Mitazamo ya Mwalimu Nyerere kuhusu uchumi

Muktasari:

Alikuwa na mitazamo inayofahamika kiuchumi, kisiasa na katika baadhi ya mambo ya kijamii.

Kila Oktoba 14 ni siku ya kumkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa namna ya pekee.

Kwa wanaomfahamu Mwalimu Nyerere hamna haja ya kutoa maelezo zaidi.

Kwa wasiokuwa na bahati ya kumfahamu, hamna maneno ya kutosha ya kumuelezea. Mwalimu Nyerere alikuwa na mitizamo mbalimbali kuhusu mambo kadha wa kadha.

Alikuwa na mitazamo inayofahamika kiuchumi, kisiasa na katika baadhi ya mambo ya kijamii.

Makala haya ni mahususi katika jitihada za kumuenzi mwalimu.

Umiliki wa uchumi

Kati ya mambo yanayomtambulisha Mwalimu Nyerere kuhusu umiliki wa uchumi ni siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha la mwaka 1967.

Mwalimu aliamini katika uchumi ambao njia kuu za kuzalisha mali zinakuwa chini ya umiliki wa Serikali. Njia hizi ni pamoja na viwanda, mashamba makubwa, migodi, benki, hoteli na kadhalika.

Hili linaonekana katika Azimio la Arusha pale ulipofanyika utaifishaji wa njia kuu za uchumi.

Njia hizi zilitoka katika mikono binafsi na kuwekwa katika mikono ya Serikali. Aliamini katika uchumi hodhi wa Serikali. Sekta binafsi kama tunavyoielewa leo haikuwa na nafasi kubwa katika uchumi wa nchi enzi za mwalimu. Mali za sekta binafsi zilitaifishwa.

Baadhi ya mitizamo ya mwalimu kuhusu umiliki wa uchumi hasa uchumi hodhi wa Serikali haionekani kuwa na nafasi kubwa kwa mazingira ya leo.

Baada ya mageuzi makubwa ya kisiasa na kiuchumi katikati ya miaka ya 1980 mitizamo hii ya mwalimu haikuendelezwa na viongozi waliopokea madaraka baada yake. Mageuzi ya kiuchumi yalibadili uchumi hodhi wa Serikali na kuwa uchumi shindani wa sekta binafsi. Majukumu ya Serikali yalibadilika kuwa majukumu ya kuweka mazingira rafiki, wezeshi na ya kuvutia ya sekta binafsi kuwa injini ya uchumi.

Tofauti na mitizamo ya mwalimu, mali zilizokuwa zimetaifishwa zilibinafsishwa.

Kujitegemea

Mwalimu aliamini katika watu na nchi kujitegemea kiuchumi. Hii inatokana na kuelewa changamoto za nchi kuwa tegemezi kiuchumi.

Changamoto hizi ni pamoja na masharti magumu na wakati mwingine yasiyokubalika, misaada kutotolewa kwa wakati na kiasi kama inavyoahidiwa, nchi kutokuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yake ikiwemo baadhi ya mambo ya kisera, kisheria na kiudhibiti.

Ili kutimiza azma ya kujitegemea kama nchi katika mazingira ya leo Tanzania, ni muhimu kwa nchi kukusanya kodi ya kutosha. Kodi husaidia Serikali kuwa na vyanzo vyake vya ndani vya mapato, hivyo kupunguza utegemezi wa misaada na kero zinazotokana na utegemezi huu.

Uchumi wa viwanda

Mwalimu Nyerere aliweka misingi ya mambo mengi ikiweamo ile ya uchumi wa viwanda.

Wakati tukiwa katika azma mpya ya uchumi wa viwanda, ni muhimu kukumbuka kuwa mwalimu alifanya mengi kuhusu viwanda. Wakati wa enzi zake mipango kadhaa ya maendeleo ilitoa vipaumbele katika uchumi wa viwanda.

Hii ni mipango ya kuanzia miaka michache baada ya uhuru hadi mwishoni mwa miaka ya 1970.

Pamoja na mambo mengine, mwalimu aliamini katika viwanda vidogovidogo, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, viwanda vya kuongeza ajira kupitia kufanya kazi wa mikono zaidi kuliko kwa mitambo.

Pia, mikakati ya mwalimu kuhusu uchumi wa viwanda ni pamoja na kuwa na viwanda vya kuzalisha bidhaa ambazo zingechukua nafasi ya zile zilizokuwa zikiingizwa kutoka nje ya nchi.

Katika zama hizi za kuwa na uchumi wa viwanda, itakuwa muhimu kujifunza na kuchota katika fikra za mwalimu kwa kutazama nini kilifanikiwa na ambacho hakikufanikiwa na kwanini.

Pale ambako fikra zake kuhusu uchumi wa viwanda hazikufanikiwa itakuwa muhimu kujua kwanini.

Kulinda wazalishaji

Kati ya maandishi ya Mwalimu Nyerere ni yale yanayohusu kulinda wazalishaji wa ndani ya nchi dhidi ya ushindani.

Mwalimu alitambua vizuri kuwa wazalishaji wadogo wa ndani lazima walindwe dhidi ya ushindani kutoka nje kama nchi inataka kuwapa wazalishaji wake wa ndani nafasi ya kukua.