Mbio za kumrithi Dk Shein zawa moto Zanzibar

Thursday September 19 2019

Makamu wa Rais na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM

Makamu wa Rais na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan, akifungua Semina ya Mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi na makada wa Chama Cha Mapinduzi iliyofunguliwa jana mjini Dodoma. Picha ya maktaba 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Kwa miezi kadhaa kila kiongozi wa CCM na Serikali yake anayezungumzia siasa za Zanzibar, haachi kuwakemea makada wanaojipitisha kutaka kuwania urais wa visiwa hivyo baada ya Dk Ali Mohamed Shein kumaliza muda wake.

Aliyeanza kuwakemea ni Dk Shein mwenyewe aliyesema yeye bado ni rais na kwamba nafasi hiyo haipatikani kwa kampeni za chinichini bali kupitia vikao vya chama.

Baadaye katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alikemea tabia hiyo alipotembelea Zanzibar akiwataka wanaofanya hivyo wakome. Hata Kamati Kuu ya CCM iliwahi kuwakemea watu hao.

Ingawa wanasiasa wanaokemewa kwa kampeni hizo za mapema hawatajwi hadharani, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan alijitokeza akasema “kuna maneno kwamba Samia anakuja kugombea urais Zanzibar, nataka kuwaambia kuwa si kweli na sina nia hiyo”.

Pamoja na kwamba wanaopigana vikumbo kwa ajili ya nafasi hiyo ya juu Zanzibar hawajatajwa wala kujitokeza, wananchi wametaja makada kadhaa wa CCM ama waliokuwa wanatajwa au wenye sifa za kurithi nafasi ya Dk Shein.

Na pengine kutokana na kukemewa na kila kiongozi anayesimama kuzungumza, wanasiasa wengi wanajitenga na nia au mipango hiyo.

Advertisement

Katibu mwenezi wa CCM Zanzibar, Catherine Peter Naye anasema kwa sasa hana taarifa kama kuna baadhi ya makada wanaendelea na kampeni.

“Rais mzuri atatoka ndani ya CCM na hata wale zaidi ya kumi waliokuwa wanajipitisha mwaka jana, baada ya Kamati Kuu kutoa tamko, wameacha kampeni zao za chinichini,” anasema Catherine.

Hata hivyo, naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma Mabodi anasema CCM upande wa Zanzibar haijatoa msimamo wa aina ya rais anayetakiwa na sifa zote za kiongozi kupitia chama hicho atapatikana kupitia kwenye vikao vya chama.

Pia, Dk Mabodi anasema CCM haitamchagua mgombea anayetokana na makundi yaliyomo ndani ya chama hicho.

Dk Mabodi anasema suala la wagombea urais Zanzibar huwa linashabikiwa sana na wapambe na “kuna wengine wanatajwa tu hata wao hawafahamu. Zanzibar wapambe wana nguvu sana kuliko wagombea wenyewe.”

Anaongeza kuwa “unajua utakuta mtu anatajwa kwamba anataka kuwania urais lakini mkimuuliza anasema hajui lolote,” anasisitiza.

Dk Mabodi anasema mwaka jana kulikuwa na wimbi la wapambe waliokuwa wakipita kunadi wagombea wao, lakini baada ya onyo la kamati kuu pia onyo lililotolewa na Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na lile lililotolewa na Dk Shein alipozungumza na mabalozi wa nyumba kumi imesaidia kutuliza hali.

Waliokuwa wanatajwa

Miongoni mwa viongozi wanaotajwa kwamba wanafaa urais ni Waziri wa Maji wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ambao hata hivyo wanajiweka mbali na nafasi hiyo.

Profesa Mbarawa anasema yeye hana vigezo vya kuwania nafasi hiyo na jukumu lake kwa sasa ni kuhakikisha Watanzania wanapata maji.

Masauni kwa upande wake anasema ana mambo mawili anayoshughulika nayo kwa sasa, mengine ni kauli za watu.

Anasema kauli kwamba anatajwa katika kuwania nafasi ya urais kwake ni ngeni na hata kama angekuwa na nia hiyo, bado ana majukumu mazito aliyopewa na wananchi na Rais John Magufuli.

“Kwangu hilo ni geni, nafasi nyeti kama hizo huwa haziombwi na wala huwezi kuanza kuzisemea bali hupangwa na Mungu kupitia wenye mamlaka, mimi waliona nafaa kuwa mbunge wakanipa, lakini mheshimiwa Rais aliona nafaa kumsaidia katika nafasi ya naibu waziri pia akanipa, namshukuru sana,” anasema Masauni.

Viongozi wengine wanaotajwa kuwa na sifa za kuwania urais wa Zanzibar ni Shamsi Vuai Nahodha, waziri kiongozi wa zamani, Dk Hussein Mwinyi (waziri wa ulinzi), Mohamed Said Dimo, Mahadhi Juma, Dk Halid Salum Mohamed na Mohamed Hija.

Samia ajitenga

Mwezi uliopita, Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema hana nia ya kuwania urais wa Zanzibar.

Anasema taarifa zinazoenezwa na watu ambao hakuwataja, kuwa anataka kuwania nafasi hiyo zipuuzwe kwa kuwa wadhifa alionao kwa sasa ni zaidi ya urais wa Zanzibar.

Samia alitoa kauli hiyo katika hafla ya siku ya Kizimkazi inayofanyika Mkoa wa Kusini Unguja kila mwaka.

“Kuna maneno kwamba Samia anakuja kugombea urais Zanzibar, nataka kuwaambia kuwa si kweli na sina nia hiyo. Ukiangalia ngazi za uongozi ndani ya Tanzania mimi ni namba mbili, sina kinachonishawishi nije kugombea huku (Zanzibar) niwe namba tatu,” alisema.

“Nimeona niseme huku kwetu (Zanzibar) nilipotoka kwa sababu maneno yamekuwa mengi. Chuki nyingi, ufisadi, majungu ila kwa Samia mimi simo.”

Amewataka wananchi kutosikiliza taarifa alizodai zinalenga kumgombanisha na wengine.

Dk Shein alivyokemea

Mei mwaka jana, Dk Shein alitoa onyo kwa watu ambao wameanza harakati za kuusaka urais Zanzibar.

Rais Dk Shein ambaye ni makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar alitoa onyo hilo katika ziara yake ya kutembelea mashina ya chama hicho katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza).

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa chama na serikali tayari wameanza kupanga timu za urais badala ya kushughulika na mambo ya msingi ya kufanya shughuli za chama zitakazofanikisha kuiweka serikali madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.

“Nafasi ya urais ndani ya CCM haipatikani kwa kampeni na makundi yasiyo halali bali kwa utaratibu maalumu kupitia vikao vya kikatiba ambavyo vipo kwa mujibu wa Katiba na miongozo na kanuni za CCM,” alisisitiza.

Kauli ya Dk Bashiru

Agosti 18 mwaka jana, Dk Bashiru akiwa visiwani humo aliungana na Dk Shein akitumia neno wakome, ili kuwaonya makada hao walioanza kampeni kuusaka urais.

Dk Bashiru alisema amesikia wapo watu baadhi wana vyeo na wengine hawana, wenye ndoto ya kushika madaraka ya urais Zanzibar akiwataarifu kuwa nafasi hiyo bado haijatangazwa kuwa wazi.

“Nafasi ya urais Zanzibar haijatangazwa, bado ina mwenyewe na kutakuwa na utaratibu wa kuijaza, utaratibu huo utasimamiwa na chama si makundi hayo mnayoyapitisha pitisha mara kwenye hoteli mara kwenye ofisi za serikali. Komeni, tabia hiyo acheni,” alisema Dk Bashiru.

Anasema CCM si chama cha kusaka vyeo bali ni chama cha mapinduzi na kitaendelea kuwafuatilia wasaka vyeo kwa kuwa baadhi wanawajua na siku zao zinahesabika.

Sifa za rais anayetakiwa

Pamoja na mijadala ya majina, wananchi wa Zanzibar wanazungumzia sifa za raia wanayemtaka.

Fatma Hajji Juma ambaye ni mmoja wa wana Maskani wa Mkoa wa Mjini Magharibi, anasema wanataka kiongozi jasiri kama alivyo Rais Magufuli.

Juma ambaye pia ni mfanyabiashara katika soko la Darajani, anasema kuna matatizo mengi katika Serikali ya Zanzibar ambayo yanahitaji kiongozi kama Rais Magufuli.

“Sina maana aliyepo hana uwezo, ila tunataka mwenye uwezo zaidi na mwenye kasi ya maamuzi kama alivyo Rais Magufuli,” anasema Juma.

Kada mwingine wa CCM kwenye Maskani ya Kisonge na aliyejitambulisha kwa jina la Mohammed Mwadini Rashid anaungana na Juma kuwa wanahitaji rais kama Magufuli.

Advertisement