Mahakama 'yamsaka'mkulima wa ukomo wa urais kwa magazeti

Wakili Jebra Kambole (katikati) akimweleza jambo Kiongozi wa Act-Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) walipokuwa wakitoka Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam jana, baada ya shauri la chama hicho kujiunga katika kesi ya kupinga ukomo wa uraisi kutajwa mahakama hapo. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. Mahakama Kuu imemtaka Dezydelius Mgoya, mkulima aliyefungua kesi ya kupinga ukomo wa urais, afike mahakamani hapo Oktoba 10, akikubali ombi la mawakili kumtangazia wito huo kwa njia ya magazeti.

Hatua inatokana na wakili Jebra Kambole anayekiwakilisha chama cha ACT–Wazalendo kinachotaka kuingizwa kwenye kesi hiyo, kumueleza Jaji Benhajj Masoud kuwa pamoja na kupewa wito wa kumtaka afike mahakamani hapo jana, hawakufanikiwa kumpata kwa sababu hawakujua anaishi wapi.

Alisema kutokana na unyeti na uharaka wa jambo hilo, Kambole aliiombia mahakama kuwa wanaweza kumtangazia wito huo kwenye gazeti ili umfikie haraka.

Mgoya amefungua kesi Mahakama Kuu akipinga ukomo wa urais ambao ni vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja, lakini ACT Wazalendo imesema ina maslahi katika kesi hiyo na hivyo kuomba kujumuishwa.

Kabla ya kukubaliana na hoja hiyo, wakili wa Serikali, Daniel Nyakiha aliomba wapewe siku saba ili kama wana hoja zozote za kupinga maombi ya ACT- Wazalendo wanaoomba kujumuishwa kwenye kesi hiyo, waziwasilishe.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Masoud aliwapa siku hizo saba na pia kukubali Mgoya atangaziwe wito kwenye magazeti yanayosomwa zaidi ili Oktoba 10, afike mahakamani kusikiliza shauri hilo na apewe nyaraka ili na yeye kama ana utetezi wowote autoe.

Maombi ya ACT-Wazalendo kujumuishwa katika kesi hiyo, yalibainishwa Septemba 30, 2019 na Jaji Kiongozi, Dk Eliezer Felesh wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya maelekezo maalumu ya namna ya usikilizwaji wa pingamizi la awali la Serikali dhidi ya kesi hiyo.

Dk Feleshi ndiye kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi ya kupinga ukomo wa Rais iliyofunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Majaji wengine ni Dk Benhajj Masoud na Seif Kulita.

Maombi hayo yamewasilishwa na bodi ya wadhamini ya chama hicho inayowakilishwa na kampuni ya uwakili ya Law Guards Advocates chini ya hati ya dharura, wakiomba yasikilizwe haraka, hivyo mahakama imesimamisha usikilizwaji wa kesi ya msingi ili kusikiliza kwanza maombi ya ACT-Wazalendo.

Mgoya alifungua kesi hiyo chini ya kifungu cha 4 cha sheria ya utekelezaji haki na wajibu, sura ya 3 ya mwaka 1994 chini ya Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Mgoya anahoji Ibara ya 40 (20) ya Katiba ambayo imeweka ukomo wa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano ya Rais.

Anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.

Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri ya masharti ya Ibara ya 42 (2) ya Katiba kwa kuhusianisha na masharti ya Ibara za 13, 21 na 22 za Katiba hiyo. Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya Ibara hiyo ya 40(2) kwa kuhusianisha na Ibara ya 39 ya Katiba.

Akizungumza jana nje ya Mahakama, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema ni wajibu wa chama chochote cha siasa pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kinalinda Katiba, na wao wanaona kesi ilifunguliwa na Mgoya inaweza kuleta shida za kikatiba.

“Kwa hiyo tuna maslahi ya kuhakikisha tunalinda ukuu wa Katiba, ndiyo maana tumeiomba mahakama na sisi tujumuishwe kwenye kesi hiyo,” alisema Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini.

Alisema lengo lao ni kuhakikisha wanajenga hoja za kulinda Katiba ya Tanzania, na hasa ukomo wa urais ili mtu anayetumikia nafasi ya rais aongoze kwa kadri Katiba inavyotamka.

“Lengo ni kuhakikisha tunalinda katika ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania,” alisema Zitto.