Mawaziri watano watangaza kujiuzulu Uingereza

Waziri Mkuu wa Uingereza, Borisi Johnson.

London, Ungereza. Kundi la mawaziri watano liko mbioni kujiuzulu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutofatiana na mpango wa Waziri Mkuu, Borisi Johnson.

Waziri Mkuu Boris anakabiliwa na upinzani mpya kutoka kwa baraza lake la mawaziri kutokana na wasiwasi wa kutofikiwa kwa makubaliano ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) maarufu kama Brexit.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa leo Jumatano Oktoba 9, katika gazeti la The Times, kundi la mawaziri hao limepanga kujiuzulu ili kupisha mpango huo.

Gazeti hilo liliwataja mawaziri walio katika orodha hiyo kuwa ni pamoja na Nicky Morgan (utamaduni), Julian Smith (anayehusika na Ireland Kaskazini), Robert Buckland (sheria), Matt Hancock (afya) na Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo, Geoffrey Cox.

Gazeti hilo lilimnukuu mmoja wa mawaziri hao ambaye hata hivyo, hakutaka kutajwa jina lake akisema kuwa idadi kubwa ya wanachama wa Conservative watajiuzulu iwapo hakutakuwa na makubaliano ya Brexit.

Hata hivyo, hivi Oktoba 3, waziri Boris alinukuliwa akisema kuwa hakuna kitu kinachoweza kucheleweza mpango wa nchi hiyo kujitoa katika Umohuo.

Tayari waziri Boris amewasilisha mapendekezo yake kuhusu marekebisho ya makubaliano ya mpango huo wa kuiondoa nchi hiyo katika EU.

Mapendekezo hayo ya mpango wa Brexit yanajumuisha pia fursa ya Uingereza kuhusu kuondolewa sera inayoleta utata ya kusimamia mpaka wa Ireland.

Zaidi ya miaka mitatu sasa tangu ilipofanyika kura ya maoni mwaka 2016, Uingereza inaelekea katika kujitoa katika Umoja huo bila ya makubaliano ifikapo Oktoba 31.

Akiwasilisha mpango huo, Boris alisema “tunaondoka EU Oktoba 31, hakuna cha kutuchelewesha. Kama ilikuwa shule ingekuwa imefungwa lakini katika hili siwezi kuomba tena Brussels nyongeza.”