Matumaini mapya gesi majumbani

Dar es Salaam. Wakati bei ya gesi ya matumizi ya majumbani ikipaa nchini bila ya dalili za kasi kupungua, angalau kuna tumaini jipya; kuna kampuni imewekeza katika kuzalisha mitungi hapa nchini.

Kampuni ya Supreme Holding inatarajia kuwekeza dola 25 milioni za Kimarekani (Sh40 bilioni) katika kiwanda cha kutengeneza mitungi, hatua ambayo inatarajiwa kushusha bei ambayo ni kikwazo kikubwa kwa mtu anayetaka kuanza kutumia nishati hiyo.

Kiwanda hicho kitajengwa wilayani Mkuranga, Pwani na kukamilika kwake kutaashiria kupungua kwa bei ya mitungi na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji, jambo ambalo Waziri wa Nchi-Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mussa Azan Zungu amesema linatakiwa ili nishati hiyo ianze kununuliwa kwa zabuni na hivyo bei yake kuratibiwa.

Kwa sasa bei ya mtungi wa kilo 15, ambao hutumika zaidi majumbani kwa ajili ya shughuli za mapishi, ni hadi Sh54,000, wakati ule mdogo wa kilo sita, ambao hutumiwa zaidi na wafanyabiashara wadogo kama mamalishe, huuzwa hadi Sh23,000.

Bei ya gesi ilipanda kwa kati ya Sh1, 000 na Sh5, 000 takriban wiki mbili zilizopita.

‘Hatujawahi kuwa na uwekezaji huu’

Hata hivyo, kujitokeza kwa mwekezaji mpya katika nishati hiyo muhimu, kunaweka matumaini ya kupungua kwa makali ya bei, hasa wakati huu ambapo Serikali inadhibiti nishati nyingine kwa sababu za kimazingira.

“Hatujawahi kuwa na kiwanda cha aina hii hapa nchini na mitungi yote inayotumika kujaza gesi imekuwa ikiagizwa kutoka nje ya nchi,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki baada ya mazungumzo na mmiliki wa Supreme Holding, Dk Moharram Helal jana.

“Hii ni fursa ya kipekee kwa Tanzania ambayo ina hazina kubwa ya gesi.”

Kairuki aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mitungi 1,000 kwa siku na pia kitajaza gesi kwenye mitungi 3,000 kwa siku, ambayo itakuwa na uzito kati ya kilo 15 na kilo 30.

“Mpaka kiwanda kitapokamilika kitaajiri Watanzania 300 na Wamisri 30,” alisema waziri huyo.

Kairuki ametoa agizo kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuhakikisha kinatoa msaada stahiki kwa mwekezaji huyo ili aweze kunufaika na huduma zinazotolewa na kituo hicho.

Alisema amemuomba pia mwekezaji huyo kufikiria pia kuzalisha mitungi yenye ujazo wa chini zaidi ili watu wa kima cha chini waweze kunufaika.

Matumizi ya gesi katika shughuli za kawaida majumbani na katika biashara ndogo yamekuwa yakikua, lakini ukuaji wake si wa kasi kutokana na gharama za kuanzia.

Mtungi wa kilo 6 unauzwa hadi Sh55,000 na wa kilo 15 ni kuanzia Sh100,000, hizo zikiwa ni bei za kuanzia, wakati za kujaza gesi wakati tayari una mtungi ni Sh23,000 na Sh54,000 kulingana na kilo.

Kwa mujibu wa Ewura, uagizaji wa gesi hiyo kutoka nje uliongezeka mwaka 2018 hadi tani 142,950 za ujazo kulinganisha na tani 107, 263 za mwaka uliotangulia.

Naye Dk Helal, ambaye aliambatana na meneja wake mkuu wa Intergas, Dk Hatem Ahmed amemhakikishia Kairuki kuwa ujenzi wa kiwanda utakamilika katika muda utakaokuwa umepangwa baada ya kukamilisha taratibu za kisheria.

“Tumeamua kuja kuwekeza hapa Tanzania kwa kuwa tunaamini uzoefu tulionao katika kutengeneza mitungi ya gesi utasaidia,” alisema.

Bei ya gesi haishikiki mitaani

Mipango hiyo itasaidia kupunguza makali yaliyopo mitaani hivi sasa katika kupata nishati hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi mikoani unaonyesha bei ya gesi kupanda licha ya kampuni moja tu ya Oryx kutangaza kupandisha bidhaa zake.

Mjini Geita; gesi ya kampuni ya Mihan/Taifa imepanda hadi Sh53,000 kwa mtungi wa kilo 15 kutoka bei ya awali ya Sh48, 000. Mtungi wa kilo sita unauzwa Sh22,000 kulinganisha na bei ya Sh20,000 siku chache zilizopita.

Mtungi wa kilo 15 wa kampuni ya Oryx uliokuwa ukiuzwa Sh50, 000 umepanda hadi Sh55,000 wakati mtungi wa kilo sita unauzwa Sh23,000 kutoka bei ya awali ya Sh21,000.

Mjini Mugumu, mtungi wa kilo sita wa Manjis hivi sasa unauzwa Sh23,000 kutoka Sh20,000 wakati mtungi wa kilo 15 unauzwa Sh55,000 kutoka Sh50,000.

Mitungi ya kampuni ya Mihan/Taifa inauzwa Sh22,000 kwa kilo sita kutoka bei ya awali ya Sh21,000 wakati mtungi mkubwa wa kilo 15 unauzwa Sh53, 000 badala ya bei ya zamani ya Sh51, 000.

Hali ni kama hiyo katika miji Musoma, Mwanza na kwingineko.

‘Ni kawaida bei kupanda’

Hata hivyo, wauzaji hawaoni kama upandaji wa bei ni kitu cha kushangaza. Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, mmoja wa maofisa wa kampuni ya Taifa Gas, Hamisi Ramadhani alisema kupanda na kushuka kwa bei ya gesi ni jambo la kawaida.

“Kila siku bei inapanda na kushuka kutegemeana na sababu nyingi sana, ikiwemo eneo, mazingira ya biashara na hitaji la soko la ndani na nje ya nchi,” alisema Hamisi ambaye aligoma kutaja cheo chake.

“La msingi tambua bei zinapanda na kushuka kila siku. Hata leo nimesaini nyaraka za bei kupanda na kushuka katika baadhi ya maeneo.”

Ewura wanasemaje

Wakati wauzaji wakisema hayo, meneja mawasiliano na uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo alisema tayari wameziagiza kampuni zinazouza gesi kuwasilisha taarifa ya sababu za ongezeko hilo.

“Bei hizi zimepanda ndani ya wiki mbili sasa. Kwa uhakika ninajua ni kampuni ya Oryx ndiyo imepandisha bei kati ya Sh1,000 hadi Sh4,000 kulingana na ujazo wa mtungi. Tumewaagiza watuletee taarifa na mchanganuo wa sababu za kupandisha bei,” alisema Kaguo

“Tusiporidhika na sababu zao tutawaagiza kushusha bei kwa sababu moja ya majukumu yetu ni kudhibiti bei na kulinda maslahi ya pande zote za wauzaji na walaji.”

Kaguo alisema ni kawaida bei za bidhaa ya mafuta kupanda na kushuka kutegemeana na mahitaji na soko la dunia.

Uagizaji wa gesi nchini umepanda katika siku za karibuni kuanzia mwaka 2008, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa ziliagizwa tani 8,000 kwa mwaka.

Athari wa kupanda kwa bei

Kupanda huko kwa bei katika nchi ambayo takriban asilimia 71.2 inatumia kuni na mkaa, kunaweza kuwa na athari tofauti, kuanzia za kimazingira hadi kiuchumi.

Mwananchi linafahamu kuwa ongezeko hilo la kutoka Sh 48,000 hadi Sh55,000 kwa mtungi wa kilo 15 linapunguza matumizi ya nishati hiyo kutokana na hali ya kiuchumi.

Lakini kikubwa zaidi ni kutosambaa kwa kasi zaidi kwa matumizi ya nishati hiyo rafiki wa mazingira na hivyo kutokoma kwa matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanaathiri mazingira.