Mbowe atoa kauli wanaotaka nafasi yake

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameweka bayana msimamo wake kuhusu hali inayoendelea ndani ya chama hicho, hasa kuhusu nafasi ya uenyekiti, akisema hana tatizo na yeyote anayetaka nafasi hiyo ilimradi utaratibu ufuatwe.

Mbowe pia amesema angependa vijana wengi wajitokeze kuwania nafasi hiyo baada ya mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe kutangaza nia ya kugombea uenyekiti huku kukiwa na mjadala kuhusu muda wa miaka takriban 15 ambao mbunge huyo wa Hai amekuwa madarakani.

Mbowe (58) amejikuta katika wakati mgumu katika miaka ya karibuni, akipata changamoto kutoka nje na ndani; biashara na mali zake zikikumbana na mkono wa dola, huku kukiwa na chokochoko kutoka kwa watu ambao hawajajiweka bayana wanaohoji ukomo wa muda wake.

Lakini juzi, Mbowe ambaye ameiongoza Chadema tangu mwaka 2004, hakuonekana kuyumbishwa na hali hiyo.

“Sina shida kabisa kwa wanaojitokeza kugombea, lakini pia ni vema wakajua taratibu za chama zinataka nini mtu anapotaka kugombea nafasi ndani ya chama ikiwemo hiyo ya uenyekiti,” alisema Mbowe katika mahojiano na Mwananchi.

“Kama Chadema, hatupo tayari kuendesha chaguzi zitakazoleta vurugu isipokuwa (zinazoleta) mshikamano na kukifanya chama chetu kiendelee kusonga mbele kama chama kikuu cha upinzani.”

Hata hivyo, hakutaka kuweka bayana msimamo wake kuhusu kutetea nafasi hiyo, akisema ni mapema mno na kwamba muda utakapofika ataeleza uamuzi wake.

Chadema ilikuwa iendeshe uchaguzi wake mkuu mwezi uliopita, lakini Kamati Kuu ikaahirisha kutokana na mazingira ya kisiasa ambayo yamekuwa hayaruhusu vyama katika ngazi za chini kuendesha shughuli zake.

Suala hilo liliifanya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutaka maelezo ya maandishi kuhusu Chadema kukiuka Sheria ya Vyama na katiba yake. Tayari Chadema wameshamjibu Msajili wakitoa hoja sita, ikiwemo ya Jeshi la Polisi kuwa moja ya sababu za wao kuchelewa kufanya uchaguzi wao mkuu.

“Mara zote ambazo uchaguzi wa ndani ulikuwa ufanyike, chama kilipata vikwazo kwa kuzuiwa na Jeshi la Polisi na kulazimika kusimama na kuahirishwa,” inasema barua ya Chadema iliyosainiwa na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji

Wakati hayo yakiendelea kumekuwa na mijadala kuhusu uenyekiti wa Mbowe, baadhi wakihoji sababu za kuendelea kushikilia nafasi hiyo, na wengine wakitoa tuhuma za ubadhirifu.

Baadhi wanasema pamoja na mchango wake mkubwa wa kukiwezesha chama hicho kukua-alikuta kikiwa na wabunge 11 na mwaka 2015 kukiwezesha kuingiza wabunge 70- wanaona muda wa kuumzika na kuwaachia wengine umefika.

Mbali na mjadala huo, changamoto nyingine ambayo anahangaika nayo ni kesi, ikiwemo inayoendelea sasa aliyoshtakiwa na viongozi wengine wanane, kesi ambayo ilimfanya akae mahabusu zaidi ya miezi mitatu. Pia amekuwa akisumbuana na mamlaka kuhusu biashara na mali zake, kuondolewa katika jengo la Shirika la Nyumba na vifaa vyake katika klabu ya usiku ya Bilicanas kupigwa mnada kutokana na masuala ya kodi, huku akishindwa kufanya mikutano jimboni kwake. Katika mahojiano na Mwananchi, Mbowe alizungumzia suala la kufuata taratibu kwa wanaotaka kuwania uenyekiti.

Kwa mujibu wa ibara ya 6.3.1(a), “uchaguzi wa viongozi utazingatia taratibu na sifa za uongozi kama zilivyofafanuliwa katika kanuni za chama”.

Kanuni hizo ndizo zinazozungumzia muda wa kuchukua fomu, kufanya kampeni na mambo mengine kuhusu uchaguzi.

Mbowe alichukua uenyekiti wa Chadema mwaka 2004 na mwaka uliofuatia aligombea urais, akisimama awali na Jumbe Rajab Jumbe ambaye baadaye alifariki na uchaguzi kusogezwa mbele.

Chadema ilimteua Anna Maulidan Komu kuwa mgombea mwenza na Mbowe akashika nafasi ya tatu, akipata asilimia 5.88 ya kura. Tangu wakati huo, Mbowe ameibukia kuwa na nguvu ndani ya Chadema na kufanikiwa kukijenga kuwa chama kikuu cha upinzani.

Katika uongozi wake Chadema imekuwa na harakati tofauti za kuhamasisha wananchi, zikiwemo programu kama “Movement for Change”, “Operesheni Sangara”, “Chadema ni Msingi” na baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 walianzisha ngazi ya uongozi katika kanda.