Mbowe aonya ya serikali za mitaa kutojirudia

Mbunge wa Jimbo la Hai, (Chadema) Freeman Mbowe.

Hai. Mbunge wa Jimbo la Hai, (Chadema) Freeman Mbowe, amewataka wananchi kukataa kuchaguliwa viongozi na kuhakikisha yale yaliyojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa hayajirudii katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika Uwanja wa Kware, Masama Kusini, wilayani Hai.

Mbowe alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba, mwaka jana viongozi walipitishwa kwenye mchakato ambao hakuendeshwa kwa haki jambo ambalo halikuzingatia demokrasia.

Aliwataka wananchi wa jimbo lake la Hai kutotoa ushirikiano kwa viongozi hao wa serikali za mitaa kutokana na kutochaguliwa katika mchakato huru na unaozingatia haki.

“Msilazimishwe kuletewa viongozi, chagueni viongozi, tatizo CCM wanaogopa uchaguzi na hiki ndicho kinachowatesa, wanaogopa upinzani kwa kuwa umeimarika nchi nzima, wanajua wakienda kwenye sanduku la kura wanashindwa.

“Mnalalamika mwenyekiti, hatukumchagua, inawezekana huyo mwenyekiti ni mwema sana, lakini mfumo uliomchagua haukuwa wa haki na haukufuata demokrasia, uhalali wa yule mwenyekiti unapotea, lakini ingekuwa mmemchagua kwa utaratibu uliokuwa wa haki hata kama ni wa CCM safi tu, au Chadema au chama chochote ni sawa tu,” aliongeza Mbowe.

“Watasema Mbowe unafanya uchochezi, hapana ni wajibu wangu, kwani sikuja hapa kuimbisha mapambio ya injili, nimekuja kujenga ujasiri kwa wananchi wangu waweze kuidai haki, kwani viongozi hawa wa serikali za mitaa watapata wapi nguvu ya kuwaongoza wakati hamkuwachagua,” alieleza.

Mbowe alisema wanataka uchaguzi wa vijiji, mitaa na vitongoji, urudiwe ili wananchi wawachague viongozi wanaowataka wao na siyo kulazimishwa.

Katika hatua nyingine, Mbowe amekumbushia Bunge kuonyeshwa mubashara kwenye televisheni na kusema kuwa serikali inayojiamini inaruhusu mikutano ya Bunge kuonyeshwa ili wananchi waone mijadala mbalimbali bungeni.

Mbowe aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Snow View, mji mdogo wa Bomang’ombe uliopo wilaya ya Hai.

Aidha Mbowe alisema kuzuiwa kuonyeshwa kwa mikutano hiyo mubashara ni kuminywa kwa demokrasia na uwazi katika utawala bora.