Mbunge ataka Chadema kifutwe

Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, akichangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Makadiro ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Temeke Nchini Tanzania (CCM), Abdallah Mtolea amehoji kwanini Msajili wa Vyama vya Siasa nchini haifuti Chadema kutokana na siasa za fujo na chuki wazozifanya.

Dodoma. Mbunge wa Temeke Nchini (CCM), Abdallah Mtolea amehoji kwanini Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini haifuti Chadema kutokana na siasa za fujo na chuki wanazozifanya licha ya kupewa meno na sheria iliyopitishwa na Bunge.
Mbunge huyo amehoji hayo leo Ijumaa Aprili 3, 2020 wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
“Mwaka jana tuliboresha sana sheria ya vyama vya siasa na kumpa nguvu sana na meno katika kuvisimamia vyama vya siasa nchini.
“Sasa ni lini msajili wa vyama vya siasa atakuwa amejiridhisha kwamba matukio ya fujo, siasa za chuki kuamshwa mihemko ya hasira kwa wananchi zinazofanywa na Chadema kuwa ni sababu za kutosha kukifuta chama hiki,”amesema.
Amesema chama hicho kimesababisha fujo nyingi na miongoni ni fujo zilizosababisha kifo cha mwanafunzi Akwilina kilichotokea Februari 16, 2018 baada ya kukataa amri halali ya polisi.
Hata hivyo, amesema chama hicho hakionyeshi kujutia jambo hilo na kwamba walitegemea baada ya hukumu ya mahakama wangelitoka kwenda kuipa pole familia ya marehemu lakini wao wakafanya vikao vya kisiasa na waandishi wa habari.
“Wakafanya vikao vingi wakilia kwa furaha wakati wao wakilia kwa furaha mama wa marehemu Akwilina analia kwa uchungu. Mama yake Akwilina hana mtu wa kumfuta machozi. Kama sisi sio wa kumsemea ni nani aliyemsemea,”amesema.
Amesema mbwembwe za kuchanganishana fedha hazikuwa zikifanywa dhidi ya CCM wala Serikali bali ni dhidi ya mama yake Akwilina ambaye amepoteza mtoto.
“Mambo haya kama msajili wa vyama vya siasa anayaangalia tu, tunakwenda wapi? Nikumbushe hatua za kuachana na ubinadamu wanazifanya kila siku,”amesema.