Mbio za urais Zanzibar zahamia mitandaoni

Wahenga wanasema mlango mmoja ukifungwa mwingine unafunguliwa. Ndivyo inavyoonekana katika mbio za urais Zanzibar ambazo sasa zimehamia mitandaoni ambako wanaCCM wanaoonekana wanafaa kuwania urais wanachambuliwa sifa zao na uwezo wao.

Huko mtandaoni ndiko wananchi wanapata fursa ya kuwaona wana CCM wanaotajwa kuwania urais na pengine kuwajua mapema.

Mtandao wa Zanzibar Forum tangu mwanzoni mwa mwaka huu umeanza kuwataja wana CCM wanaoweza kuwania urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, Katibu mwenezi wa CCM Zanzibar, Catherine Peter anasema tangu viongozi wa kitaifa wa CCM walipopiga marufuku watu kujipitisha kuwania nafasi hiyo, Zanzibar sasa hivi imetulia.

Anasema japokuwa kuna baadhi ya makada wanaandikwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba ni watia nia hiyo, wao hawajathibitisha kama ni wao.

“Unajua Zanzibar kuna wapambe wengi, anaweza akatajwa Catherine au Shija wanataka kuwania nafasi, lakini kumbe si kweli, lakini hata kama ni kweli kuna mtu anafanya hivyo, usisafirie nyota ya mwenzako,” anaonya Catherine.

Anaongeza kwamba; “Sasa hivi kulivyotulia utafikiri hatutapata mgombea mzuri, lakini ndani ya CCM kuna makada wengi wenye uwezo.”

Hata hivyo, mtandao huo kwa sasa ndio umeonekana mbadala kwa Wazanzibari kuhusu nani anaweza kuvaa viatu vya Dk Shein atakapomaliza muda wake Oktoba mwaka huu.

Makada wanaotajwa

Miongoni mwa viongozi wanaotajwa kwamba wanafaa urais ni Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano, Profesa Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ambao hata hivyo wanajiweka mbali na nafasi hiyo.

Profesa Mbarawa anasema yeye hana vigezo vya kuwania nafasi hiyo na jukumu lake kwa sasa ni kuhakikisha Watanzania wanapata maji.

Masauni kwa upande wake anasema ana mambo mawili anayoshughulika nayo kwa sasa, mengine ni kauli za watu.

Anasema kauli kwamba anatajwa katika kuwania nafasi ya urais kwake ni ngeni na hata kama angekuwa na nia hiyo, bado ana majukumu mazito aliyopewa na wananchi na Rais John Magufuli.

“Kwangu hilo ni geni, nafasi nyeti kama hizo huwa haziombwi na wala huwezi kuanza kuzisemea bali hupangwa na Mungu kupitia wenye mamlaka. Mimi waliona nafaa kuwa mbunge wakanipa, lakini mheshimiwa Rais aliona nafaa kumsaidia katika nafasi ya naibu waziri pia akanipa, namshukuru sana,” anasema Masauni.

Wengine wanaotajwa kwenye mitandao ni Haji Omar Kheir ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za mitaa na idara maalumu za SMZ.

Haji aliyezaliwa Tumbatu Januari 10, 1960 anaelezwa anazijua kiasi siasa za Zanzibar na baadhi ya mambo nyeti kutokana na nafasi yake ya uwaziri.

Mwingine anayetajwa na mtandao huo Balozi Ali Karume ambaye amekuwa Balozi wa Tanzania nchi mbalimbali ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar. Pia, ni kaka wa Rais wa awamu ya tano wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Anatajwa kuwa na uzoefu kiasi katika masuala ya kidiplomasia, anatoka katika familia ya uongozi ambao umetawala Zanzibar.

Karume anatajwa kuwa na shauku ya kuwania urais wa Zanzibar na ule wa Jamhuri ya Muungano bila mafanikio.

Mwingine anayetajwa ni Shamsi Vuai Nahodha waziri kiongozi mstaafu na mwandishi wa habari aliyezaliwa Makunduchi Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja mwaka 1962.

Anatajwa ni moja wa watu waliopata bahati ya kuaminiwa akiwa na umri mdogo na kupewa nafasi katika siasa za Zanzibar. Anatajwa kama mmoja wa watu wenye kiu ya kuukwaa urais wa Zanzibar.

Shamsi ana shahada ya kwanza aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani ya elimu na pia stashahada aliyoipata katika Chuo cha Diplomasia, Kurasini Dar es Salaam.

Mwingine anayetajwa ni Salama Aboud Talib ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ardhi, Maji na Nishati wa SMZ.

Salama anatajwa kuwa na ushawishi kwa baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT), hasa maeneo ya Mjini Unguja na Unguja Kusini.

Vilevile anatajwa Meja Jenerali (mstaafu), Issa Suleiman Nassor ambaye anaelezwa ni mtu mpole kwa tabia na amekuwa mwanajeshi kwa kipindi chake chote cha utumishi wake na kumalizia kuwa Balozi wa Tanzania chini Misri akiiwakilisha Tanzania pia katika nchi za Lebanon, Palestine, Libya, Iraq, Syria and Jordan.

Mwingine anayetajwa ni Dk Khalid Salum Mohammed ambaye ni waziri wa zamani wa Fedha na Mipango wa SMZ.

Dk Mohammed anatajwa kuwa ni msomi na amekuwa katika uongozi kwenye vitengo mbalimbali kwa muda mrefu tangu ukurugenzi, ukatibu mkuu, uwaziri na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi. Pia, anatajwa ni hodari katika kazi zake za utaalamu.

Mwingine anayezungumzwa ni Khamis Mussa Omar ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha wa SMZ ambaye amedumu kwa muda mrefu nafasi hiyo.

Anaaminika katika uongozi wa umma pande zote mbili za muungano na ana uzoefu wa muda mrefu na inaelezwa kuwa si mtu wa papara.

Pia anatajwa Dk Hussein Mwinyi ambaye amezaliwa kwenye familia ya uongozi, na akahudumu katika wizara nyeti kwa muda mrefu.

Kwa sababu hizo, anaelezwa kuwa na mtaji wa kisiasa na kwa kufanya kazi sehemu nyeti kwa muda mrefu, kunampata nafasi ya kuaminika.

Mwingine anayetajwa ni Balozi Mohamed Ramiya ambaye kwa sasa ndiye Waziri wa Fedha wa SMZ.

Mwanasiasa mwingine anayetajwa ni Zubeir Ali Maulid alizaliwa mwaka 1968 ambaye kwa nafasi yake ya Spika wa Baraza la Wawakilishi unampa nafasi kubwa.

Kinachompa nguvu ni kwamba anazijua siasa za Zanzibar na anaungwa mkono na sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Katika orodha hiyo yumo kijana Hamad Yussuf Masauni ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani aliyezaliwa mwaka 1973.

Anatajwa kuwa amekulia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), maana yake anazijua siasa za CCM na ana marafiki wengi.

Orodha hiyo pia inamhusisha Ayoub Mohammed Mahmoud ambaye kwa sasa ni mkuu wa mkoa wa Kusini Unguja.

Nguvu yake inatajwa kuwa ni ushawishi alionao kwa baadhi ya makundi ya vijana wa CCM hasa maeneo ya mijini Unguja na Pemba.

Mwanasiasa muda mrefu katika siasa za Zanzibar Mohamed Aboud ambaye alizaliwa mwaka 1960 haye hakuachwa nyuma.

Anatajwa kuwa pamoja na uzoefu wake, mwaka 2010 alikuwa mmoja wa wagombea urais wa Zanzibar.

Zuio la CCM

Wanasiasa hao wamebaki kutajwa tu mitandaoni ambako hata mijadala juu yao hufanyika.

Hii ni baada ya vikao vya juu vya CCM kupiga marufuku harakati hizo kufanyika kabla ya muda wake.

Hata hivyo, kampeni za chinichini Zanzibar haziepukiki kutokana na nafasi hiyo kuwa wazi baada ya Dk Shein kufikia mwisho wa muhula wake.

Dk Shein hakuweza kuivumilia hali hiyo, aliona imeanza mapema wakati yeye bado yuko madarakani. Aliwaonya makada walioanza kampeni kabla ya muda, huku kiwataka watambue kwamba yeye bado ni Rais wa Zanzibar.

Kama hiyo haitoshi, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliwatahadharisha wanachama hao akisema watachukuliwa hatua za nidhamu.

Hali ya watu kutajwa kutaka kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar ilikumba pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye naye hakuivumilia hali hiyo na kuamua kutoka hadharani kusema hana nia ya kuwania urais wa Zanzibar.

Samia anasema taarifa zinazoenezwa na watu ambao hakuwataja, kuwa anataka kuwania nafasi hiyo zipuuzwe kwa kuwa wadhifa alionao kwa sasa ni zaidi ya urais wa Zanzibar.

“Kuna maneno kwamba Samia anakuja kugombea urais Zanzibar, nataka kuwaambia kuwa si kweli na sina nia hiyo. Ukiangalia ngazi za uongozi ndani ya Tanzania mimi ni namba mbili, sina kinachonishawishi nije kugombea huku (Zanzibar) niwe namba tatu,” alinukuliwa katika moja ya mikutano yake huko Pemba.

“Nimeona niseme huku kwetu (Zanzibar) nilipotoka kwa sababu maneno yamekuwa mengi. Chuki nyingi, ufisadi, majungu ila kwa Samia mimi simo.”

Hivi karibuni, naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma Mabodi anasema CCM haitamchagua mgombea anayetokana na makundi yaliyomo ndani ya chama hicho.

Dk Mabodi anasema suala la wagombea urais Zanzibar huwa linashabikiwa sana na wapambe na “kuna wengine wanatajwa tu hata wao hawafahamu. Zanzibar wapambe wana nguvu sana kuliko wagombea wenyewe.”

Anaongeza kuwa “unajua utakuta mtu anatajwa kwamba anataka kuwania urais lakini mkimuuliza anasema hajui lolote,” anasisitiza.

Dk Mabodi anasema mwaka juzi kulikuwa na wimbi la wapambe waliokuwa wakipita kunadi wagombea wao, lakini baada ya onyo la kamati kuu pia onyo lililotolewa na Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na lile lililotolewa na Dk Shein alipozungumza na mabalozi wa nyumba kumi imesaidia kutuliza hali.