Miaka mitatu Tanzania yapoteza lita bilioni 1.4 za petroli, kodi

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (Ewura) imeshindwa kuthibitisha matumizi ya lita bilioni 1.4 zilizoingia nchini kwa miaka mitatu huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikikosa mabilioni ya kodi na tozo ya nishati hiyo.

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2018/19, Mdhibti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere anasema Ewura haikuzitumia ipasavyo kanuni zake za udhibiti hivyo kushindwa kung’amua matumizi ya lita hizo za petroli.

Mkaguzi huyo alisema utaratibu wa udhibiti unataka bidhaa zote za petroli zilizoingizwa nchini kwa matumizi ya ndani kuthibitishwa na kuwekwa alama isipokuwa zilizosamehewa kodi.

“Hata hivyo, katika kupitia ripoti ya utendaji kwa bidhaa zilizoingizwa nchini kati ya mwaka 2015/16 na 2018/19, nilibaini tofauti ya lita bilioni 1.4 kati ya bidhaa zilizothibitishwa na zilizoingia nchini kwa matumizi ya ndani,” anasema Kichere kwenye ripoti yake aliyoiwasilisha bungeni jana.

Pia, anasema amebaini mamlaka hiyo haina utaratibu unaoiwezesha kugundua chanzo cha tofauti iliyoonekana.

Pamoja na rasilimali za umma ilizonazo Ewura, CAG amesema tofauti iliyoonekana inaashiria udhaifu katika ufuatiliaji wa bidhaa zinazoingia nchini kwa matumizi ya ndani, jambo linaloweza kusababisha upotevu wa mapato.

“Napendekeza menejimenti ya Ewura iweke utaratibu utakaowezesha kufuatilia na kupatanisha taarifa za bidhaa zilizoingia kwa matumizi ya ndani kwa usimamizi na udhibiti madhubuti,” anashauri.

Vilevile, CAG Kichere ameeleza kubaini mapungufu katika ukusanyaji wa kodi.

Katika ripoti ya ukaguzi wa Serikali Kuu anasema hakuna udhibiti wa kuridhisha katika ukusanyaji wa kodi kwenye mafuta yanayoingia na kutumika nchini.

Katika ukaguzi huo, CAG amesema alibaini zaidi ya Sh124.69 milioni zilizokadiriwa kwenye mafuta kwa ajili ya ushuru wa forodha hazikulipwa na kampuni husika za uuzaji nishati hiyo kutokana na ufuatiliaji usioridhisha wa maofisa wa TRA.

Vilevile, CAG anasema baada ya kupitia taarifa za mafuta yaliyoingizwa nchini alibaini nyaraka 11 za zaidi ya lita milioni 11.68 ambayo licha ya kuingizwa kwenye mfumo wa forodha hayakukadiriwa kodi.

Kutokana na hali hiyo, CAG amesema kodi na ada za bandari zaidi ya Sh3.57 bilioni hazikukusanywa na TRA.

CAG ameishauri Serikali kuimarisha udhibiti wa usafirishaji na utoaji wa bidhaa bandarini ikijumuisha kuthibitishwa katika mfumo wa forodha kwa bidhaa zinazokwenda nje ya nchi.

Udhaifu mwingine alioubaini CAG katika usimamizi na udhibiti wa uingizaji na matumizi ya mafuta nchini ni kutokusanywa kwa riba ya ucheleweshaji wa kodi.

Kuhusu ukadiriaji na ukusanyaji wa mapato kwenye mafuta yaliyoingizwa kwa matumizi ya ndani na yaliyokusudiwa kusafirishwa kwenda nje ya mipaka, amesema kulikuwa na ucheleweshaji wa malipo ya kodi za forodha na hakuona ushahidi kuthibitisha ukusanyaji wa riba ya zaidi ya Sh1.36 bilioni.

“Kutokukusanya riba hii kunaikosesha Serikali mapato.”