Maswali yasiyojibika uandikishaji uchaguzi Serikali za Mitaa

Dar/ Mikoani. Wakati Serikali na vyama vya siasa wakiwahamasisha wananchi kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, kumekuwa na maswali mengi yasiyo na majibu kuhusu uchjaguzi huo.

Uchaguzi huo wa ngazi ya kwanza ya uongozi wa Serikali utahusu wenyeviti wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji pamoja na wajumbe wao.

Lakini maandalizi yake, hasa uandikishaji wapigakura, yameibua maswali kadhaa, na hasa kutoka kwa viongozi wa vyama vya upinzani na Mwananchi ilipitia sehemu kadhaa za uandikishaji kushuhudia matatizo hayo.

Maswali yaliyozuka miongoni mwa wadau ni pamoja na utunzwaji wa vifaa vya kuandikishia wapigakura kama daftari la orodha ya wanaojiandikisha, uandikishaji usiotumia utambulisho wowote rasmi, uandikishaji usio na mwongozo wa maswali ya jinsi ya kupata taarifa za anayetaka kujiandikisha na mawakala kuweza kuondolewa vituoni.

Wasiwasi huo unakuja wakati Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo akitangaza ongezeko la takriban watu milioni 4 kutoka idadi iliyotangazwa siku tatu zilizopita.

Jafo aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa hadi kufikia saa 12:00 jioni Oktoba 14, watu milioni 15.54 (sawa na asilimia 68) ya matarajio ya watu milioni 22.9, walikuwa wamejiandikisha.

Hifadhi ya daftari

Kuhusu utata wa hifadhi ya daftari wanalotumia kuandikisha wapigakura, waandishi wetu walielezwa na baadhi ya waandikishaji kuwa hiyo ni changamoto kubwa.

“Tukifunga kituo kama hakuna usafiri wa uhakika tumekuwa tukihifadhi nyaraka ofisi za serikali na wengine tunaondoka navyo,” alisema mwandikishaji aliyeomba kuhifadhiwa jina.

Mwingine kutoka wilayani Arumeru, alisema kutokana na tatizo la usafiri na mvua, wanahifadhi popote wanapoona pana usalama.

Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi jijini Arusha, Bina alisema: “Mwandishi naomba utuachie sisi masuala ya usalama kwa kuwa vifaa vyote vipo salama na tunaomba vyombo vya habari mtusaidie kuhamasisha watu kujiandikisha.”

Kamanda wa polisi wa Arusha, Jonathan Shana juzi alisema hali ni salama baada ya kutembelea vituo vya uandikishaji.

Hali ni tofauti kwa msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Lain Kamendu aliyesema baada ya shughuli za uandikishaji kukamilika, vifaa vyote huhifadhiwa ofisi ya kata kwa ajili ya ulinzi.

Baadhi ya mawakala waliozungumza na Mwananchi katika mitaa ya Rengua, Kilimani, Relini na Hindu, walisema vifaa huhifadhiwa ofisi maalumu ndipo kila mmoja hutawanyika.

Akijibu swali la mwandishi wa Mwananchi kuhusu utata huo, Waziri Selemani Jafo alisema: “Kuna utaratibu maalumu wa kuhifadhi na wahusika wameshapewa. Nisingependa kwenda mbele zaidi kuliongelea.”

Uhakika wa wakazi

Suala jingine tata ni jinsi ya waandikishaji wanavyoondoka vituoni kufuata watu kwa ajili ya kuwaandikisha, jambo lililozua malalamiko kwa mawakala

Utata huo umeibuka baada ya wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Muslim Kinondoni kuvutana na mawakala wawili wa Chadema na uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kinondoni Shamba jijini Dar es Salaam kutokana na wanafunzi takribani 60 kwenda kujiandikisha katika mtaa huo.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Chau Timbuka alisema wanafunzi hao wana sifa ya ukazi licha ya kanuni kutotafsiri aina gani ya ukazi unaotambulika.

“Hawa wanafunzi wanasoma chuo kilichopo mtaani, wengine wanasoma kozi miaka miwili hadi minne, huwa wanakwenda likizo nyumbani na kurudi kwa hiyo serikali ya mtaa imeshawatambua kama wakazi,” alisema Timbuka.

Lakini wakala wa Chadema, Zakazeck Massumo aligoma kuwakubalia na kwamba angewasilisha taarifa makao makuu ya chama hicho kwa ajili ya hatua zaidi.

“Hii ni mara ya pili kwa mwanafunzi hawa, hadi sasa nina orodha waliojiandikisha bila sifa ya ukazi hapa,” alisema Massumo.

“Uandikishaji unatakiwa kuzingatia kanuni, hawa wanafunzi si wakazi. Kama tunaruhusu kila mwanafunzi tutaandikisha wangapi?”

Kwa upande mwingine, NCCR -Mageuzi mkoani Kilimanjaro imelalamikia hatua ya baadhi ya waandikishaji kuhamisha kituo na kwenda kuandikisha wapigakura, maeneo ya mashambani na shule, bila ya kuwa na mawakala.

Katibu mwenezi wa NCCR Mageuzi, Hemed Msabaha alisema waandikishaji wamekwenda shule ya sekondari Royal na Scolastica kwa ajili ya kuandikisha wanafunzi bila ya kuwepo kwa mawakala, jambo alilosema ni kinyume cha taratibu.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, msimamuzi wa uchaguzi Halmashauri ya Moshi, Juma Tukosa alithibitisha kuwepo na suala hilo na kwamba walifanya hivyo kwa mujibu wa kanuni na kwamba wakati wanafanya hivyo hapakuwepo na mawakala kituoni.

Naye mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira jana aliagiza maofisa wa uchaguzi kuwafuata wale ambao bado hawajajiandikisha.

Tatizo jingine ni waandikishaji kutohoji watu wanaotaka kuandikishwa ili kupata taarifa zaidi kuhusu ukazi wao wa mtaa husika.

Waandishi wetu walishuhudia waandikishaji wakijiandikisha bila ya kuulizwa maswali wala utambulisho kuhusu ukazi wao.

Akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya uandikishaji, Waziri Jafo aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mkoa wa Dar es Salaam ni moja ya mikoa sita inayofanya vizuri ikishika nafasi ya pili, huku Kilimanjaro ikiendelea kubaki kusuasua, ikifuatiwa na Kigoma na Arusha.

“Tangu tulivyoanza mchakato huu mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Lindi na Iringa ndiyo imefanya vizuri hadi jana jioni,” alisema Jafo.

Waziri Jafo alisema Mkoa wa Pwani unaongoza kwa kuandikisha wapiga kura 473, 639 sawa na asilimia 80, ukifuatiwa na Dar es Salaam ulioandikisha watu milioni 2.06 (asilimia 77).

Alisema hadi sasa Kilimanjaro imeandikisha watu 444, 954 (asilimia 48), Kigoma 555, 856 (asilimia 53) na Arusha 551,614 (asilimia 59).

Akizungumzia tatizo la watu kuiandikisha zaidi ya mara moja, Jafo alisema tayari mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Ngeze Mwagilo (29) mkazi wa Kasanga, Manispaa ya Morogoro, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujiandikisha mara mbili ndani ya Manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Wilibroad Mutafungwa aliwaambia waandishi wa habari jana mtuhumiwa anadaiwa kujiandikisha katika kituo cha Kasanga, Kata ya Mindu na baadaye kwenda kujiandikisha kituo cha Kiwanja cha Ndege, kata ya Kiwanja cha Ndege.

Imeandikwa na na Elias Msuya, Bakari Kiango, Elizabeth Edward, Florah Temba, Kelvin Matandiko, Mussa Juma, Joyce Joliga na Fina Lyimo.