Mbunge Katani ‘amfuata’ Harmonize jimbo la Tandahimba

Dar es Salaam. Miezi minne baada ya Rais John Magufuli kutamani msanii wa Bongofleva, Rajab Abdul maarufu Harmonize kuwa mbunge wa Tandahimba, mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF, Katani Katani amejiunga CCM.

Katani amechukua uamuzi huo jana mkoani Mtwara katika kikao cha ndani cha CCM kilichofanyika jimbo la Nanyamba, Mtwara Vijijini na kuongozwa na katibu mkuu wa chama hicho tawala, Dk Bashiru Ally.

Oktoba 15, mwaka jana Rais Magufuli katika mkutano wa hadhara mjini Ruangwa mkoani Lindi alisema anatamani Harmonize awe mbunge.

Alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara ambao Harmonize alitumbuiza, “sijui Harmonize anatoka jimbo gani, anatoka Tandahimba? Mbunge wa kule (Tandahimba) ni nani? Aaah ningetamani kweli Harmonize akagombee kule akawe mbunge wa Tandahimba.”

Kwa uamuzi huo, Katani anakuwa mbunge wa 12 wa upinzani kujiunga na CCM tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wabunge 11 wa upinzani waliojiunga CCM walipitishwa na chama hicho kuwania tena ubunge na kuibuka na ushindi.

Wabunge hao ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Dk Godwin Mollel (Siha), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati Mjini), Marwa Chacha (Serengeti), Joseph Mkundi (Ukerewe), Abdallah Mtolea (Temeke), Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara (Ukonga), Zuberi Kuchauka (Liwale) na Cecil Mwambe ambaye hawezi kuwania ubunge kutokana na muda wa kufanyika uchaguzi mdogo kupita kwa mujibu wa katiba.

Taarifa kutoka kikao hicho cha ndani zilieleza kuwa Dk Bashiru aliwaeleza viongozi wa mashina, matawi na kata kuwa wengi watajiunga na chama hicho kwa kuwa kimejiimarisha na kufuata misingi ya kuanzishwa kwake. Alisema kinazingatia demokrasia na kufanya mambo yanayowagusa wananchi.

“Dk Bashiru alisema tangu uanzishwaji wa vyama vingi CCM ni chama kilichowahi kuwa na wenyeviti watatu jambo ambalo ni tofauti na vyama vingine vyenye mwenyekiti huyo huyo miaka yote. Alisema wananchi wanaona uhalisia huo na wanajua,” kilieleza chanzo chetu kutoka katika mkutano huo.

Mwananchi lilimtafuta Katani bila mafanikio kwani namba yake ya simu iliita bila majibu.