Matukio matano yatikisa kesi ya Mbowe, vigogo Chadema

Thursday September 12 2019

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe (katikati)

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe (katikati) akiwa na viongozi wenzake na wanachama wao walipokuwa wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar Es Salaam. Wakati kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ikiahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, matukio matano yameibuka katika kesi hiyo.

Matukio hayo ni Mbowe kutaka kujua idadi ya mashahidi; mbunge wa Tarime Mjini, John Heche na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) kulalamika kutumia gharama kubwa kuja katika kesi hiyo na kuwa na shughuli nyingi; wakili upande wa utetezi, Peter Kibatala kushindwa kumhoji shahidi wa saba; shahidi wa nane kushindwa kutoa ushahidi wake na wakili Profesa Abdallah Safari kuhoji kuhusu idadi ya mashahidi.

Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho wakiwemo wabunge sita wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Washtakiwa hao wamefikia hatua hiyo, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi wakiitaka mahakama iahirishe kesi hiyo hadi leo, kutokana na shahidi wa nane, Bernad Nyambari(42) ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Kipolisi ya Mbagala, kutoka safarini na kupitilia moja kwa moja mahakamani hapo kutoa ushahidi bila kupata muda wa kupumzika.

Ombi la kuahirisha kesi hiyo lilitolewa na Wakili wa Serikali Faraja Nchimbi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba.

Nchimbi alisema Nyambari alikuwa katika oparesheni ya kikazi ya siku tatu nje ya mkoa wa Dar es Salaam, hivyo alipopewa barua ya kuitwa mahakamani alikuja moja kwa moja bila kupata muda wa kupumzika.

Advertisement

Lakini Mchungaji Msigwa alinyoosha mkono na kuomba kesi isiahirishwe kwa kuwa washtakiwa wanatoka sehemu tofauti na wana majukumu mengine.

Naye Heche alidai anatoka mbali na gharama za kukaa Dar es Salaam ni kubwa “hivyo kuahirisha kesi hii ni kama tunakomolewa”.

Kwa upande wake Mbowe alihoji idadi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, swali ambalo hata wakili wao, Profesa Safari alidai alishauliza lakini hakuambiwa.

Akijibu hoja hiyo, Nchimbi alidai kuwa hilo si hitaji la kisheria, na kwamba wajibu wao ni kuhakikisha kuwa wanaleta mashahidi wa kutosha ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea .

Awali, akitoa ushahidi wake, Nyambari alidai kuwa anakumbuka Februari 2018, wilaya ya Kinondoni ilikuwa katika kampeni ya uchaguzi mdogo wa ubunge.

Akiongozwa na wakili mkuu wa Serikali, Dk Zainabu Mango, shahidi huyo ambaye ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, alidai kuwa kabla ya kuwa mkuu wa upelelezi wia Mbagala, alikuwa msaidizi wa Mkuu wa upelelezi Kinondoni.

Advertisement