Matumaini mapya Magufuli na wapinzani

Dar es Salaam. Katika kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni kuibua matumaini mapya ya maridhiano, Rais John Magufuli jana alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi watatu wa vyama vya upinzani Ikulu, Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuhimiza haja ya kudumisha amani, usalama na upendo.

Viongozi waliokutana na Rais kwa nyakatofauti ni Mshauri wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.

Hata hivyo, haikueleweka mara moja kama kukutana huko kutakuwa na mwendelezo wa vikao vingine vya viongozi wengine wa upinzani.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa alipoulizwa kwa simu alisema suala hilo ni siri ya ratiba za rais.

“Siwezi kusema kama kutakuwa na mikutano mingine au hapana. Hilo litategemea uamuzi wa rais na hao wanaotafuta kuonana naye au ambao anataka kukutana nao,” alisema Msigwa.

Kupitia video iliyotumwa kwenye mitandao ya jamii, Maalim Seif baada ya kukutana na Rais alisema mazungumzo yao yalijikita katika mambo ya nchi na kuifanya nchi kuwa na amani, salama na upendo kwa wote.

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alimsifu Rais Magufuli kwa kuwa wazi na kuwa tayari kwa kuzungumza na raia wake akiwamo yeye.

Hata hivyo hakutaka kwenda kwa undani wa kile walichozungumza.

“Nimefurahi sana, nimeridhika, sasa kwa hayo mengine tumezungumza mimi na rais, sasa yale ya ndani huwezi kuyasema publicly (hadharani), bila shaka akitaka tukutane tutakutana tena,” alisema.

Pia Maalim Seif alielezea kufurahishwa na dhamira ya Rais Magufuli kukutana na viongozi mbalimbali na kujadiliana mambo yenye maslahi na nchi.

Hii ni mara ya pili kwa maalim Seif kukutana na Rais Magufulu Ikulu, mara ya kwanza ilikuwa Desemba 21, 2015 Maalim Seif akiwa bado katibu mkuu wa CUF, alifika Ikulu ambapo pamoja na mambo mengine, walizungumzia kuvurugika kwa uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Hata hivyo, CUF walisusia uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, 2016 na kuzidisha mpasuko kati ya chama hicho na CCM.

Machi 2019 Maalim Seif na kundi lake walihamia ACT-Wazalendo baada ya kutofautiana na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahm Lipumba.

Maalim Seif amekutana na Rais Magufuli wakati chama chake kikiwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa ndani ambao yeye amepitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa kugombea uenyekiti wa chama hicho.

Mbali na Maalim Seif, Rais pia alikutana na Profesa Lipumba ambaye baada ya kutoka alimpongeza mwenyeji wake kwa ahadi kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu (2020) utakuwa huru na wa haki.

“Amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano kupambana na rushwa, kudhibiti matumizi ya Serikali, kulinda na kutumia vizuri rasilimali za Taifa, kuboresha elimu na kuimarisha uchumi,” taarifa ya Ikulu imemnukuu akisema.

Profesa Lipumba naye aliwahi kukutana na Rais Magufuli Ikulu Novemba 2015 ambapo pamoja na mambo mengine alimpongeza kwa kushinda katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Hata hivyo, wakati huo Profesa Lipumba alikuwa amejiuzulu uenyekiti wa CUF tangu Agosti 2015 alipoeleza kutoridhishwa na mwenendo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliohusisha chama chake na vyama vingine vya upinzani ambavyo kwa pamoja vilikuwa vikimuunga mkono Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea urais.

Profesa Lipumba aliyerudi kwenye uongozi wa chama hicho tangu Agosti 2016 na kutofautiana na Maalim Seif na kundi lake, amekuwa akisisitiza siasa za maridhiano.

Kwa upande wake Mbatia naye alifika Ikulu jana akieleza dhamira ya Rais Magufuli juu ya Uchaguzi Mkuu kuwa huru na wa haki ametaka wanasiasa waache kukamiana na kuchochea mambo hasi dhidi ya Taifa.

Novemba 13, 2018 Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) alikutana na Magufuli ikiwa ni jitihada za kituo hicho kutafuta maridhiano ya kisiasa. “Kubwa kuliko yote, la msingi ni meza ya masuluhisho, meza ya maridhiano na ndiyo maana mimi sikujikita kwenye masuala binafsi, nilisema nimekuja kwa mambo ya msingi ya Taifa na ndiyo msimamo wangu mpaka kesho,” alisema Mbatia alipozungumza na Mwananchi Januari 2019.

Akizungumza kuhusu mazungumzo yake na Rais Magufuli jana, Mbatia alisema Rais Magufuli ameendelea kusisitiza uchaguzi huo kuwa huru na haki. “Nadhani ameongea na vyama vingine pia, na mie amenialika kama NCCR, nimeuliza nchi hii tunaipeleka wapi? Akaniambia ‘kama nilivyowaambia mabalozi naendelea kusisitiza uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na haki’,

“Mie nikamwambia uchaguzi ukishamalizika, nchi inaendelea kuwepo, kwa hiyo wadau hasa vyama vya siasa tukae tuzungumze tuone yanayowezekana kwa mujibu wa sheria, kanuni tuyazungumze, (Rais) amenihakikishia, kauli yake ilikuwa thabiti, naamini ameongea na vyama vingine.”

Kukutana kwa Rais Magufuli na viongozi hao wa upinzani kumekuja miezi michache tangu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipomshauri Rais Magufuli kuanzisha maridhiano ya kisiasa wakati wa maadhimisho ya uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika Desemba 9, 2019 jijini Mwanza.

Kama hiyo haitoshi, katika barua waliyomwandikia Rais Magufuli Januari 29, 2020, Chadema walimwomba mambo matatu likiwemo la marekebisho ya katiba yatakayozaa tume huru ya uchaguzi.