Mbunge wa CCM amwambia waziri atalaaniwa

Mbunge wa Ulanga  (CCM),Goodluck Mlinga akichangia mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Ulanga Nchini Tanzania (CCM) Goodluck Mlinga amemtadharisha Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama kuwa wazee 57 wa jimbo lake wanaodai kiinua mgongo kwa miaka miwili sasa watamlaani.

Dodoma.  Mbunge wa Ulanga Nchini Tanzania (CCM) Godluck Mlinga amemweleza Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Jenista Mhagama kuwa wazee wa Ulanga wanaodai mafao yao kwa miaka miwili mfululizo bila mafanikio watamlaani.
Akichangia katika bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2020/2020, Mlinga amesema walimu
57 wa jimboni mwake wamestaafu tangu mwaka juzi lakini hawajapata kiinua mgongo cha wala hawapati pensheni.
“Hebu ‘imagine’ mtu alifanya kazi miaka 30 alizoea kila mwezi anapata mshahara leo hii ana mwaka wa pili hapati pensheni yake ya kila mwezi wala kiinua mgongo chake,”amesema.
Amesema yeye kama mbunge ameenda ofisi ya kanda Morogoro lakini hakupata majibu badala yake ameambiwa aende mkoani Dodoma ndipo yalipo makao makuu.
“Huo ni uhakiki gani mnafanya? Mtakuja kuwaua wazee. Wametaka kufika kwenye Bunge hili nimewaambia hapana wageni hawaruhusiwi. Wamesema bora wafe na corona kuliko kufa na njaa,”amesema.