo Makonda amevifanya vinavyoonyesha kuwa alikiuka haki za binadamu, kuzuia uhuru wa kujieleza na kukusanyika na kushambulia makundi ya wachache.

Lakini mkuu huyo wa Dar es Salaam amekuwa akiendesha shughuli zake kwa mikakati inayoonekana ni kampeni, lakini hufifia na baadaye kutoweka, mambo ambayo yamekuwa yakisababisha akosolewe kila mara na wakati mwingine kujadiliwa na Bunge.

Miongoni mwa matukio hayo ni kutangaza kuzuia wanasiasa mkoani kwake na mbunge wa Sumbawanga (CCM), Aeshi Hilaly alidai ni miongoni mwa walioathirika.

Alisema hayo Aprili 11, 2017 bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alisema Makonda alimtishia maisha mbele ya mkuu wa wilaya ya Kinondoni Ali Hapi (sasa Mkuu wa Mkoa Iringa).

Makonda pia alituhumiwa kwenda kituo cha televisheni cha Clouds usiku wa Machi 17, 2017, akiwa na askari na kulazimisha watangazaji wa kipindi cha Shilawadu kurusha habari aliyoitaka.

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye aliunda kamati ya kuchunguza suala hilo na kutoa ripoti iliyomtia hatiani, lakini kamati hiyo ilidai kuwa Makonda hakukubali kuhojiwa.

Tukio jingine ni la Februari 2017, wakati Makonda alipoitwa kujieleza mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa madai ya kutoa kauli za kulidharau Bunge.

Matukio mengine yaliyozua gumzo ni hatua ya Makonda kutoa orodha ya watu aliowatuhumu kuhusika na matumizi na biashara ya dawa za kulevya Februari 2017.

Orodha hiyo iliwahusisha wanasiasa, viongozi wa dini na wafanyabiashara, ikielezwa hatua hiyo ililenga kuwakomoa wabaya wake.

Hatua hiyo ilimuingiza Makonda katika mgogoro na Askofu Josephat Gwajima wa kanisa la Ufufuo na Uzima, ambaye alikuwa akikosoa masuala mbalimbali ya nchi na wakati mwingine kumsema Makonda.

Miongoni mwa masuala hayo ni kudai kuwa Makonda alighushi vyeti vya elimu. Hata hivyo Makonda hakuwahi kujibu madai hayo.

Lakini Oktoba 4, 2017 Rais alisema hana shida naye endapo ameonekana kuwa mchapakazi katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Katika tukio jingie, Makonda alianzisha kampeni ya kuwasaka wapenzi wa jinsia moja, jambo lililoibua mgogoro na Umoja wa Ulaya.

Lakini baadaye Serikali ilimkana, ikisema hatua hizo ni zake binafsi na hazina baraka za nchi.

‘Hatujafikia ukiukwaji huo’

Hatua hiyo ya Marekani imepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wadau wa haki za binadamu.

“Hatua hiyo inalenga kutoa tahadhari kwa Tanzania katika eneo la haki za binadamu kabla mambo hayajaharibika,” alisema mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo ole Ngurumwa.

“Licha ya Tanzania kutofikia kiwango kikubwa cha uvunjifu wa haki za binadamu, Marekani imechukua hatua hiyo kabla mambo hayajaharibika kabisa.

“Haya mambo huwa yanakwenda polepole, hata Rwanda walianza tangu miaka ya sitini, lakini walikuja kupigana mwaka 1994. Hoja yao ni kwamba tufike mahali tukae pamoja tuzungumze. Hakuna kitu kizuri kama kuzungumza mkiwa na amani.

“Rwanda ilifika mahali wanazungumza, lakini ndugu wameshauana. Kenya hivyo hivyo, walikuja kukaa kwenye vikao watu wameshauana.“Mwaka huu ni wa uchaguzi ndiyo maana Marekani wanakuwa makini kwa sababu wanajua siasa zisiposimamiwa vizuri zitatuingiza kwenye machafuko, kwa hiyo tusifike huko,” alisema.